Mchengerwa aipa Wizara ya Afya mwelekeo mpya, watumishi waonywa

December 8, 2025 5:49 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Aagiza kuanza kwa mchakato wa ithibati ya kimataifa na matumizi ya teknolojia za kisasa sekta ya afya.
  • Watumishi wa afya waonywa kutokana na ucheleweshaji wa huduma kwa wagonjwa.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk Seif Shekalaghe, kuhakikisha hospitali zote za kanda zinaanza mara moja mchakato wa kupata Ithibati ya kimataifa ili kuongeza ubora na kutambulika kimataifa.

Waziri Mchengerwa aliyekuwa akizungumza leo Desemba 8, 2025 kwenye kikao kazi na watumishi wa sekta ya afya jijini Dar es Salaam kilichofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga, amesema kuwa ithibati hizo zitaziwezesha taasisi za afya nchini kuendana na viwango vya kimataifa, hatua itakayoboresha utoaji wa huduma pamoja na kuongeza pato la Taifa. 

“Ninazielekeza hospitali zote za kanda, taasisi zetu zote kuanza mchakato wa kupata ithibati za kimataifa. Tutakuwa na vigezo mahsusi ambavyo tutalazimika kuvifuata. Tutaongeza utolewaji wa huduma lakini pia kuongeza pato la Taifa kwa kupata wageni kutoka maeneo mbalimbali,” ameeleza Waziri Mchengerwa.

Pamoja na agizo hilo, Mchengerwa amemtaka Katibu Mkuu kusimamia uanzishwaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba, kuimarisha ‘medical tourism’ (Tiba utalii) kama chanzo kipya cha mapato na kuimarisha huduma za afya ya kinga.

Vile vile, kuongeza nguvu katika utafiti, ubunifu na tiba shirikishi, pamoja na kuhakikisha matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo mifumo ya afya ya kidijitali na akili unde (digital health na AI) yanaimarishwa katika mfumo wa afya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa ametoa wito kwa viongozi na watumishi wa sekta ya afya nchini kuhakikisha wagonjwa wanahudumiwa kwa wakati ili kuondoa foleni zisizo za lazima.

Aidha, amesema foleni mara nyingi si matokeo ya wingi wa wagonjwa bali ni dalili ya udhaifu wa mifumo ya utoaji huduma, akiwataka watumishi kuchukua hatua za kuboresha mifumo hiyo mara moja.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Delilah Kimambo, amesema hospitali hiyo inatekeleza majukumu yake kupitia Kurugenzi 14, Idara 54 na Vitengo 228. 

Watumishi Sekta ya afya waonywa

Waziri Mchengerwa ametoa onyo kali kwa viongozi wa taasisi na watumishi wa sekta ya afya, akiwataka kubadilika na kuwahudumia wagonjwa kwa weledi na kwa wakati.

Amesema haikubaliki wagonjwa kusubiri huduma kwa muda mrefu kwa sababu ya changamoto ambazo zinaweza kutatuliwa mara moja katika mazingira ya kawaida.

Akitolea mfano, Mchengerwa amesema Taasisi ya Saratani ya Ocean Road imepokea mashine mpya ya matibabu lakini haijaanza kutumika kwa madai ya kusubiri hafla ya ufunguzi.

Aidha, ameeleza kuwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ina mashine tatu ambazo hazifanyi kazi kwa takribani miezi miwili, bila hatua madhubuti kuchukuliwa, hali inayosababisha wagonjwa kukosa huduma muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks