Wasiofuata vitambulisho vya Nida kikaangoni
- Nida yasema itawasitishia matumizi ya namba ya utambulisho wa Taifa.
Arusha. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) imetangaza kusitisha matumizi ya namba ya utambulisho wa Taifa (NIN) kwa Watanzania watakaoshindwa kuchukua vitambulisho vyao kwa wakati.
Taarifa ya James Kadi, Mkurugenzi Mkuu wa Nida iliyotolewa leo Januari 17, 2025 inabainisha kuwa watakaofungiwa matumizi ya namba hizo ni wale ambao watashindwa kuvifuata vitambulisho vyao mwezi mmoja baada ya kutumiwa ujumbe mfupi (sms) na mamlaka hiyo.
“Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa inawatangazia wale wote ambao hawajajitokeza kuchukua vitambulisho vyao na watakaopokea ujumbe mfupi wa maandishi katika simu zao (sms), kufika katika ofisi za NIDA za wilaya walikojisajili kuchukua vitambulisho vyao kama itakavyoelezwa katika ujumbe huo…
… Atakayeshindwa kufanya hivyo matumizi ya Namba ya Utambulisho wake wa Taifa (NIN) yatasitishwa baada ya mwezi mmoja tangu kupokea ujumbe huo,” imesema taarifa ya Kadi.
Taarifa ya Nida inakuja ikiwa umesalia mwezi mmoja kutekeleza agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani Innocent Bashungwa aliyeitaka mamlaka hiyo kugawa vitambulisho milioni 1.2 ndani ya miezi miwili.
Waziri Bashungwa alitoa agizo hilo Disemba 17, 2024 katika ziara ya kikazi katika mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo pia aliwataka kupunguza urasimu unaokwamisha ufanikiwaji wa zoezi hilo nchini.
Nida imetoa taarifa hiyo baada ya jitihada za kuwafikia wananchi wenye vitambulisho vilivyokamilika kupitia ofisi za watendaji wa Kata, Vijiji, Mitaa Vitongoji na Shehia kugonga mwamba.
Zoezi hilo lililofanyika Oktoba 12, 2023 hadi Machi 2024 lillilenga kuongeza upatikanaji wa vitambulisho hivyo kwa Wananchi baada ya umuhimu wake kuongezeka katika shughuli mbalimbali ikiwemo za kijamii.
Ikiwa matumizi hayo ya namba yatasitishwa kuna baadhi ya Wananchi watakosa huduma muhimu ikiwemo kusajili laini za simu, kujiunga na huduma za kibenki, kuomba kazi katika mifumo rasmi ya serikali, kupokea vipeto na vifurushi pamoja na huduma nyingine nyingi.