Wahamiaji haramu waongezeka kwa asilimia 112 ndani ya mwaka mmoja
- Idadi hiyo imeongezeka kutoka watuhumiwa 49,469 kwa mwaka 2026/27.
- Serikali yaendelea kuimarisha operesheni za misako, doria na ukaguzi katika maeneo ya mipakani.
Dar es Salaam. Idadi ya wahamiaji haramu waliokamatwa nchini imeongezeka kwa asilimia 112 ndani ya mwaka mmoja licha ya Serikali kuimarisha operesheni za misako, doria na ukaguzi katika maeneo ya mipakani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma leo Mei 25, 2026, amesema Wizara kupitia Idara ya Uhamiaji imekamata watuhumiwa 49,469 hadi kufikia Aprili 2026.
Ongezeko hilo ni zaidi ya mara mbili ya kiwango cha watuhumiwa 23,315 waliokamatwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.
“Kati ya hao wahamiaji haramu 34,099 waliokamatwa mwaka huu, waliondoshwa nchini,” ameeeleza Waziri Katambi
Uchambuzi wa Nukta Habari umebaini ongezeko la makundi ya wahamiaji hao haramu karibu kila mwaka.
Mathalani, mwaka 2025 kulikuwa na ongezeko la asilimia 31 kutoka watuhumiwa 17,791 waliokamatwa hadi Aprili 2024 ambapo kati yao 13,045 waliondoshwa nchini na kurudishwa katika nchi zao.
Licha ya ongezeko hilo, Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Pwani, SACI Dorah Luoga Februari 27 mwaka huu alisema pamoja na kuongezeka kwa wahamiaji haramu waliokamatwa, hali hiyo inaashiria kuimarika kwa udhibiti na si kuongezeka kwa tatizo.
“Mwaka 2024 tulikamata wahamiaji haramu 958, huku mwaka 2025 idadi ikifikia 1,479, ongezeko hili limetokana na kuimarishwa kwa doria, misako na ushirikiano wa wananchi, jambo linalosaidia kuwabaini wanaoingia kupitia njia zisizo rasmi mapema na kuchukuliwa hatua za kisheria,” alieleza Luoga.
Aidha, ili kukabiliana na wahamiaji haramu hususan katika mikoa ya mipakani, Wizara kupitia Idara ya Uhamiaji imeanzisha Kanda Maalum za Uhamiaji Mikoa ya Kagera na Kigoma ili kudhibiti wahamiaji haramu kwa kuongeza askari na vitendea kazi katika maeneo hayo.
Waziri amesema kupitia bajeti ya Sh2.4 trilioni ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka 2026/27, idara itaendelea na misako, doria na kuanzisha kanda mpya katika maeneo ya kimkakati kudhibiti wahamiaji haramu.
Kati ya fedha hizo Sh1.9 trilioni sawa na asilimia 80 ya bajeti yote ya Wizara ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh1.1 trilioni ni Mishahara na Sh7.6 bilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.