Si kweli Nida yatoa mkataba kwa kampuni ya Babuleo kusambaza vitambulisho
- Nida imewataka Wananchi kuwasiliana nao simu 0232210500 au kutembelea ofisi zao zilizopo nchi nzima kwa ajili ya msaada zaidi.
Arusha. Mamlaka ya Vitambulisho Tanzania (Nida) imetahadharisha umma juu ya taarifa potofu inayosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kutoa kibali kwa kampuni ya Babuleo kutoa vitambulisho.
Chapisho hilo la uzushi linalosambaa kwenye mitandao ya kijamii katika mfumo wa barua inayodaiwa kutoka Nida linasema mamlaka hiyo imetoa idhini kwa kampuni ya Babuleo kutoa vitambulisho kwa wananchi wenye namba za utambulisho wa Taifa (NIN) kuanzia mwaka 2020 hadi 2025.
Taarifa iliyotolewa na Nida leo Septemba 19, 2025 inabainisha kuwa mamlaka hiyo haina mkataba wowote na kampuni ya Babuleo hivyo wananchi wanatakiwa kupuuzia chapisho hilo.
“NIDA haina mkataba na Shirika la BABULEO LTD Wala Wakala wa aina yoyote katika utoaji huduma zake. Malipo halali ya huduma za NIDA pale inapobidi, zinalipwa kupitia Namba ya Malipo yaani Control Number,”imesema taarifa ya Nida.
Kwa mujibu wa Nida hii si mara ya kwanza kwa shirika linalojitambulisha kwa jina la BABULEO LTD kupotosha umma kuhusu ushirikiano wake na mamlaka hiyo katika kutoa huduma mbalimbali ikiwemo vitambulisho vya Taifa namba za utambulisho wa Taifa.
Taarifa hizo potofu zinaweza kupoteza uaminifu wa shirika hilo husuani katika utoaji wa huduma muhimu kama vitambulisho na namba za Taifa ambazo ni muhimu sana katika shughuli mbalimbali ikiwemo uombaji wa kazi na usajili wa laini za simu na huduma nyingine/
Aidha, Nida imewataka Wananchi kuwasiliana nao kwa namba 0232210500 au kutembelea ofisi zao kwa msaada zaidi.
Latest
