Mapitio bei ya CNG, watalaamu wa uchumi watia neno
- Waonya ongezeko la bei linaweza kuwafanya watumiaji kurejea petroli na dizeli.
- Ewura kufanya mapitio ya bei na viwango vya faida baada ya miaka 15 bila mabadiliko.
Dar es Salaam. Wachambuzi wa uchumi wanaonya kuwa Ikiwa mapitio ya bei ya Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) yanayofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) yataongeza gharama, matumizi ya nishati hiyo yatazorota.
Hayo yanajiri ikiwa ni siku moja tu tangu Ewura itangaze kufanya mapitio ya bei ya CNG iliyosalia kuwa Sh15,000 kwa kilo kwa miaka 15.
Taarifa Mhandisi Lorivii Long’idu, Meneja wa Ewura Kanda ya Mashariki, inabainisha kuwa mapitio hayo yanalenga kuweka mfumo wa bei unaozingatia gharama halisi za uendeshaji, viwango vya faida kwa watoa huduma na uwezo wa wananchi kumudu gharama za nishati hiyo.
Naye Meneja wa CNG, Selemani Chombo, alieleza kuwa mapendekezo hayo ya bei yanatarajiwa kuanza kutumika Desemba 2026 yatazingatia gharama za uendeshaji, mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni pamoja na gharama za kusafirisha gesi kutoka kwenye vyanzo vya uzalishaji hadi maeneo mbalimbali nchini.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) na wadau wa gesi asilia iliyokandamizwa (CNG), wakiwemo watoa huduma na watumiaji, katika semina inayolenga kuongeza uelewa kuhusu usalama, ubora na ufanisi wa huduma za gesi asilia nchini. Picha | Ewura.
Wachumi watia neno
Kufuatia mchakato huo, Mtaalamu wa fedha na uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof Abel Kinyondo, amesema iwapo bei ya CNG itaongezeka na kukaribia gharama za petroli na dizeli, baadhi ya watumiaji wanaweza kuachana na nishati hiyo.
“Wakati vituo vya CNG vinahesabika kwenye vidole. kokote pale hata ukiwa porini, utakuta kituo cha petroli na dieseli. Kwa hiyo kama tofauti ya bei haitakuwa ‘significant’ ilivyo sasa hivi watu watakimbia,” amesema Prof Kinyondo.
Aidha, Prof Kinyondo ameseshauri mapitio ya bei hizo yafanyike kwa kuwazingatia baadhi ya wamiliki wa bajaji, pikipiki na magari madogo waliobadilisha mifumo ya vyombo vyao na kutumia CNG wakikwepa maumivu ya petroli na dizeli.
Ameongeza kuwa gesi asilia ni sehemu ya mchakato wa mabadiliko ya matumizi ya nishati (Energy Transition), unaolenga kupunguza utegemezi wa mafuta ya kisukuku na kuelekea kwenye nishati safi zaidi, ikiwamo umeme.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya uchumi na fedha, Paul Chengula, amesema mapitio hayo ni hatua muhimu kwa kuwa yatasaidia kutathmini gharama na kuweka viwango vya bei vinavyoweza kuwanufaisha watoa huduma bila kuwaongezea mzigo wananchi.
“Ni hatua nzuri kwa sababu wataangalia bei gani inaweza kumfaa mfanyabiashara na wakati huohuo isimwumize mwananchi kiasi cha kuathiri uchumi wake,” amesema Chengula.