Ucheleweshaji vifaatiba unavyowatesa wenye ulemavu Bahi

July 9, 2026 10:16 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Wazazi wa watoto wenye changamoto za viungo walia na gharama, ucheleweshaji wa huduma. 

Dodoma. Kwa miaka miwili mfululizo Richard Ndaga amekuwa akihudhuria hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma angalau kila mwezi kupigania afya ya mwanae. 

Ndaga ana mtoto wa kiume (2) mwenye ulemavu wa miguu na mikono ambaye anahitaji kunyooshwa viungo ili virejee katika hali ya kawaida. 

Safari ya Ndaga, baba wa watoto watano, si ya kupenda. Yeye ni miongoni mwa mamia ya wazazi, walezi na watu wenye ulemavu nchini wanaolazimika kutembea umbali mrefu kusaka kusaka huduma ya kurekebishwa viungo. 

Kitaalamu, watoto na watu wazima wenye ulemavu au matatizo ya viungo hutakiwa kupewa huduma za mazoezi tiba ili kuwasaidia kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maisha ya kila siku. 

Huduma hiyo haipatikani katika hospitali ya karibu na anakoishi Ndaga na familia yake. Zahanati na kituo cha afya vilivyopo karibu naye, havina huduma hizo. Hivyo wakazi wote wanatakiwa kwenda kupata huduma katika hospitali ya wilaya ya Bahi. 


Baadhi ya vifaa vya mazoezi tiba (Physiotherapy) pamoja na vifaa vingine vya matibabu vinavyotumika kuwahudumia wagonjwa. Picha|Canva.

Kwa maskini ni mtihani

Hata hivyo, hospitali ya wilaya ambayo ni tegemeo kwao nayo haitoi huduma stahiki za kurekebisha viungo kutokana na uhaba wa vifaa vya mazoezi tiba ama mashuhuri kwa kimombo kama physiotherapy. 

“Nilienda hospitali wakaniambia nimpeleke Dar es Salaam au Mwanza. Nauli pekee yake tu ni changamoto, huko unapoenda hujui unafikia wapi? Bado hujamuona daktari, hujanunua viatu,” anasema Cliff Fredrick mkazi wa Bahi, wilayani humo aliyempeleka mwanaye katika hospitali hiyo mwaka 2022 na kukosa huduma. 

Fredrick anasema kama vifaa hivi vingepatikana karibu na wananchi, watu wengi zaidi wangeweza kupata matibabu kwa wakati.

Hali hiyo ni kinyume na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Urekebishaji wa Tanzania (National Rehabilitation Strategic Plan 2021–2026) wa Wizara ya Afya unaotaka huduma za urekebishaji viungo zitolewe kwa ufanisi kuanzia hospitali za wilaya, rufaa, kanda, na Taifa ikiwa ni sambamba na kuwajengea uwezo watoa huduma hizo.

Ukosefu wa vifaa tiba vya mazoezi huchelewesha matibabu kwa wakati na kwa mujibu wa wataalamu wa afya hali hiyo inahatarisha maelfu ya watoto kupata ulemavu wa kudumu katika ukuaji wao.

Kwa mujibu wa takwimu za Msingi za Tanzania mwaka 2024 za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2022 Tanzania ilikuwa na watu wenye ulemavu milioni 5.34 sawa na asilimia 11.2 huku wenye ulemavu wa kutembea wakiwa 876,290.

Hii ni sawa na kusema watu 11 kwa kila watu 100 waliopo nchini wana aina fulani ya ulemavu ikiwemo wa kutembea na kushika vitu. Watu wenye ulemavu, wasipotibiwa mapewa na kupatiwa mazingira wezeshi hukosa fursa za kijamii na kiuchumi kama wanazopata wasio na ulemavu. 

Uhaba wa vifaa, maumivu kwa familia

Ally Rajabu, mlezi wa mtoto mwenye ulemavu wa miguu, mikono na mdomo wilayani Bahi, anasema kwa familia maskini ni ngumu kumudu gharama za huduma za mazoezi tiba hususan zinapohusisha kusafiri umbali mrefu. 

Licha ya gharama ya awali ya kupata viatu maalum vya matibabu kuwa ni Sh50,000 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, familia yake hulazimika kujichanga fedha za chakula na nauli kila mwezi ili kuhakikisha mtoto wao anaendelea kupata huduma zinazohitajika.

Ili kusafiri kutoka Bahi hadi Dodoma mjini, Veronica Pius anaeleza hutumia wastani wa Sh8,000 kwa nauli kila mwezi, fedha ambazo zingeelekezwa katika mahitaji mengine ya familia kama huduma hizo zingepatikana katika hospitali ya karibu. Siku anayoenda kliniki ya mazoezi, husitisha kila kitu ikiwemo shughuli za ufundi cherehani zinazomsaidia kupata kipato cha kuhudumia familia yake akiwemo mtoto mwenye ulemavu anayemlea. 

Kwa mujibu wa tovuti ya Physiopedia kutoka nchini Uingereza watu bilioni 2.4 wa rika zote duniani wanahitaji huduma za urekebishaji wa uwezo wa kufanya shughuli za kila siku (rehabilitation).

Ripoti ya CAG yafichua pengo la vifaa

Huduma hizi zinajumuisha teknolojia saidizi pamoja na afua mbalimbali kama vile mazoezi, mafunzo, elimu, msaada na ushauri nasaha, pamoja na urekebishaji wa mazingira.

Kukosekana kwa huduma stahiki za matibabu ya viungo katika Hospitali ya Wilaya ya Bahi, kwa mujibu wa uchunguzi wa Nukta Habari ni matokeo ya kutopokelewa kwa vifaa muhimu katika huduma za kurekebisha viungo. 

Awali Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023/24 ilibaini kuwa vifaa tiba vyenye thamani zaidi ya Sh65.3 milioni katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi havikupokelewa. 

Vifaa tiba ambavyo havikupokelewa, kwa mujibu wa ripoti kuu ya mwaka ya ukaguzi wa Tamisemi, Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, ni sawa na asilimia 16 au moja ya sita ya Sh400 milioni iliyokuwa imetolewa kwa Bohari ya Dawa (MSD) kupitia mfumo wa malipo ya awali (prepayment).

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dk Lilian Mpanda aliiambia Nukta Habari mkoani Dodoma kuwa baadhi ya vifaa vya mazoezi tiba vilishindikana kufikishwa kutokana na changamoto ya upatikanaji wake kwa upande wa MSD.

Baadhi ya dawa, vifaa tiba na bidhaa muhimu za afya zilizohifadhiwa katika stoo ya dawa ya Hospitali ya Halmashauri ya Bahi. Picha | Fatuma Hussein.

‘Ishu ni MSD’

Anasema hospitali imekuwa ikifuatilia mara kwa mara suala hilo kwa muda mrefu, lakini imeendelea kupata taarifa kuwa vifaa hivyo havikuwa vinapatikana kwenye bohari.

“Tuna mtaalamu wa mazoezi tiba, lakini baadhi ya wagonjwa wanahitaji vifaa maalumu ili huduma itolewe kikamilifu. Hapo ndipo changamoto kubwa ilipo,” anasema Dk Mpanda.

Wagonjwa wanaohitaji huduma hizo hususan watoto, anasema hulazimika kupelekwa katika hospitali za mkoa au Hospitali ya Taifa ya Benjamin Mkapa ili kupata huduma zinazohitajika.

Ukosefu wa vifaa hivyo, anabainisha Dk Mpanda, unaweza kusababisha kuchelewa kwa maendeleo ya watoto, maumivu ya muda mrefu kwa watu wazima na hata uwezekano wa ulemavu wa kudumu endapo matibabu hayatapatikana kwa wakati.

Hospitali hiyo ilipokea vifaa tiba vingi, Mfamasia wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi, Atusungukile Sanga anaeleza, ila sehemu kubwa ya vifaa vya mazoezi tiba bado havijapatikana.

Sanga anasema hospitali ilipokea Sh300 milioni kati ya Sh400 milioni zilizotengwa kwa ununuzi wa vifaa tiba, huku Sh100 milioni zikigawanywa kwenye vituo vingine vya afya. 

“MSD bado inadaiwa Sh34 milioni zinazohusishwa zaidi na vifaa vya mazoezi tiba ambavyo havijawasilishwa,” anaeleza. 

MSD: Hatuhusiki na ucheleweshaji

Licha ya viongozi wa hospitali ya wilaya kuwamwagia lawama MSD juu ya kucheleweshwa vifaa tiba hivyo, Mkurugenzi wa Ugavi na Uendeshaji wa MSD, Hassan Ally anasema hawana deni la vifaa vya mwaka wa fedha 2023/24 kwa halmashauri ya Bahi.

Oda za mwaka huo, anaeleza kuwa zilitekelezwa kwa wakati na changamoto ya vifaa vya mazoezi tiba ilishughulikiwa kwa kutoa taarifa rasmi ya kutokuwepo kwa bidhaa hizo (out of stock notification), hatua ambayo iliruhusu hospitali kutafuta vifaa hivyo kutoka kwa wasambazaji wengine.

“Tulitoa taarifa rasmi kuwa vifaa hivyo havikupatikana na kisheria waliruhusiwa kuvinunua kutoka chanzo kingine,” anasema Ally.

Mahitaji ya vifaa vya mazoezi tiba, kwa mujibu wa Meneja wa Kanda wa MSD Dodoma, Mwanashehe Jumaa, yalikuwa sehemu ya mpango wa mwaka 2024/25 na si katika oda iliyolipiwa mwaka 2023/24.  

Bohari ya Dawa (MSD) ni kiungo muhimu katika kuhakikisha dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinawafikia wananchi kwa wakati. Picha| Goodluck Gustaph| Nukta Africa.

Kisheria, taratibu za manunuzi ya umma kupitia MSD zinasimamiwa na misingi mbalimbali ikiwemo hati ya ukosefu wa bidhaa (out of stock notification – OS), ruhusa ya kununua nje vifaa hivyo kutoka kwa wazalishaji au wasambazaji binafsi pindi wanapopewa taarifa hiyo. 

Hapa kuna maswali muhimu ya kuelewa safari ya uwajibikaji. Kwa nini Halmashauri ya Wilaya ya Bahi haikununua vifaa hivyo kwa wakati baada ya kuambiwa havipatikani? Kama MSD wanasema hawakuwa na oda ya vifaa tiba vya mazoezi katika mwaka wa fedha 2023/24 kwa nini viongozi wa hospitali wanasisitiza vilikuwepo?

‘Juni 2026 wasipoleta tutanunua kwingine’

“MSD wametuahidi kuwasilisha vifaa hivyo kabla ya Juni. Wasipofanikiwa, watatupa ruhusa ya kuvinunua kwa wasambazaji wengine,” anasema Atusungukile Sanga Mfamasia wa hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya mwaka 2023 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2024, taasisi za umma zinalazimika kuhakikisha bidhaa na huduma zinapatikana kwa wakati, kwa kuzingatia thamani ya fedha, uwazi na ufanisi wa matumizi ya rasilimali za umma. 

Hivyo, ucheleweshaji wa upatikanaji wa vifaa muhimu vya mazoezi tiba unaweza kuathiri utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuibua maswali kuhusu ufanisi wa uratibu wa mahitaji, ugavi na ufuatiliaji wa manunuzi kati ya taasisi husika. 

Mchambuzi wa Sera na Maendeleo kutoka mtandao wa asasi ya kiraia wa Policy Forum, Samwely Mkwatwa anasema anavyoona upatikanaji wa vifaa tiba katika hospitali hiyo unatokana zaidi na udhaifu wa uratibu kati ya MSD na halmashauri kuliko uhaba wa fedha.

Anaongeza kuwa mifumo ya taasisi hizo hazisomani, jambo linalofanya maombi ya dawa na vifaa tiba kufanyika bila taarifa sahihi kuhusu bidhaa zilizopo au zisizokuwepo.

Kutokana na hali hiyo, Mkwatwa anashauri Serikali kuunganisha mifumo ya kidijitali ya MSD na halmashauri ili watumishi wa afya waweze kuona hali halisi ya bidhaa zilizopo kabla ya kuwasilisha maombi.

“Mfumo huu wa kidijitali utaondoa utegemezi wa taratibu za kuandika kwa mkono na kupunguza makosa yanayotokana na mifumo kutosomana,” anasema Mkwatwa.

Wakati familia zikiendelea kubeba gharama za matibabu na watoto wakisubiri huduma zinazoweza kubadili maisha yao, hatma ya vifaa hivyo ipo chini ya viongozi wa Halmashauri ya Bahi katika kutatua tatizo hilo ambalo limedumu kwa muda mrefu. 

Huduma zaendelea kwa kuazima vifaa

Kwa sasa pamoja na changamoto hizo za uhaba wa vifaa tiba, hospitali haijasitisha kabisa huduma za mazoezi tiba.

Dk Mpanda anaongeza kuwa, mtaalamu wa mazoezi tiba amekuwa akitafuta msaada kutoka hospitali nyingine za Serikali kwa kuazima baadhi ya vifaa vinavyohitajika na kuvirudisha baada ya matumizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
9 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
9 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Ulinzi waimarishwa Dar, maduka yachelewa kufunguliwa

Ulinzi waimarishwa Dar, maduka yachelewa kufunguliwa

Nukta TV

MFUMUKO WA BEI kuendelea kuwa mdogo licha ya gharama za mafuta

MFUMUKO WA BEI kuendelea kuwa mdogo licha ya gharama za mafuta

Nukta TV

Hali ya uchumi Tanzania: Makadirio ya ukuaji wa uchumi Bara 6%, Zanzibar 6.6%

Hali ya uchumi Tanzania: Makadirio ya ukuaji wa uchumi Bara 6%, Zanzibar 6.6%

Nukta TV