Makundi haya hatarini zaidi kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi
- Unyanyapaa na ubaguzi watajwa kuzidisha hatari kwa makundi muhimu.
- WHO yaonya kusimama kwa kasi ya kuzuia Ukimwi kunavyorudisha nyuma mafanikio ya miongo kadhaa.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani watalaam wa afya wasema watu wanaojidunga dawa za kulevya wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Kwa mujibu Shirika la Afya Duniani (WHO) kundi hilo la watu liko kwenye hatari mara 34 zaidi ya watu wengine wasiotumia madawa hayo.
Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS) iliyotolewa leo Desemba 1,2025 iinaonyesha kuwa mwaka 2024 pekee, karibu nusu ya maambukizi mapya ya VVU (asilimia 49) yalitokea katika makundi muhimu.
“Jitihada za kuzuia maambukizi ya VVU zilikwama na watu milioni 1.3 walipata maambukizi mapya, mengi yakiathiri makundi muhimu na yenye mazingira hatarishi,” inaeleza sehemu ya taarifa ya UNAIDS iliyotolewa na WHO.
Kulingana na takwimu hizo makundi mengine yenye mazingira hatarishi ni wafanyakazi wa ngono na wanawake waliobadili jinsia wako katika hatari mara 17 zaidi ya kupata VVU.
Aidha, wanaume wanaofanya ngono na jinsia yao wakikabiliwa na hatari mara 18 zaidi hali ambayo wataalamu wanaielezea kama hofu inayoendelea kimataifa.
Kulingana na Umoja wa Utetezi wa Chanjo ya Ukimwi, kufikia Oktoba 2025 takribani watu milioni 2.5 waliokuwa wakitumia dawa za kinga (PrEP) mwaka 2024 walipoteza upatikanaji wa dawa hizo kutokana na kupunguzwa kwa ufadhili.
Wataalamu wanaonya kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha malengo ya kimataifa ya kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Takribani watu milioni 2.5 waliokuwa wakitumia dawa za kinga (PrEP) mwaka 2024 walipoteza upatikanaji wa dawa hizo kutokana na kupunguzwa kwa ufadhili. Picha/All Africa.
Sababu zinazoongeza hatari kwa makundi haya
Wataalamu wanasema sababu zinazoongeza hatari kwa makundi haya ni pamoja na unyanyapaa na ubaguzi unaowafanya washindwe kufikia huduma za afya na vikwazo vya kisheria vinavyowazuia kutafuta huduma bila hofu.
Licha ya vikwazo hivyo pia changamoto za kijamii na kimfumo zinazozuia upatikanaji wa kinga, matibabu na elimu sahihi ya afya ya VVU ni mambo yanayopfanya kasi ya maambukizi miongoni mwa makundi hayo kuendelea kuwa makubwa.
Hata hivyo, inakadiriwa kuwa watu milioni 40.8 walikuwa wanaishi na VVU mwaka 2024 ambapo ni ongezeko la asilimia 0.9 ya watu waliokuwa wakiishi na maambukizi hayo kwa mwaka 2023.
Wakati huo huo, idadi ya watu wanaoendelea kupoteza maisha kwa miaka miwili mfululizo ikiendelea kuwa takribani watu 630,000 kutokana na sababu zinazohusiana na virusi hivyo idadi inayoendelea kuonyesha umuhimu wa kuimarisha huduma.
Sanjari na hilo wadau wa afya ya jamii wanasisitiza kuwa kukomesha maambukizi mapya kunahitaji hatua madhubuti zinazowalenga moja kwa moja walio katika hatari kubwa, sambamba na uwekezaji unaoendelea katika elimu, tiba na upatikanaji wa huduma rafiki kwa makundi yote.
Latest