Matatizo ya afya ya akili: Kaburi jipya la wanandoa-2

July 6, 2022 6:45 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Mtu kufanya vitu visivyo vya kawaida inaweza kuwa dalili ya matatizo ya akili.
  • Wataalam washauri watu waende hospitali kupima.
  • Serikali, wadau kukaa chini kutafuta suluhu ya kudumu.

Utambuaje mtu mwenye matatizo ya afya ya akili?

Dar es Salaam. Mtaalamu wa Saikolojia kutoka mkoani Mbeya, Pulumba Msafiri anaeleza kuwa mtu aliye na ugonjwa wa akili siyo lazima awe kichaa au mwendawazimu kama wengi wanavyodhani kwani hiyo ni hatua ya mwisho ambapo viashiria hupimwa kwa kutazama mwenendo wa maisha wa mtu husika. 

“Watu wengi wanaamini mgonjwa wa akili ni kichaa, kitaalamu hiyo ni hatua ya mwisho, sisi tunatizama zile hatua za mwanzo ambazo zinaweza kuhusisha utendaji hasi katika shughuli zake za kila siku,” anasema mtaalam huyo wa saikolojia. 

Anasema wapenzi wanaweza kutumia baadhi ya viashiria mbalimbali kujua kama wenza wao wana matatizo ya akili ikiwemo kukosa umakini wa shughuli zake za kila siku na kupoteza kumbukumbu.

Pia kukosa uwezo wa kupambanua mambo kwa mitazamo tofauti, kutokujali, kuwa na imani zisizo za kawaida kama vile kuamini kuwa na nguvu ya ziada kutoka nje ya mwili pamoja na kuwa na mawazo yasiyo na mtiririko unaoeleweka. 


Nini kifanyike?

Mtaalamu wa masuala ya afya ya akili, Dk Sylvia Ngonyani anasema  kwanza jamii inapaswa kuelimishwa kuhusiana na umuhimu wa afya ya akili kwani ndiyo msingi wa mambo yote kwa mwanadamu.

“Watu hawaelewi kama afya ya akili ni afya, hauwezi kuongelea  afya bila kutaja afya ya akili kwa sababu kila kitu kwenye mwili wa binadamu kinahitaji akili, sasa akili ikiwa sivyo maana yake vitu vingine lazima vipotee,” anasema.

Hata hivyo, Dk Ngonyani ameshauri jamii kutoa taarifa katika kituo chochote cha afya mara tu wanapobaini mtu anayeonesha mabadiliko ya tabia na kuanza kufanya vitu ambavyo sio vya kawaida. 

“Kitu kinachopaswa cha kwanza, kuwasili katika kituo cha afya chochote ili kueleza matatizo ya huyo mtu kwa sababu kule ndiko ambako unaweza kupata ushauri na kupata matibabu,” anasema Dk Ngonyani.

Kwa mujibu wa mtaalam huyo wa afya ya binadamu, hakuna uhusiano wowote kati ya matatizo ya afya ya akili na imani za kishirikina, hivyo ameitaka jamii kuachana na mtazamo huo mara moja kwani wagonjwa wanaoenda hospitali hupona baada ya kupata matibabu.

Ili kutibu tatizo la afya ya akili hasa kwa watu waliopo kwenye mahusiano kuna umuhimu wa kuwatambua mapema na kuwafikisha katika vituo vya afya. Picha| Verywellmind.

Mwanasaikolojia Msafiri Pulumba ameishauri Serikali kuwawezesha wanasaikolojia binafsi na walioko kwenye asasi za kiraia kwenda  kutoa elimu kwa jamii ili kupunguza madhila ya matatizo ya afya ya akili hasa kwa watu waliopo kwenye mahusiano. 

“Serikali inafanya kwa upande wake lakini haiwezi kumaliza tatizo pekeyake, iangalie kwa jicho la pili wale watu ambao wana taaluma lakini hawajapata fursa ya kujiendesha peke yao kwa sababu kwa namna yoyote ile hatuwezi kukwepa visababishi vya matatizo ya afya ya akili,” anasema  Pulumba.


Viongozi wa dini wanasemaje? 

Mchungaji Yanick Muliri wa kanisa la Ebeneza lililopo Mkoani Iringa anasema vijana wengi wanaingia kwenye ndoa kwa kufuata mkumbo bila kuandaliwa vya kutosha kukabiliana na changamoto watakazokutana nazo ndani ya ndoa.

Anasema changamoto nyingine ya ukatili kwa wanandoa ni jamii kutokuwa na hofu ya Mungu, jambo linalochochea vitendo hivyo, na kuiasa jamii kuwa na hofu ya Mungu ili kuepuka kutenda vitendo viovu. 

“Vijana wengi hawaandaliwi kuingia kwenye ndoa, wanafuata mkumbo akiona  fulani kaoa na yeye anaoa, ndio maana hawana uvumilivu kwenye ndoa unatakiwa uvumilivu pamoja na kusameheana kwa sababu kila mtu anakuja na tabia zake.

“Kikubwa zaidi hofu ya Mungu, watu wakiishi kwa kuwa na hofu ya Mungu hakutakuwa na matukio haya ya mauaji sio tu kwa wenza bali kwa jamii nzima,” anasema Mchungaji Muliri.

Kwa upande wake Sheikh wa Msikiti wa Malimbe uliopo  jijini Mwanza Haidari Maulid anasema kutokana na kila binadamu kuumbwa na wivu, basi utumike katika kumjali mtu pamoja  na kuishi katika mipaka ya Mungu.

“Mafundisho yanatutaka tuwe na wivu kwa wenzi wetu lakini wivu huo ni kwa ajili ya kuwapenda zaidi na kuwasitiri….hivyo wivu upo katika kumcha mwenyezi Mungu.

“Kuua au kujiua ni kinyume na maagizo ya mwenyezi Mungu. Watu waishi katika mipaka ya mwenyezi Mungu kwa kufuata mafundisho yake na kuomba sana, hawawezi kufika hatua ya kutoana uhai,” anasema Sheikh Maulid.


Soma zaidi:


Mikakati ya Serikali 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk Dorothy Gwajima alipokuwa katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ITV hivi karibuni wakati makala hii inaandaliwa alisema ni muhimu kuweka utaratibu wa kuwaandaa wanandoa kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimahusiano kabla hawajafunga ndoa. 

“Tuanze kuwapa hii mitihani itokanayo na matukio yaliyotokea kwenye jamii ikiwezekana twende mpaka kwenye vyeti kwamba hawa sasa wameiva…wanajua matatizo na changamoto na wanajua jinsi ya kutoka,” alisema Dk Gwajima.

Amesema lazima jamii ielimishwe ijue kuwa hili tatizo lipo na limechukua maelfu ya watu na linaweza kumpata mtu yeyote ambapo namna nzuri ya ni kupewa miongozo wanapoingia kwenye ndoa.

Hata hivyo,  Waziri Gwajima amesema bado kuna ombwe katika jamii ambapo wanajamii wanaona kuna tatizo lakini bado wanakumbatia kwa kuona ni kitu cha kawaida akirejea kisa cha mauwaji ya wanandoa Mwanza ambapo inaelezwa Swalha alishawahi kupigwa na kitako cha bunduki lakini hakuripoti popote ambapo angeweza kusaidiwa. 

“Bado kuna ombwe fulani, unalijua tatizo alafu hutaki kukubali kuwa hili ni tatizo na nichukue hatua hizi au hujui uchukue hatua gani lakini unaliona ni tatizo kwa hiyo hili ni eneo ambalo lazima tukariimarishe.

“Kuna kipindi tunahitaji viongozi wa dini, wataalamu wa afya, wanasihi mbalimbali pamoja na watu wenye busara na hekima ili kumtengeneza mwanandoa ili safari yake ya ndoa iende sambamba na malengo yake,” anasema waziri huyo.


Tangazo:


Naye Waziri wa Afya Ummy Mwalimu anasema kuna mpango wa Serikali kufanya kongamano la kitaifa kuhusu matatizo ya afya ya akili athari zake kuzidi kuongezeka.

“Hali inazidi kuwa mbaya, nataka kuwe na kongamano la kwanza la kitaifa la afya ya akili tuangalie ukubwa wake na tunakwenda mbele kwa namna gani,” alisema Waziri Ummy Juni 5, 2022 wakati akizindua Baraza la Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).   

Pia kuna haja ya Serikali na sekta binafsi kuongeza wataalamu wa saikolojia ili kutoa ushauri na elimu kwa watu kuhusu masuala ya mahusiano.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW