Necta yatangaza matokeo ya darasa la nne, kidato cha pili ufaulu waongezeka kiduchu
- Ufaulu wa darasa la nne umeongezeka kwa asilimia 2.67 na kidato cha pili umeongezeka kwa asilimia 1.52.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne na kidato cha pili huku ufaulu ukiongezeka kiduchu.
Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo Januari 10, 2026 amesema ufaulu wa darasa la nne umeongezeka kwa asilimia 2.67 na kidato cha pili umeongezeka kwa asilimia 1.52.
“Kwa upimaji wa darasa la nne, ufaulu umepanda kwa asilimia 2.67 ambapo wanafunzi 1,324, 970 sawa na asilimia 88.91 wamefaulu kwa kupata madaraja ya A,B,C na D….
….. Ufaulu wa kidato cha pili kwa mwaka 2025 umeimarika kwa ongezeko la asilimia 1.52 kutoka asilimia 85.41 na asilimia 85.31 ya mwaka 223,” amefafanua Dk Mohamed.
Kwa mujibu wa Necta jumla ya wanafunzi 898,718 walisajiliwa kufanya upimaji wa kidato cha pili wakiwemo wasichana 497,891 na wavulana 400,827.
Kati ya hao, waliofanya mtihani huo uliofanyika Novemba, 2025 ni wanafunzi 811,575 sawa na asilimia 91.3 katika shule za sekondari 6,223 huku wanafunzi 77,689 sawa na asilimia 8.7 wakiingia mitini.
Kwa upande wa mtihani wa darasa la nne, Dk Mohamed amesema waliosajiliwa walikuwa 1,583,686 na waliofanya mitihani hiyo walikuwa 1,490,377 kutoka shule za msingi 20,508.
Upimaji huo wa darasa la nne kwa mwaka 2025 ulizingatia mitaala iliyoboreshwa yaani masomo tisa kwa darasa la nne ambapo matano yalikuwa ya lugha, mawili ya sanaa, mawili ya sayansi na hisabati.
Pamoja na kuingizwa kwa masomo hayo mapya Dk Mohamed amesema ufaulu wa masomo yote ni mzuri.
“Kwa ujumla, ufaulu katika masomo yote ni mzuri ufaulu wa somo la kiswahili ni asilimia 92.1, somo la kiingereza ni asilimia 72.71, somo la kifaransa wamefaulu kwa asilimia 95.73, kiarabu asilimia 80.45, kichina kwa asilimia 93.16, sayansi 87.93 na hisabati ni asilimia 81.44,” amesema Dk Mohamed.
Kwa upande wa kidato cha pili Necta imesema ilipima wanafunzi hao kwa mitaala miwili ambayo ni mtaala wa awali na mtaala ulioboreshwa kwa wanafunzi wa mkondo wa amali ambao umepimwa kwa mara ya kwanza.
Licha ya ingizo hilo jipya la mkondo wa upimaji Necta umesema ufaulu ni mzuri.
“Kwa kuzingatia ufaulu watahiniwa 240,469 wa kidato cha pili wamepata madaraja la kwanza mpaka la tatu, mwaka 2024 waliopata madaraja hayo walikuwa 239,707 sawa na asilimia 30.08,” amesema Dk Mohamed.
Latest