Mfumo wa zungumza na Waziri wa Afya kuimarisha sekta ya afya Tanzania
- Mwananchi atatakiwa kupiga namba ya bure 119, kutuma ujumbe mfupi, mitandao ya kijamii au tovuti rasmi.
Arusha. Serikali ya Tanzania imezindua mfumo mpya wa kidigitali wa ongea na Waziri wa Afya ikilenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na utatuzi wa haraka wa changamoto za afya nchini.
Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa mfumo huo leo Januari 26, 2026 amesema kuwa mfumo huo utatatua changamoto za wananchi na kuboresha sekta ya afya.
“Tunatamani kusikia sauti ya mwananchi kwani ndiyo itakayotuwezesha kufanya mabadiliko makubwa katika sekta ya afya….
…Tunajua sekta ya afya inahudumia mamilioni ya Watanzania na tunaamini bado zipo changamoto ndogo ndogo ambazo bado hazijatatuliwa,” amesema Mchengerwa.

Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa (wa pili kulia) akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha huduma za wagonjwa wa saratani chini ya ufadhili wa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru. Picha WAF.
Mfumo huo wa kwanza katika Wizara ya Afya nchini umezinduliwa wakati ambao wizara hiyo inabiliwa na malalmiko lukuki kutoka kwa wananchi mengine yakigusia mwenendo wa wahudumu wa afya au utolewaji wa huduma.
Licha ya uwepo wa masanduku ya maoni, changamoto hizo hufanyiwa kazi kwa uchache hali inayosababisha baadhi ya wananchi kutegemea mitandao ya kijamii kuwafikia viongozi wa hospitali au wa wizara hiyo muhimu.
Kutokana na ukweli huo, Mchengerwa amesema mfumo huo utasaidia kusikiliza kero na mapendekezo kwa haraka, kuzifikisha kero hizo kwenye ngazi sahihi za maamuzi na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Ili kuwasiliana na Waziri wa Afya kwa ajili ya kuwasilisha kero hizo mwananchi atatakiwa kupiga namba ya bure 119, kutuma ujumbe mfupi, mitandao ya kijamii au tovuti rasmi www.owa.moh.go.tz
Latest