Necta yatangaza matokeo ya kidato cha nne 2025
- Watahiniwa 526,620 wamefaulu kwa kupata dvision I, II, III, na IV.
Arusha. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika Novemba, 2025, ambapo ufaulu umeongezeka kiduchu.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Prof Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam leo Januari 31, 2026 amesema kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.61 kulinganisha na ufaulu wa mwaka 2024.
“Takwimu zinaonesha kuwa ufaulu wa jumla umepanda kwa asilimia 2.61 na hivyo kufikia asilimia 94.98 ambapo watahiniwa 526,620 wamefaulu kwa kupata dvision I, II, III, na IV, mwaka 2024 watahiniwa waliofaulu walikuwa 477,262 sawa na asilimia 92.37 na mwaka 2023 walikuwa 471,427 sawa na asilimia 89.36 ,” amesema Prof Said.
Kwa mujibu wa Necta, jumla ya watahiniwa wa shule 595,810 walisajiliwa kufanya mtihani huo ambapo asilimia 97.49 sawa na watahiniwa 555,606 walijitokeza kufanya mitihani hiyo Novemba 10 hadi 28 mwaka 2025.
Watahiniwa 14,277 sawa na asilimia 2.51 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali licha ya kuwa walisajiliwa.
Ubora wa ufaulu waongezeka
Dk Said amewaambia wanahabari kuwa ubora wa ufaulu kwa mwaka 2025 umeongezeka kwa asilimia 3.1 kulinganisha na ule wa mwaka 2024.
Ubora wa ufaulu hupimwa kwa kuangalia idadi ya wanafunzi waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ambapo kwa mwaka 2025 watahiniwa 255,404 sawa na asilimia 46 walipata madaraja hayo.
Mwaka 2024 watahiniwa waliopata ufaulu wa Madaraja ya I III walikuwa 221,953 sawa na asilimia 42.96.
Kwa mujibu wa Necta katika kipengele cha ubora wa ufaulu wavulana wamefanya vizuri zaidi kulinganisha wasichana.
“…Wavulana ni 135,676 sawa na asilimia 52.30 ya Wavulana wote wenye matokeo na Wasichana ni 119,728 sawa na asilimia 40.58 ya Wasichana wote wenye matokeo.,”amesema Prof Said.
Latest