Mikoa mitano inayoongoza kwa ukatili wa kijinsia dhidi ya wanaume Tanzania
- Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Arusha, Kagera, Morogoro na Tanga.
- Mmonyoko wa maadili, utandawazi wachangia ukatili kwa wanaume.
- Wadau, Serikali waingilia kati kutafuta suluhu ya kudumu.
Dar es Salaam. Alipofunga ndoa yake ya pili, Abdallah Omary (38) alijawa na matarajio makubwa ya kupata furaha na vicheko maishani mwake.
Badala ya faraja na upendo, Omary anasema amejikuta akikumbwa na maumivu ya kihisia kutoka kwa mke wake.
Mkazi huyu wa jiji la Tanga anadai mkewe amekuwa akimlazimisha waishi kwenye nyumba ya mtalaka wake, jambo ambalo anahisi linamnyima amani na linamvunjia heshima mbele ya wanaume wenzake.
“Wakati mwingine ananiambia niende kulala kwa mume wake wa kwanza. Nalala nikiwa na hofu kubwa, nikijiuliza kama anaweza kujitokeza ghafla. Hali ile si ya kawaida, nimemwambia tuishi kwenye nyumba yetu tuliyopanga, lakini yeye anasisitiza kubaki pale kwa sababu ya mtoto wake mdogo,” anaeleza Omary.
Omary ni miongoni mwa wanaume wengi Tanzania wanaokumbwa na matukio ya ukatili wa kijinsia unaochangia kurudisha nyuma maendeleo ya kundi hilo ambalo ni nguzo muhimu ya familia na Taifa.
Takwimu za bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum ya mwaka 2025/26 zinaonesha kuwa katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025 jumla ya manusura wa ukatili 19,717 waliripotiwa nchini Tanzania.
Kati ya manusura hao, wanaume ni 4,472 sawa na asilimia 22.6 au karibu robo ya manusura wote walioripotiwa katika kipindi hicho cha miezi 10.
Licha ya kuwa ukatili wa kijinsia huwakumba zaidi wanawake, idadi ya wanaume wanaofanyiwa vitendo hivyo imekuwa ikiongezeka katika miaka ya hivi karibuni, jambo linaloibua maswali mengi kuhusu hatma yao.
Ripoti ya Takwimu za Unyanyasaji na Ukatili wa Kijinsia ya 2024 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inaonesha kuwa mwaka 2023 wanaume 12,028 waliripotiwa kufanyiwa ukatili wa kijinsia.
Idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 32.2 kutoka 9,100 ya mwaka 2022.
Ukatili wa kijinsia ni kitendo chochote cha unyanyasaji ambacho husababisha, au kinaweza kusababisha madhara ya kimwili, kihisia, kiakili au mateso kwa mhanga wa tukio la ukatili.
Ni muhimu kufahamu kuwa ukatili umegawanyika katika makundi manne makuu: ambayo ni ukatili wa kimwili, ukatili wa kingono, ukatili wa kihisia na ukatili mwingine.
Aina hizi za ukatili zinajumuisha makosa kama kubaka, kulawiti, shambulio la aibu, mauaji, mauaji ya vikongwe kwa imani za kishirikina, kujeruhi, kukeketa, shambulio, na kutupa watoto.
Nyingine ni wizi wa watoto, usafirishaji haramu wa binadamu, kutelekeza familia, kupoka, kuzorotesha masomo ya mwanafunzi na ndoa za utotoni.

Dar es Salaam kinara kwa ukatili dhidi ya wanaume
Uchambuzi wa ripoti hiyo ya Takwimu za Unyanyasaji na Ukatili wa Kijinsia uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unashika nafasi ya kwanza kati ya mikoa 31 ya Tanzania kwa ukatili wa kijinsia dhidi ya wanaume.
Ripoti hiyo ambayo inapatikana katika tovuti ya NBS inaonesha kuwa mikoa ya Dar es Salaam uliripoti wahanga wanaume 3,805 mwaka 2023, Hii ni sawa na kusema kwa kila wahanga wanaume 10 waliofanyiwa ukatili watatu walikuwa katika mkoa huo wa kibiashara.
Dar es Salaam imefuatiwa kwa karibu na Arusha iliyoripoti wahanga wanaume 2,371, Tanga (1,451). Kagera imeshika nafasi ya nne kwa wahanga 535 huku Morogoro ikifunga ya orodha hiyo kwa wahanga 392.
Wakati Dar es Salaam ikiwa kinara wa ukatili dhidi ya wanaume Tanzania, Kusini Pemba imeripotiwa kuwa na wahanga wachache wanaume ambapo mwaka 2023 walikuwa 13 tu.

Ulawiti tishio kwa wanaume
Ukatili wa wanaume kulawitiwa umeonekana kuwa na ongezeka katika mikoa yote katika kipindi cha mwaka 2022 na 2023 huku ripoti hiyo ikieleza kuwa wanaume wengi wenye miaka 18 na zaidi wameongoza kwa kulawitiwa kuliko wanawake.
Mwaka 2023, Dar es Salaam iliongoza kwa kuwa na wanaume waliolawitiwa 412 ukifuatiwa na Arusha (237) na Mjini Magharibi 215.
Ukatili mwingine ambao umekuwa ukiwatesa zaidi wanaume ni kujeruhi au shambulio la kudhuru mwili ambapo Dar es Salaam bado ni kinara. Mwaka 2023, mkoa huo uliripoti wahanga 1,706.
Kwa ukatili wa kujeruhi, mkoa huo wa mashariki mwa Tanzania unafuatiwa na Arusha kwa wahanga 873 huku Tanga ikishika nafasi ya tatu kwa wahanga 502.

Sababu na athari za ukatili kwa wanaume
Mtaalamu wa Masuala ya Saikolojia na Mkufunzi Chuo cha Maendeleo ya Jamii Korogwe, Tatu Mbuguni anasema ukatili wa kijinsia kwa wanaume unaambatana na athari mbalimbali ikiwemo msongo wa mawazo, kudharaulika na kupoteza heshima kwenye jamii na mwelekeo wa maisha.
Mbuguni anasema ongezeko la ukatili dhidi ya wanaume linachangiwa na wivu wa mapenzi, kukosekan kwa usawa wa kiuchumi, elimu, mmomonyoko wa maadili kwenye jamii na utandawazi.

“Nimepokea kesi nyingi sana za wanaume wanaolalamika kuonewa au kudharauliwa. Chanzo mara nyingi unakuta ni tofauti za kielimu, kiuchumi pamoja na wivu,” anasema Tatu. “Mwenye nguvu za kiuchumi ndiye anayejiona mtoa maamuzi, mwanaume anakosa sauti, hata pale anapohitaji tendo la ndoa, anaamuliwa nikupe au nisikupe.”
Hatua zinazochukuliwa kukomesha ukatili kwa wanaume
Mwenyekiti wa Shirika la Wanaume Wanaopitia Changamoto kwenye Ndoa (SIWACHANDO) Ernest Komba anasema wanatoa elimu kwa jamii kuhusu athari za ukatili dhidi ya wanaume ili kujenga jamii yenye usawa.
Komba ambaye pia ni Rais wa wanaume wanaopigwa na wake zao majumbani anasema wanahamasisha wanaume kuripoti matukio ya ukatili badala ya kuchukua sheria mkononi au hata kujiua.
“Baadhi ya wanaume wanafikiria kuzungumza kwamba nimefanyiwa ukatili ni kama kujidhalilisha. Kwa sisi kama taasisi kazi yetu ni kutoa elimu kwa wanaume kwamba wanapaswa kuripoti matukio ya ukatili wa kufanyiwa majumbani kwa sababu msiporipoti madhara tunayaona tunakimbia watoto,” anasema Komba.

Mbali na elimu, shirika hilo pia hutoa ushauri, msaada wa kisheria na kusuluhisha migogoro ya kifamilia kwa lengo la kuunganisha ndoa na kuhakikisha ukatili wa kijinsia unapungua.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk Dorothy Gwajima katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2025/26 alisema wizara kwa kushirikiana na wizara za kisekta pamoja na wadau, itaendelea kuratibu utoaji wa elimu na huduma kwa manusura wa vitendo vya ukatili wa kijinsia kupitia madawati ya jinsia.
Jinsi ya kumsaidia mwanaume aliyefanyiwa ukatili
Mtaalam wa Saikolojia na Mahusiano, Tatu Mbuguni anaeleza kuwa hatua ya kwanza ya kumsaidia mtu aliyepitia ukatili ni kufahamu chanzo cha tatizo kilichosababisha mwanaume kufanyiwa ukatili wa kijinsia.
“Sababu tunaposema ukatili wa kijinsia sio lazima ufanyiwe na jinsia tofauti unaweza kufanyiwa ukatili wa kijinsia na jinsia moja.
Haijalishi nani walihusika kwenye kutengeneza tukio inawezekana ni taasisi za dini inawezekana familia, inawezekana ni jamaa wa karibu au wakawa ni mtu wa mbali,” anaeleza Tatu.
Tatu anasema mhanga wa ukatili asitengwe wala kulaumiwa bali asaidiwe kwa kukaa naye pamoja na kumuwekea utaratibu wa kwenda maeneo yatakayomfurahisha ili kumpunguzia msogo wa mawazo.
Pia anatakiwa akutanishwe na watu sahihi ikiwemo kupata tiba ya saikolojia kutoka kwa wataalam ili kumrejesha katika hali ya kawaida itakayomfanya aendelee kutimiza malengo yake.
Hatua hizi zitamjengea hali ya kujiamini, kujithamini, kujitegemea na kuheshimiwa na watu wanaomzunguka.
Latest



