Usafiri, bidhaa za vyakula vyapaisha mfumuko wa bei kwa asilimia 0.8 Tanzania
- Mfumuko wa bei wafikia asilimia 4.0 kwa mwaka unaoishia Aprili, 2026.
- NBS yasema kiwango hicho ni cha wastani ikitazamia kuongezeka zaidi.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini kwa mwezi Aprili 2026 umefikia asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2026 ikichangiwa zaidi na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa usafiri na bidhaa za vyakula.
Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2026 imeongezeka kwa asilimia 0.8 ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2026.
Taarifa ya mwenendo wa mfumuko wa bei nchini iliyotolewa Mei 8, 2026 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa kiwango cha bei ya usafiri kimeongezeka kwa asilimia 5.2 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja hali iliyochangia kupaa kwa mfumuko huo.
Huenda ongezeko hili limechochewa na kupaa kwa bei ya mafuta duniani kunakotokana na vita vinavyoendelea kati ya Marekani, Israeli na Iran.
Vita hivyo vilivyoanza mwishoni mwa Februari, 2026 vimesababisha gharama ya mafuta yanayopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi Aprili kufikia Sh4,115 kwa petroli na dizeli Sh4,248 kwa lita baada ya Serikali kuweka ruzuku ya Sh259 kwa kila lita kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).
Kufuatia ongezeko hilo la mafuta lililoanza Machi, 2026 Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilitangaza bei mpya ya nauli kwa vyombo vya usafiri wa umma ikiwemo daladala iliyoanza kutumika Mei Mosi mwaka huu suala lililowaacha watumiaji wa usafiri huo katika maumivu.
Mara ya mwisho kiwango cha mfumuko wa bei kufikia asilimia 4.0 ilikuwa Mei 2023 na miezi iiyofuatia kiwango hicho kimekuwa kikipanda na kushuka kwa wastani wa kati ya asilimia 3.9 hadi 3.0.
Pamoja na kupaa huko kwa mfumuko wa bei NBS imesema ongezeko hilo bado ni la wastani ikitazamia kuongezeka zaidi.
“Kiwango cha mfumuko wa bei pia umekuwa na mwenendo imara kwa ujumla jambo linaloashiria utulivu wa bei kwa ujumla huku kukiwa na shinikizo la mfumuko wa bei linaloongezeka kwa kiwango cha wastani kuelekea mwisho wa kipindi,” imesema taarifa ya NBS.
Pamoja na usafiri, mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi umeongezeka hadi asilimia 5.7 kutoka asilimia 5.5 iliyorekodiwa kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2026.
Kwa upande mwingine, mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Aprili, 2026 umeongezeka hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 2.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2026.
Latest