Rais Samia aagiza mawaziri, Necta kutafuta suluhu ya udanganyifu wa mitihani
- Asema udanganyifu huo unaongeza wimbi la wahitimu wasio na uwezo.
- Amtaka Waziri Mkenda kuwa mkali kudhibiti wizi huo.
- Necta yaahidiwa mashine za uchapaji.
Dar es Salaam.Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kushughlikiwa kwa changamoto ya udanganyifu wa mitihani inayosababisha Tanzania kuwa na wimbi kubwa la wahitimu wasio na uwezo.
Rais Samia, aliyekuwa akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) leo Disemba 12, 2023 jijini Dar es Salaam amesema anatumaini Necta itaishughulikia changamoto hiyo mapema ili kuboresha elimu inayotolewa nchini.
“Changamoto ya wizi wa mitihani lazima itafutiwe mwarobaini katika ngazi yoyote itakayofanyika…natumaini baada ya leo wizara itakuja na mikakati mizuri ya kushugulikia suala hili na mtaendelea kuwa wakali zaidi,” amesema Rais Samia.
Soma zaidi:Serikali yaunganisha mashirika, taasisi 16 za umma, nne zafutwa
Awali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, aliwaambia wahudhuriaji kuwa wizara yake kwa kushirikiana na Necta imedhibiti tatizo hilo kwa kiasi kikubwa na jitihada zaidi zinaendelea kuhakikisha linaisha kabisa.
“Wowote watakaojaribu kuiba mtihani hasa kwa mfumo wa kitaasisi hapana shaka tutawakamata tu…tunaendelea kuwa macho kuhakikisha kwamba huko hatuwezi kufika,” amesema Prof. Mkenda.

Rais Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Afisa Mitihani kutoka Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Bi. Fatma Muhidini Mshana kuhusu utengenezaji wa vyeti pamoja na shughuli mbalimbali zinazofanywa na Baraza hilo.PichalIkulu
Kwa mujibu wa Necta Mwaka 2023 idadi ya wanafunzi wa darasa la saba waliofanya udanganyifu katika mitihani ya kuhitimu elimu ya shule ya msingi imepungua hadi kufikia 31 kutoka wanafunzi zaidi ya 200 waliofanya udanganyifu katika mitihani hiyo ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2022.
Idadi hiyo ni sawa na badiliko la asilimia 84.5 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Serikali yaahidi kuongeza mitambo ya uchapaji Necta
Aidha, Rais Samia akiwa katika maadhimisho hayo, ameiahidi Necta mashine tatu za uchapaji zitakazorahisisha shughuli mbalimbali zinazofanyika na baraza hilo ikiwemo uchapaji wa mitihani na vyeti.
Rais Samia ameeleza kuwa anatumaini baraza hilo likiongezewa mitambo hilo litaweza kujiingizia faida zitakazoliwezesha kupunguza utegemezi kwa Serikali.
Itakumbukwa kuwa Agosti 19, 2023 Rais Samia alieleza dhamira yake ya kuyawezesha mashirika ya umma ili yajitegemee na kupunguza mzigo kwa Serikali.
Latest