INEC yasisitiza Mpina, Ferej si wagombea Urais Tanzania
- ACT Wazalendo yaaswa kuzingatia sheria za uchaguzi.
Arusha. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesisitiza uamuzi wake kuwa Luhaga Mpina na Fatma Ferej hawajapitishwa na tume hiyo kugombea nafasi ya Urais nchini Tanzania.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi Ramadhani Kailima, iliyotolewa leo Septemba 22, 2025 imesema kuwa imebaini Chama cha ACT Wazalendo kinaendelea kuwatambua wagombea hao katika matukio ya chama hicho kama wagombea Urais taarifa ambayo si sahihi.
“Tunasisitiza kwamba, chama cha ACT Wazalendo hakina wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025..
…Kwa kuzingatia uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wa tarehe 15 Septemba, 2025 uliotengua uteuzi wa Ndugu Luhaga Joelson Mpina aliyependekezwa na chama hicho kugombea Kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia pingamizi lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,’ imesema taarifa ya Kailima.
Msisitizo huo wa INEC unakuja ikiwa zimesalia siku 37 kufikia Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani huku ACT Wazalendo ikiendelea kuweka mapingamizi mahakamani juu ya uamuzi wa kufutwa kwa mgombea Urais kupitia chama hicho.
Kwa mujibu wa taarifa ya ACT Wazalendo iliyotolewa jana Septemba 21, 2025 pingamizi hilo la INEC la khA kumuondoa Mpina katika orodha ya wagombea uchaguzi litasikilizwa leo katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma mbele ya Majaji watatu ambao ni Jaji Sylvester Kainda, Jaji Fredrick Manyanda, na Jaji Abdallah Gonzi.

ACT Wazalendo bado inaendelea kumtambua Luaga Mpina (pichani) kama mgombea Urais kupitia chama hicho.Picha/ACT Wazalendo/Instagram.
Aidha, INEC imeitaka ACT Wazalendo kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ikiwemo kuheshimu ratiba ya uzinduzi wa kampeni za ubunge katika maeneo husika
“Tunashauri na kusisitiza kuwa, Chama cha ACT Wazalendo kizingatie masharti ya Kanuni ya 35 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za Mwaka 2025 inayohusu utaratibu na ratiba za kampeni za ubunge,” imesema taarifa ya Kailima.