Afya ya akili inavyowatesa wanawake kazini
- Shinikizo la kazi na majukumu ya kifamilia vyachochea msongo wa mawazo kwa wanawake.
- Unyanyasaji na ubaguzi kazini bado ni jeraha kwa afya ya akili ya mwanamke.
Dar es Salaam. Kila siku Gloria Simba huamka asubuhi na mapema tayari kwa ajili ya kukabili majukumu yake ya kila siku yanayomfanya awe na maisha ya pande mbili.
Katika upande mmoja Gloria (37) ni mama wa watoto watatu wanaohitaji uangalizi wa karibu na upande mwingine ni mfanyakazi katika moja ya ofisi zenye shughuli nyingi jijini Dar es Salaam.
Kwa zaidi ya miaka nane mwanamke huyo amekuwa akijitahidi kuishi maisha hayo bila kulalamika akimini kwamba ndivyo fungu alilopangiwa, suala linalogharimu afya yake ya akili.
“Majukumu yanapozidi huwa napata msongo wa mawazo…inafikia hatua natamani hata kuacha kazi lakini siwezi,” anasema Gloria.
Wengi wanaopata msongo wa mawazo kutokana na presha za kazi hawashirikishi wengine wakiwemo viongozi, marafiki au wasaikolojia kwa ajili ya kuwasaidia.
Baadhi wanaamini sehemu kubwa ya wanaoshirikishwa hawana siri na kuvujisha madhila yanayowakumba.
Wakati Gloria akipambana kuhakisha majukumu ya kazini na familia yanatimizwa bila mawaa, Chiku Sijaona mkazi wa jijini Tanga anasema ni ngumu kuwashirikisha watu wa karibu changamoto za afya ya akili anazozipita kazini hali inayoongeza ukubwa wa tatizo hilo.
“Si rahisi kumshirikisha mtu changamoto zako za kiafya kazini. Unaweza kumwambia mtu jambo leo, kesho likawa gumzo kwenye korido. Hivyo, wengi wetu tunabaki kimya,” anasema Chiku.
Wanawake hao ni miongoni wa watu bilioni moja wanaokumbana na matatizo ya afya ya akili duniani huku asilimia 15 kati yao wakiwa ni wafanyakazi kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani(WHO).
WHO inaeleza kuwa changamoto ya afya ya akili huwaathiri zaidi wanawake wakiwa ni zaidi ya nusu ya waathiri wakiwa ni asilimia 53.1 ukilinganisha na wanaume (kwa asilimia 46.9). Hali hiyo, WHO inaeleza kuwa huchangiwa zaidi na msongo wa mawazo, mazingira ya kazi yasiyofaa na mlundikano wa majukumu.
“Siku bilioni 12 za kazi hupotea kila mwaka duniani kutokana na msongo wa mawazo na wasiwasi, hali inayosababisha hasara ya takribani Dola za Marekani trilioni 1 kutokana na kupungua kwa uzalishaji,” inasema WHO.
Kazi nyingi ujira duni
Ripoti ya mwelekeo wa jinsia na soko la ajira nchini Tanzania iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mwaka 2021 inabainisha kuwa kumekuwa na mwitikio chanya wa wanawake nchini Tanzania katika soko la ajira suala linaloongeza ujumuishi wa kiuchumi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo asilimia 86.2 ya wanaume wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea nchini Tanzania wapo katika soko la ajira huku wanawake wakiwa asilimia 80.3.
Hii inamaanisha katika kila wanawake 100, 80 wapo katika soko la ajira katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, huduma na viwanda .
Pamoja na mwelekeo huo chanya uliobainishwa, ripoti ya NBS pamoja na ile ya uchambuzi wa hali ya usawa wa kijinsia nchini Tanzania inayotolewa na Benki ya Dunia (WB) zinabainisha bado kundi hilo halipewi fursa sawa katika soko la ajira. Wengi, ripoti hizo zinabainisha huambulia nafasi za chini na ujira duni usiokidhia gharama za maisha jambo ambalo huchangia zaidi kuathiri afya zao za akili.
Chiku ambaye pia ni mfanyakazi katika taasisi binafsi jijini Tanga ameiambia Nukta Habari kuwa licha ya kufanya kazi kwa muda mrefu bado ujira anaolipwa haukidhi mahitaji.
“Unakuta unatumia muda mwingi kazini, kazi unafanya nyingi lakini maslahi yanakuwa madogo, wakati gharama za maisha zinaongezeka kila siku inaumiza sana,” anasema Chiku.

‘Stress juu ya stress’
Kutokana na hali hiyo, mara nyingi Chiku hujikuta akipoteza ufanisi wa kufanya kazi zake kwa usahihi zaidi ya kujikuta anafanya tu ili kukimbazana na muda, huku akifikiria namna ya kutatua shida za familia.
Hata baada ya wanawake hao kutoka kazini bado hutegemewa kufanya majukumu mengine ya nyumbani licha ya uwepo wa wasaidizi wengine pamoja na wenzi wao suala linaloshusha uwezo wao wa kufanya kazi katika siku inayofuata.
Ripoti ya NBS inaeleza kuwa wanawake hutumia saa nne hadi sita kufanya shughuli za nyumbani licha ya kufanya shughuli nyingine zinazowaingizia kipato ukilinganisha na saa moja ambao wanaume huitumia kufanya kazi hizo.
Wataalamu wa afya wanasema katika nyakati zenye presha za kikazi na maisha kama hizi ni vema wanawake wakajitahidi kulinda afya zao za akili kupata ustawi wa kijamii na kiuchumi.

Tunachokijua kuhusu afya ya akili
Daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili, Silvia Ngonyani wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, anasema afya ya akili ni hali ya ustawi wa kisaikolojia inayomwezesha mtu kukabiliana na changamoto za maisha, kutumia uwezo wake kikamilifu, kufanya kazi kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya afya ya Appolo hospitals ya India, magonjwa ya afya ya akili husababishwa na asili, changamano inayohusisha mwingiliano wa mambo ya kimazingira na kibaolojia.
Tovuti hiyo inabainisha kuwa, baadhi ya tafiti zinaonesha kuwa maambukizi ya virusi wakati wa ujauzito, kama mafua, mfiduo wa sumu kama metali nzito au dawa za wadudu yanaweza kuchangia kuibuka kwa changamoto za afya ya akili.

Sababu nyingine ni urithi wa vinasaba, ambapo historia ya familia yenye matatizo ya afya ya akili huongeza uwezekano wa mtu kuathirika, jambo linaloashiria mchango wa urithi wa vinasaba.
Hata hivyo, tovuti ya Cleveland clinic inaeleza, kuwa vinasaba hivyo hakumaanishi lazima utaendeleza ugonjwa huo.
Wanawake wapigika zaidi kuliko wanaume
Ingawa mwanaume anaweza kupata matatizo ya msongo wa mawazo, Dk Theresia Mwanjala, mwanasaikolojia kutoka Hospitali ya Saifee jijini Dar es Salaam, anasema upande wa mwanamke hatari huwa kubwa zaidi kutokana na mwingiliano wa majukumu mengi anayobeba kila siku.
“Mwanamke anapokuwa kazini anapaswa kutekeleza majukumu yake ya kikazi kwa ufanisi, lakini wakati huohuo bado anawaza na kupanga masuala ya nyumbani kuhakikisha familia inaendelea vizuri,” anasema.
Baada ya kutoka kazini, mwanamke hurudi nyumbani na kuendelea na majukumu ya familia kama kuwahudumia watoto na kusimamia mahitaji ya nyumbani.
Hali hii, anasema humfanya mwanamke ashindwe kupata muda wa kujijali, kupumzika, kulala vya kutosha, kufanya mazoezi, au hata kupata muda mdogo wa starehe binafsi.
Aidha, anaongeza kuwa pamoja na majukumu ya kazi na familia, pia kuna majukumu ya kijamii kama kuhudhuria misiba, harusi na shughuli nyingine, ambayo huongeza mzigo zaidi. Kutokana na hali hii, mwanamke hukosa muda wa kufanya mambo muhimu ya kujitunza kama kula vizuri, kupumzika, na kuwa karibu na ndugu na marafiki mambo ambayo ni muhimu kwa kulinda afya ya akili.

Rushwa ya ngono ni mtihani
Dk Silvia anaeleza baadhi ya wanawake hukumbana na masharti ya kingono, wakati ambao wanapotafuta au wanapokuwa kazini jambo ambalo linawaweka hatarini kukumbana na changamoto ya afya ya akili.
“Wengine wako kwenye ndoa anatafuta kazi, huku mwajiri huyo anamwambia naomba unipe kitu hiki. Mtu anawaza nawezaje kutoka kwenye ndoa yangu kwa sababu nataka kazi alafu kutoa mwili wangu kwa ajili tu ya kazi,” anaeleza Dk Ngonyani.
Wapo wanaoingia katika mahusiano ya kulazimishwa kwa hofu ya kupoteza ajira, Dk Ngonyani anaongeza, na baadaye kuishi katika sintofahamu, hatia, hofu ya maradhi au kuvunjika kwa familia.
Hali hii humweka mwanamke katika mgongano wa maadili, ndoa na heshima binafsi jambo ambalo huenda akashindwa kulitatua kwa muda mrefu.
Ukiacha na masuala ya ngono, Professa wa Chuo Kikuu cha Thompson cha Marekani, Katrina Daly anasema aliwahi kukutana na ubaguzi uliomfanya kuhisi kudhulumiwa haki yake baada ya kushutumiwa jambo ambalo hakulifanya.
“Tukio hilo lilinisumbua kwa muda,” anaeleza Daly.
Usikose kusoma sehemu ya pili ya mfululizo wa makala hii kesho…