Rais Samia aomboleza kifo cha Kardinali Pengo

February 20, 2026 10:07 am · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema Taifa limepoteza kiongozi mwadilifu na alitejitolea na mchango wake katika malezi ya kiroho na maadili utaendelea kukumbukwa, kuthaminiwa na kuenziwa.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa waamini wa Kanisa Katoliki na wote walioguswa na msiba kufuatia kifo cha aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na Kardinali wa Kanisa Katoliki, Polycarp Pengo.

Kupitia taarifa ya  Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyotolewa leo Februari 20, 2026 Rais Samia amesema Taifa limepoteza kiongozi mwadilifu na alitejitolea na kwamba mchango wake katika malezi ya kiroho na maadili utaendelea kukumbukwa, kuthaminiwa na kuenziwa.

“Rais Samia anamkumbuka Kardinali Pengo kama kiongozi wa kiroho na mzalendo aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani, maadili, umoja na mshikamano wa kitaifa, kupitia uongozi wake wa muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki,” imeeleza taarifa hiyo.

Kardinali Pengo amefariki usiku wa Februari 19, 2026 majira ya saa 04:00 usiku akiwa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu Mkuu wa Dar es Salaam, Thaddaeus Ruwa ‘ichi aliyetangaza taarifa za kifo hicho ratiba ya mazishi ya Kardinali Pengo itatolewa mara baada ya mipango kukamilika.

Rais Samia amesema Kardinali Pengo atakumbukwa kama kiongozi wa kiroho na mzalendo aliyetoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani, maadili, umoja na mshikamano wa kitaifa, kupitia uongozi wake wa muda mrefu ndani ya Kanisa Katoliki.

Safari ya utume ya Kardinali Pengo

Kardinali Pengo, alizaliwa Agosti 5, 1944 kata ya Mwazye, mkoani Rukwa. Alipata daraja la upadre mwaka 1971 baada ya masomo ya Falsafa na Teolojia nchini, kabla ya kujiendeleza na masomo ya juu ya Teolojia katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, Roma, ambako alipata Shahada ya Udaktari. 

Mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Nachingwea, na baadaye kushika nafasi mbalimbali za kiuaskofu ikiwemo Askofu wa Tunduru-Masasi na Askofu Msaidizi wa Dar es Salaam. 

Mwaka 1992 alikua Askofu Mkuu wa Dar es Salaam, nafasi aliyohudumu kwa zaidi ya miongo miwili hadi alipostaafu kwa mujibu wa kanuni za Kanisa Katoliki Agosti 15, 2019 chini ya Papa Francis. 

Pengo aliteuliwa na Mtakatifu Papa Yohane Paulo II kuwa Kardinali Februari 21, 1998, na kuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa Kanisa Katoliki barani Afrika nafasi aliyohudumu mpaka umauti wake.

Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umwangazie, Kardinali Pengo apumzike kwa amani, Amina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks