Rais Samia awatunuku kamisheni maafisa 296 wa JWTZ, 120 waingia mitini
- Idadi ya maafisa wanafunzi waliotunukiwa kamisheni imeongezeka kutoka 236 hadi 296, ongezeko la maafisa 60 sawa na asilimia 25.4 ikilinganishwa na wale waliohitimu mwaka 2024.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewatunuku kamisheni maafisa wanafunzi 296 waliohitimu mafunzo ya kijeshi huku wengine 120 wakishindwa kuhitimu kwa sababu mbalimbali ikiwemo makosa ya kinidhamu.
Wahitimu hao ni wale waliopata mafunzo katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi (TMA) Monduli, mkoani Arusha, kundi la 06/22 waliosoma shahada ya sayansi ya kijeshi kuanzia Oktoba 24, 2022 na kundi la Kundi la 72/24 – Regular lilioanza kozi hiyo 10 Desemba 2024 na kuhitimu leo.
Ikilinganishwa na mwaka jana, idadi ya maafisa wanafunzi waliotunukiwa kamisheni imeongezeka kutoka 236 hadi 296, ongezeko la maafisa 60 sawa na asilimia 25.4.
Kati ya maafisa wanafunzi 296, waliohitimu leo wanaume ni 257 na wanawake 39 ambao wanaanza rasmi siafari ya kulitumikia Taifa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mpaka pale watakapostaafu.
Meja Jenerali Jackson Mwaseba, Mkuu wa chuo hicho aliyekuwa akizungumza katika mahafali ya wahitimu hao yaliyofanyika leo Novemba 22, 2025 mkoani Arusha amesema kuwa sababu za wanafunzi hao kushindwa kuhitimu zimegawanyika katika makundi tofauti.
Kwa mujibu wa Jenerali Mwaseba, Kundi la 06/22 – Shahada ya Sayansi ya Kijeshi lililoanza mafunzo Oktoba 24, 2022 likiwa na wanafunzi 125, kati yao wanafunzi 106 pekee ndio waliotunukiwa kamisheni huku wengine 49 wakishindwa kuhitimu kutokana na sababu tofauti.
“Kwa bahati mbaya maafisa wanafunzi 49 waliachishwa mafunzo kwa sababu mbalimbali ikiwemo maombi binafsi watano, kutofikia viwango kitaaluma 31, kukosa uaminifu wanne, ugonjwa watano na utoro wanne,” amefafanua Jenerali Mwaseba.
Hata hivyo, idadi ya wanafunzi ambao hawakuhitimu pia imeongezeka kutoka 59 mwaka jana hadi 120 mwaka huu, ongezeko la wanafunzi 61 ambalo ni sawa na asilimia 103.4.

Kundi lingine ni Kundi la 72/24 – Regular, walio anza mafunzo yao Disemba 10, 2024 likiwa na wanafunzi 173, wakiwemo maafisa 23 kutoka nchi rafiki za Burundi, Comoro, Kenya, Malawi, Msumbiji, Rwanda, Uganda na Zambia.
Hata hivyo, maafisa 71 kati yao hawakuhitimu kutokana na sababu mbalimbali ambapo maafisa wanne walifariki wakati wakiwa bado wanaendelea na masomo, maafisa 12 walikimbia mafunzo na maafisa 17 walitoa maombi binafsi.
Wengine walioshindwa kuhitimu ni maafisa tisa kutokana na matatizo ya kiafya, maafisa 17 kutofikisha viwango vya kitaaluma, maafisa saba kutokana na mwenendo usioridhisha huku maafisa wanne wakiachishwa kwa kukosa ufanisi na mmoja kukosa uaminifu.
Maafisa waliopata mafunzo kutoka vyuo rafiki
Aidha pia, wapo maafisa 111 waliopata mafunzo kutoka vyuo rafiki amabo waliripoti makao makuu ya jeshi kuanzia Julai 2025 baada ya kupata mafunzo kutoka vyo mbalimbali ndani na nje ya Afrika.

Nchi hizo ni pamoja na Afrika Kusini ambapo maafisa 10 walipata mafunzo, Burundi maafisa wawili, Ethiopia maafisa wawili, India maafisa sita, Kenya maafisa wawili, Misri maafisa nane na Morocco mafisa wawili,
Mafisa 10 kutoka Chuo cha Anga cha Kijeshi, maafisa 12 kutoka nchini Uganda na wengine wakipata mafunzo kutoka nchini Urusi.
Sherehe hizo zimeendelea kuonesha dhamira ya Serikali katika kuimarisha uwezo wa kiutendaji wa majeshi ya ulinzi na kuongeza nguvu kazi yenye taaluma, nidhamu na weledi kwa maslahi ya usalama wa nchi.
Latest