Fahamu kuhusu udalali na jinsi ya kujisajili kielektroniki
- Mwombaji atatakiwa kulipia Sh150,000 ili kupata kibali kwa kipindi cha mwaka mmoja au nusu mwaka kwa Sh75,000.
Arusha. Udalali ni miongoni mwa shughuli ya kiuchumi inayowaingizia kipato mamia ya Watanzania hususani waishio maeneo ya mijini ikimuunganisha mnunuzi na muuzaji wa bidhaa au huduma kwa lengo la kusaidia mchakato wa uuzaji au ununuzi.
Kazi hiyo ni muhimu katika shughuli kama uendeshaji wa minada ya hadhara, uuzaji wa mali zilizotaifishwa, udalali wa mali isiyohamishika kama nyumba na viwanja, kukusanya madeni au ushuru kwa niaba ya taasisi fulani na udalali wa kisheria wa mali zinazouzwa kwa amri ya mahakama.
Licha ya umuhimu wa kazi hiyo katika jamii, baadhi ya watu huifanya kiholela bila kujisajili jambo linaloweza kuleta hatari mbalimbali ikiwemo za utapeli.
Kwa kufahamu umuhimu huo, Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeanzisha mfumo mpya wa kielektroniki wa utoaji wa leseni za udalali na uendeshaji minada unaojulikana kama GAMIS Portal.
Mfumo huo unatajwa kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo ambayo awali ilikuwa ikipatikana kwa shida na gharama kubwa kwa waombaji walioko mikoani kutokana na umbali na mlolongo wa kupata kibali makao makuu.
“Mfumo wa GAMIS Portal, umetengenezwa kwa lengo la kuondoa urasimu na kuwapa urahisi zaidi wananchi wanaohitaji leseni za udalali kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa Sheria ya Waendesha Minada (Auctioneer’s Act 1928, Cap 227 R.E 2002)” imesema taarifa ya Wizara ya Fedha iliyotolewa leo Septemba 18, 2025.
Hatua za kujisajili na kuomba leseni ya udalali
Wizara ya Fedha imebainisha kuwa mwombaji anapaswa kupakua fomu ya maombi kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha (www.mof.go.tz) kupitia GAMIS Portal kisha kujaza kikamilifu nyaraka za maombi na baadae kuziwasilisha kwa Katibu Tawala wa Wilaya anayotokea mwombaji kwa ajili ya uhakiki na sahihi.
Mwombaji anatakiwa kuandaa na kuambatisha nyaraka muhimu kikiwemo Cheti cha uthibitisho wa kulipa kodi (Tax Clearance) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Cheti cha Usajili wa Kampuni kutoka BRELA na Leseni ya Biashara kutoka Halmashauri au Manispaa.
Nyaraka hizo zinapaswa kuskaniwa na kupakiwa kwenye mfumo kabla ya kutuma maombi rasmi kwa kuchagua kitufe cha ‘Add Auctioneer Licence’ na kuambatisha mafaili husika na kubonyeza kitufe cha hifadhi
Ili kukamilisha usajili wa leseni hiyo muombaji atatakiwa kulipia Sh150,000 ili kupata kibali kwa kipindi cha mwaka mmoja au nusu mwaka kwa Sh75,000 ambazo hutumika katika minada ya hadhara, ukusanyaji wa madeni, ushuru, tozo mbalimbali na uuzaji wa mali kama nyumba na viwanja.
Latest