Wadau waangilia kati Polepole kudaiwa kutekwa

October 7, 2025 5:08 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • LHRC yasisitiza kuwa iwapo anashikiliwa kwa tuhuma zozote, afikishwe mahakamani mara moja ili haki itendeke kwa mujibu wa sheria.

Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa haki za binadamu na vyombo vya habari wameingilia kati sakata la kudaiwa kutekwa kwa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole. 

Taarifa za kutekwa kwa balozi huyo mstaafu zilianza kusambaa mitandaoni kuanzia asubuhi ya Oktoba 6 mwaka huu baada ya kuthibitishwa na ndugu wa karibu wa Polepole.

Baada ya kutokea kwa tukio hilo wadau mbalimbali ikiwemo Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Shirika la Haki za Binadamu nchini (LHRC) wamejitokeza wakitaka tukio hilo lichunguzwe kwa haraka ili kubaini ukweli na kuhakikisha haki inatendeka.

“Tunalisihi Jeshi la Polisi kuchunguza kwa haraka na kwa umakini taarifa hizi, kisha Taifa letu litangaziwe kwa uwazi nini kimetokea…

…Nani mhusika na afikishwe mbele ya vyombo vya sheria haraka,” imeeleza taarifa ya Deodatus Balile, Mwenyekiti wa TEF iliyotolewa leo Oktoba 7, 2025

TEF imekumbushia matukio mengine ya utekaji yaliyowahi kufanyika nchini ikisisitiza kuwa vitendo hivyo vina hatari kubwa kwa usalama wa Taifa na vinaweza kudhoofisha amani na umoja wa Watanzania. 

““Tunasema kwa kauli moja: utekaji haukubaliki Tanzania. Amani ya nchi yetu ni urithi wa thamani unaopaswa kulindwa na kila Mtanzania,” imebainisha taarifa ya Balile.

Katika hatua nyingine LHRC imelaani vikali tukio hilo na kuwataka mamlaka husika, hususan Jeshi la Polisi, kuchukua hatua za haraka

“ Tunazitaka mamlaka husika, hususan Jeshi la Polisi zichukue hatua za haraka kuchunguza tukio hili. Iwapo anashikiliwa kwa tuhuma zozote, afikishwe mahakamani mara moja ili haki itendeke kwa mujibu wa sheria. Tunaendelea kufuatilia kwa karibu,” imeeleza taarifa ya LHRC.

Wakati wadau hao wakipaza sauti, Jeshi la Polisi limesema limeanza uchunguzi wa kina kuhusu taarifa hizo baada ya kupokea maelezo kutoka kwa Augustino Polepole anayedaiwa kuwa kaka wa Polepole. 

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime, amesema jeshi hilo lilifungua jalada la uchunguzi tangu Oktoba 6, 2025, na limeanza kukusanya taarifa na ushahidi kutoka vyanzo mbalimbali.

“Kwa sasa tunaendelea kumtafuta Augustino Polepole ili apate kutoa ushirikiano na maelezo ya kina yatakayosaidia kufafanua madai yake, ikiwemo tuhuma kwamba ofisa wa polisi alihusika katika tukio hilo,” amesema Misime.

Aidha, Misime aliongeza kwamba uchunguzi unalenga kubaini kama Polepole alikuwa akiishi katika nyumba inayodaiwa kuwa eneo la tukio au kama alikuwa mpangaji. 

Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa matokeo ya awali ya uchunguzi yatatangazwa mara tu hatua muhimu zitakapokamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks