Bado sana: Vitambulisho vya Taifa vyazidi kuitesa NIDA
Rais mstaafu Jakaya Kikwete akionyesha mfano wa kitambulisho cha Taifa kwa baadhi ya viongozi wa wakati wa utawalawa wake ulioasisi zoezi la utoaji vitambulisho hivyo. Picha|IPP.
- Hadi Machi mwaka huu, NIDA imezalisha na kusambaza vitambulisho va Taifa milioni 7.1.
- Ni asilimia 38 ya wananchi wenye namba za utambulisho ndiyo waliopata vitambulisho vya Taifa.
- Zaidi ya wananchi milioni 18 wapata namba za utambulisho.
Dar es Salaam. Serikali imesema hadi kufikia Machi mwaka huu imefanikiwa kuzalisha na kusambaza vitambulisho vya Taifa milioni 7.1, licha ya kugawa namba za utambulisho (NIN) milioni 18.7 kwa wananchi, jambo linalowaacha mamilioni ya Watanzania bila vitambulisho.
Hiyo ina maana kuwa ni takriban asilimia 38 au sawa takriban Watanzania wanne kati ya 10 wenye NIN ndiyo waliopata vitambulisho vya Taifa.
Vitambulisho vya Taifa ni moja ya nyaraka muhimu kwa sasa nchini Tanzania inayohitajika katika shughuli mbalimbali ikiwemo kwenye shughuli za kielimu na biashara.
Utoaji wa NIN miaka ya hivi karibuni umesaidia Watanzania kuepuka usumbufu licha ya wengine kukwama kupata huduma kutokana na kutokuwa na vitambulisho.
“NIDA imezalisha na kusambaza vitambulisho 925,342 na hivyo kufanya idadi ya vitambulisho vilivyozalishwa na kusambazwa hadi Machi, 2021 kufikia milioni 7.1,” amesema Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/22 bungeni leo Mei 3, 2021.
Simbachawene amesema kazi ya uzalishaji vitambulisho vilivyobaki inaendelea na inatarajiwa hadi kufikia mwezi Julai, 2021 watu wote wenye namba za utambulisho (NIN) watapata vitambulisho vyao.
Ili ahadi hiyo ya Simbachawene itimie ya kusambaza vitambulisho milioni 11.6, itahitaji Nida kuzalisha na kusambaza wastani wa vitambulisho milioni 3.1 kwa mwezi kwa kipindi cha miezi minne iliyosalia ya Aprili hadi Julai mwaka hii.
Kiwango hicho kwa mwezi ni zaidi ya mara tatu ya vitambulisho vyote vilivyozalishwa na kusambazwa kuanzia Julai 2020 hadi Machi mwaka huu.
Soma zaidi:
Licha ya changamoto hizo, Simbachawene amesema usajili wa wananchi kwa ajili ya kupata vitambulisho umeongezeka na kufikia watu milioni 22.4 ikilinganishwa na lengo la kusajili watu milioni 25.3.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha utendaji wa NIDA ikiwemo kukamilisha upembuzi yakinifu ili kupata njia mbadala ya kuunganisha ofisi za wilaya 14 ambazo hazijafikiwa na mkongo wa mawasiliano wa Taifa ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kasi ya NIDA kutengeneza na kusambaza vitambulisho imekuwa ndogo, licha ya kufanikiwa kutoa NIN kwa wananchi wengi wenye sifa ya kupata vitambulisho hivyo huku kukiwa na ripoti za kutotumia vema rasilimali zilizopo katika uandaaji wa vitambulisho hivyo.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2019/20 imeibaini uwepo wa kadi 426,757 zenye thamani ya Sh3.4 bilioni ambazo zimeharibika na hazifai kwa matumizi ya kutengeneza vitambulisho vya Taifa.
CAG Charles Kichere katika ripoti hiyo ya Ukaguzi wa Serikali Kuu alibaini kuwa muda wa mkataba wa mtoa huduma wa kadi hizo zenye kasoro ulikuwa umeisha tokea miaka mitatu nyuma (Machi 14, 2018), ikiwa ni moja ya kasoro za kitendaji zilibainishwa kutoka katika taasisi hiyo.
Mapungufu kama hayo yanayojitokeza kwenye taasisi hiyo ndiyo yamekuwa yakiwachelewesha watu kupata vitambulisho vya Taifa na hivyo kuwakosesha baadhi ya huduma kwenye jamii.
Katika mwaka wa fedha wa 2021/22, Wizara ya Mambo ya Ndani inatarajia kutumia Sh939.1 bilioni, kati hiyo hizo Sh27.5 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Latest
