TMA yatoa tahadhari mvua kubwa mikoa 19 kesho
- Mvua hizo zinatarajiwa kunyesha kesho Jumapili, Desemba 28, 2025.
- Zinaweza kusababisha mafuriko, maporomoko ya udongo na usumbufu wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na madhara ya mvua kubwa inayotarajia kunyesha katika mikoa 19 nchini ikiwemo Dar es Salaam.
TMA imesema mvua hizo zinatarajiwa kunyesha kesho Jumapili, Desemba 28, 2025, na huenda zikasababisha madhara mbalimbali ikiwamo mafuriko, maporomoko ya udongo na usumbufu wa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Taarifa ya TMA iliyotolewa leo Desemba 27, 2025 imeeleza kuwa mvua hiyo itanyesha katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Kigoma, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa.
Mikoa mingine ni Njombe, Morogoro, Ruvuma, Tanga, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia.
Wananchi wanaoishi katika maeneo tajwa, hususan walioko mabondeni na maeneo hatarishi, kuchukua tahadhari za mapema ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.
TMA imewasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na utabiri wa hali ya hewa unaotolewa mara kwa mara ili kupata taarifa sahihi na za wakati.
Latest