Wizara tano zilizoidhinishiwa fedha nyingi 2026/27
- Ni pamoja na Wizara ya Fedha,Ujenzi na Uchukuzi.
- Wizara hizo tano kwa pamoja zitatumia zaidi ya nusu ya bajeti yote.
Dar es Salaam. Wakati Bunge la 13 likikaribia kufunga shughuli zake, wizara 27 pamoja na Serikali Kuu zimehitimisha mchakato wa kuwasilisha na kupitisha bajeti zao, hatua inayoweka msingi wa kuanza kwa mwaka mpya wa fedha 2026/27
Wizara hizo zilianza rasmi kuwasilisha bajeti zao Aprili 1, mwaka huu na kuhitimisha Juni 2, 2026, ikifuatiwa na Bajeti Kuu ya Serikali iliyoidhinishiwa Sh62.33 trilioni Juni 11,2026 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.Â
Baada ya wiki kadhaa za majadiliano, Bunge la Tanzania liliipitisha bajeti hiyo ya Serikali kwa asilimia 97.66 hatua inayoweka msingi wa kuanza utekelezaji wa baadhi ya vipaumbele katika mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai 1, 2026.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa kati ya wizara 27, zipo zilizopata mgao mkubwa zaidi wa fedha ukilinganisha na nyingine hali inayoonyesha utofauti wa vipaumbele kulingana na mahitaji ya kisekta
5. Wizara ya Ujenzi
Wizara ya Ujenzi imeshika nafasi ya tano baada ya kuidhinishiwa bajeti ya Sh2.56 trilioni katika mwaka wa fedha 2026/27, ikiongezeka kwa asilimia 12.5 kutoka Sh2.28 trilioni iliyopitishwa mwaka 2025/26.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alisema kati ya fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya mwaka ujao, Sh97.1 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya wizara na taasisi zake, huku Sh2.46 trilioni zikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Sh92.2 bilioni ni za mishahara ya watumishi na Sh4.8 bilioni ni za matumizi mengineyo.
Kwa mujibu wa Waziri Ulega, bajeti ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inajumuisha Sh1.54 trilioni za fedha za ndani na Sh922 bilioni za fedha za nje.Â
Fedha za ndani zinajumuisha Sh1.04 trilioni kutoka mfuko wa barabara na Sh497 bilioni kutoka mfuko mkuu wa Serikali.
4.Wizara ya Uchukuzi
Wizara ya Uchukuzi nayo imebahatika kuingia katika orodha ya wizara zilizopata fedha nyingi baada ya kuidhinishiwa na Bunge Sh2.87 trilioni.
Kwa mujibu wa waziri wa wizara hiyo Prof Makame Mbalawa, Sh126 biloni zimetengwa kwa matumizi ya kawaida na Sh2.74 trilioni kwa miradi ya maendeleo.
Ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 kiasi hicho ni sawa ongezeko la Sh127.3 bilioni ikiwa ni sawa na asilimia 4.6
Hii ni sawa na kusema kuwa kwa mwaka ujao wa fedha takribani asilimia 95.61 ya bajeti hiyo itaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Kutokana na bajeti hiyo, wizara hii itasimiamia miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya bandari na huduma za usafiri majini ambayo inajumuisha Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DMGP).
Vile vile, miradi ya kuboresha usafiri wa anga na hali ya hewa nchini ,miradi ya uendelezaji wa miundombinu ya reli na miradi ya uboreshaji wa vyuo vya mafunzo ya kisekta.Â
3.Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeshika nafasi ya tatu baada ya kuidhinishiwa bajeti ya Sh4.28 trilioni katika mwaka wa fedha 2026/27.
Bajeti hiyo imeongezeka kwa kwa asilimia 17.6 kutoka Sh3.64 trilioni zilizopitishwa mwaka 2025/26.Â
Aidha, kati ya fedha hizo zilizoombwa bungeni, sehemu kubwa imeelekezwa kwenye shughuli za ulinzi wa taifa, uendeshaji wa Jeshi la Kujenga Taifa, pamoja na miradi ya maendeleo ya miundombinu ya kijeshi na kijamii kupitia mafungu yake matatu.
2. Ofisi ya Waziri Mkuu
Ofisi ya Waziri Mkuu imeshika nafasi ya pili kwa baada ya kuidhinishiwa bajeti ya jumla ya Sh12.50 trilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake pamoja na taasisi zilizo chini yake.Â
Kati ya fedha hizo, Sh8.7 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh3.7 trilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasiliosha bajeti hiyo alieleza kuwa hizo, Sh225.02 bilioni ni kwa ajili ya Mfuko wa Bunge.
Kati ya fedha hizo Sh207.9 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 17.02 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Bajeti hii ya jumla ya Sh12.50 trilioni ni sawa na takribani asilimia 20.0 ya bajeti kuu ya Serikali ya Sh62.33 trilioni, hivyo kuifanya Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa miongoni mwa taasisi zinazopokea mgao mkubwa wa rasilimali za taifa.
Bajeti hii inajumuisha taasisi zote zilizopo chini yake ikiwemo, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu (Sh183.95 bilioni) Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Sh12.26 bilioni).
Pia, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano ambapo bajeti yake ni (Sh49,93 bilioni) bila kusahau mfuko wa Bunge (Sh225.02 bilioni).
Aidha, Ofisi hii ni miongoni mwa taasisi ambazo zimeongezewa majukumu na taasisi zilizo chini yake katika mwaka huu wa fedha, hatua inayoendana na kuimarishwa kwa uratibu wa shughuli za Serikali na usimamizi wa utekelezaji wa sera na mipango ya kitaifa.
1.Wizara ya Fedha
Wizara yaFedha imeongoza kwa kuwa na bajeti kubwa zaidi miongoni mwa wizara na taasisi baada ya kuomba na kuidhinishiwa Sh21.34 trilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27.Â
Bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 5.75 kutoka Sh20.18 trilioni zilizopitishwa mwaka 2025/26.
Hadi mwisho wa Aprili 2026, mafungu manane yalikuwa yamepokea Sh14.08 trilioni, sawa na asilimia 70.63 ya bajeti iliyohuishwa kwa mwaka 2025/26.
Waziri wa wizara hiyo, Balozi Khamis Omar alisema kati ya bajeti ya mwaka 2026/27, Sh19.45 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh1.89 trilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Aidha, Fungu 045, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi linaomba kuidhinishiwa Sh132.22 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo katika mwaka 2026/27.
Kati ya fedha hizo, Sh120.39 bilioni ni kwa matumizi ya kawaida na Sh11.83 bilioni kwa matumizi ya maendeleo.
Wizara zenye bajeti ndogo
Wakati wizara hizo tano zikiidhinishiwa kitita kikubwa cha fedha zipo baadhi ya wizara zimeambulia kiasi kidogo cha fedha ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Sh108.02 bilioni.
Wizara nyingine ni Madini, (Sh174. 98 bilioni) Viwanda na Biashara (Sh137.8 bilioni), Nyumba Maendeleo na Makazi (Sh210.2 bilioni) pamoja na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Sh359.3 bilioni)