Teknolojia ya ufuatiliaji hali za wagonjwa inatakayoleta mapinduzi sekta ya afya
- Ni mfumo unaowekwa chini ya godoro kufuatilia viashiria muhimu vya mgonjwa kwa saa 24.
- Unakusanya na kuchambua taarifa za afya bila kumgusa mgonjwa.
- Imeanza kutumika Tanzania na itaokoa maisha ya wagonjwa wengi kila mwaka.
Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza kutumia teknolojia ya Dozee kufuatilia hali za wagonjwa kwa saa 24 bila kuwaunganisha na vifaa vingi mwilini, hatua inayotarajiwa kuboresha utoaji wa huduma za afya na kuokoa maisha ya wagonjwa maisha ya Watanzania.
Mkugugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge alieyekuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa teknolojia inayotumia akili unde (AI) Julai 15, 2026 jijini Arusha alisema Dozee ni shuka maalum ambalo humuwezesha daktari kutambua hali ya mgonjwa hata akiwa nyumbani.
“Mkoa wa Arusha tunaenda kuweka kitu ambacho hakijawahi kutokea, kutakuwa na shuka maalumu, mtu ukigundulika una tatizo ukienda kule nyumbani tunaenda kukuwekea lile shuka linaitwa Dozee. Hospitali tutakua tunakuona mapigo yako ya moyo, oksijeni yako, jinsi unavyopumua, presha yako kwa kutumia hilo hilo shuka,” alisema Dk Kisenge.
Ujio wa teknolojia hiyo ni hatua muhimu katika uboreshaji wa huduma za afya hasa matumizi ya AI ili kuokoa maisha ya wagonjwa ambao hufariki kwa kukosa uangalizi wa karibu wa wahudumu wa afya.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda akizungumza katika uzinduzi huo alisema matumizi ya Dozee yanatarajiwa kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa, hususan wenye magonjwa ya moyo, kwa kuwezesha wahudumu wa afya kufuatilia viashiria muhimu vya afya kwa wakati halisi bila kuwaunganisha wagonjwa na vifaa vingi.
“Shuka hili ni mkombozi… na linaokoa vifo vya ghafla,” alibainisha Makonda ambaye ni Mbunge wa Arusha Mjini.
Dozee inafanyaje kazi?
Kwa mujibu wa tovuti ya dozee health ai, Dozee ni mfumo wa ufuatiliaji wa wagonjwa kwa mbali (Remote Patient Monitoring–RPM) unaotumia akili unde na kufanya kazi bila kumgusa mgonjwa.
Tofauti na mifumo mingine inayohitaji nyaya au sensa zinazounganishwa mwilini, Dozee hutumia sensa inayowekwa chini ya godoro. Sensa hiyo hutumia teknolojia ya mtetemo kutambua mitikisiko midogo inayosababishwa na mapigo ya moyo, kupumua na harakati za mwili.
Taarifa hizo huchambuliwa na mfumo ya Ai na kutafsiriwa kuwa viashiria vya kitabibu vinavyoweza kutumiwa na madaktari na wauguzi kufanya maamuzi ya matibabu.
Mfumo huo hufuatilia mapigo ya moyo, kiwango cha upumuaji, shinikizo la damu, kiwango cha oksijeni mwilini na joto la ngozi. Pia inaweza kubaini viashiria vya awali vya matatizo ya kupumua wakati wa usingizi.
Taarifa zote hutumwa moja kwa moja kwenye kituo cha uangalizi, kompyuta au simu za wahudumu wa afya bila kuhitaji vipimo vya mara kwa mara kwa mikono.
Moja ya sifa zake kuu ni mfumo wa tahadhari za mapema unaochambua mwenendo wa viashiria vya afya na kutoa tahadhari za mapema kuhusu kuzorota kwa hali ya mgonjwa.
Kwa mujibu wa tovuti ya Cancer National Grid ya India, mfumo huo unaweza kutoa tahadhari kati ya saa nane hadi 16 kabla mgonjwa hajafikia hatua ya dharura, hivyo kuwapa wahudumu wa afya muda wa kuingilia kati mapema.
Pia hurahisisha kazi ya wauguzi kwa kurekodi taarifa moja kwa moja, huongeza usalama wa wagonjwa na kuboresha maamuzi ya kitabibu kupitia taarifa za wakati halisi.
Dozee inaweza kuunganishwa na mifumo ya kidijitali ya kuhifadhi rekodi za wagonjwa inayotumiwa hospitalini. Mfumo huo huwezesha madaktari na wauguzi kufuatilia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja, kupokea tahadhari na kuchambua mwenendo wa afya wa kila mgonjwa.
Kulingana na watengenezaji wake, mfumo huo unakidhi viwango vya kimataifa vya usalama wa taarifa za afya vinavyolenga kulinda taarifa binafsi za wagonjwa.
Mpaka sasa teknolojia hiyo imejishindia tuzo saba na kutambuliwa na taasisi mbalimbali, zikiwemo Birac na Assocham, zote nchini India.
Historia ya Dozee
Teknolojia hii ya Dozee, ilianzishwa mwaka 2015 nchini India na kampuni ya Sukra Infotek Solutions Private Limited, kwa lengo la kuboresha matokeo ya matibabu kwa wagonjwa na kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa mwendelezo bila kukatizwa.
Mwaka 2016, waanzilishi wa Dozee walipata kile walichokiita ‘Eureka Moment’ kupitia mbwa wao aliyefahamika kwa jina la Pi. Waligundua kuwa teknolojia hiyo ingeweza kufanya kazi bila kumgusa mgonjwa moja kwa moja.
Ugunduzi huo uliweka msingi wa matumizi ya teknolojia ya kufuatilia mapigo ya moyo na upumuaji kupitia sensa inayowekwa chini ya godoro (Ballistocardiography (BCG).
Dozee ilifanyiwa majaribio ya kitabibu na kuthibitishwa kuwa na asilimia 98.4 ya usahihi ikilinganishwa na vifaa vinavyotumika katika vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU).
Wakati wa janga la Uviko-19, hitaji la kufuatilia wagonjwa bila kuwagusa liliongezeka, na Dozee ikawa mojawapo ya suluhisho lililotumiwa kupunguza mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wagonjwa na wahudumu wa afya.
Baadaye mfumo huo ulipanuliwa kutumika pia katika wodi za kawaida, hatua iliyosaidia kupunguza mzigo wa kazi kwa wauguzi kwa kurekodi na kutuma taarifa za wagonjwa moja kwa moja.
Mwaka 2022, Sukra Infotek Solutions Private Limited ilizindua kampeni ya ‘Har Bed Dozee Bed’, ikilenga kuhakikisha kila kitanda cha hospitali kinakuwa na mfumo huo wa ufuatiliaji.
Kwa sasa Dozee inatumika katika zaidi ya hospitali 280 nchini India, Marekani na baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.