Jinsi ya kupata Pasipoti ya kusafiria
- Ni muhimu mwombaji ahakikishe ana viambata vyote hitajika wakati wa kufanya maombi ikiwemo cheti cha kuzaliwa na kitambulisho cha Taifa.
- Gharama ya maombi ni Sh150,000 na vizuri mwombaji kufuatailia maombi yake mwenyewe bila kutumia vishoka.
Dar es Salaam. Huenda ukawa una ndoto za kusafiri kwenda nje ya Tanzania na hujui ni jinsi gani unaweza kupata Pasipoti ya kusafiria. Ndoto hizo yawezekana ni kwa ajili ya shughuli za kibiashara, kimasomo au hata kwa ajili ya kutalii.
Pasipoti ya kusafiria ni hati rasmi ya utambulisho wa kimataifa inayotolewa na Serikali ya Taifa fulani kwa raia wake, inayomruhusu kusafiri kwenda nje ya nchi na kurejea nyumbani kisheria.
Utambulisho huu unamsaidia raia kufanya shughuli rasmi zilizompeleka mahali husika bila kizuizi na hata kupatiwa msaada pale inapohitajika.
Kwa Tanzania, Pasipoti hutolewa na Idara ya Uhamiaji.
Viambata muhimu kwa ajili ya maombi
Kabla ya kuanza mchakato wa maombi ya pasipoti ni lazima mwombaji ahakikishe ana viambata vyote hitajika wakati wa kufanya maombi.

Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, mwombaji anatakiwa kuwa na Raia wa Tanzania mwenye Cheti cha Kuzaliwa, Cheti au Kiapo cha kuzaliwa mzazi wa mwombaji, Kitambulisho cha Taifa, picha ya mwombaji iliyopigwa siku za karibuni yenye kivuli cha rangi ya buluu isiyokoza, ushahidi wa safari au ushahidi wa shughuli anayofanya mwombaji, bila kusahau barua ya utambulisho kutoka Serikali za Mtaa anakoishi mwombaji.
Hatua kwa hatua jinsi ya kufanya maombi
Mchakato wa maombi ya pasipoti unanzia kwenye tovuti ya idara ya uhamiaji, www.immigration.go.tz ambapo ukishaingia katika tovuti hiyo unatakiwa kwenda katika kipengele cha huduma za uhamiaji ‘eservice’.
Bofya kitufe kilichoandikwa ‘Fomu ya Maombi ya Pasipoti’ na kufuatia kitufe kilichoandikwa ‘Ombi Jipya’.
Mfumo wa uhamiaji utakupeleka kwenye kurasa ambayo unahitajika kujaza taarifa muhimu ikiwemo taarifa zako binafsi, taarifa za wazazi, dhumuni la kusafiri, watu wa dharula na kuambatanisha viambata vinavyotakiwa kwenye mfumo wa uhamiaji.
Mara baada ya kujaza taarifa hizo, mwombaji anatakiwa kuhakiki tena taarifa hizo na kuthibitisha kuwa taarifa zote zilizojazwa ni sahihi na baada ya kufanya hivyo utapewa namba za kumbukumbu ya malipo na utalipia kiasi cha Sh20,000.

Hata hivyo, katika hatua hii ni muhimu kuhakikisha taarifa zilizojazwa zinafanana na zile zilizoko kwenye kitambulisho cha Taifa na cheti cha kuzaliwa, kwani ikiwa mwombaji atakosea hata herufi moja ya jina basi atafanya mchakato kuwa mrefu zaidi.
Ukishalipia kiasi cha Sh20,000 fomu ya maombi itakuwa tayari kupakuliwa.
Baada ya kupakua, mwombaji anatakiwa kuichapisha ambapo wadhamini wawili watatakiwa kujaza na kutia sahihi kisha fomu kupelekwa kwa Wakili au Mwanasheria kwa ajili ya kuthibitishwa na kugongwa mhuri.
Kufikia hatua hii mwombaji atakuwa amefikia nusu ya mchakato wa maombi ya Pasipoti.
Zoezi la ujazwaji wa fomu likishakamilika, mwombaji anatakiwa kupeleka fomu hiyo akiambatanisha na viambata vyote hitajika nakala na halisi kwenda katika Ofisi za Idara ya Uhamiaji zilizoko karibu nae.
Ikiwa mwombaji anatarajia kusafiri siku za karibuni ama ameshakata tiketi, ni muhimu huambatanisha kwenye nyaraka, hii itasaidia ombi lake kufanyiwa kazi kwa haraka kulingana na dharula aliyonayo.

Mwombaji atafanyiwa mahojiano na maafisa uhamiaji na ikiwa kila kitu kipo sawa atapewa namba ya kumbukumbu ya malipo ambayo atahitajika kulipia kiasi cha Sh130,000.
Baada ya kufanya hivyo, mwombaji atapewa utaratibu kwa ajili ya kupigwa picha na kuchukuliwa alama za vidole, na maombi yake yatakuwa yamepokelewa.
Ikiwa hakutakuwa na jambo lolote la ziada mwombaji atasubiri mchatao wa ndani wa Idara ya Uhamiaji na Pasipoti yake ikishatoka, Idara itawasiliana nae kwa ajili ya kwenda kuichukua.
Huchukua muda gani hadi kutoka?
Kwa mujibu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, pasipoti hutoka siku tano za kazi baada ya ombi kukalimilika, kwa maombi yaliyowasilishwa Makao Makuu ya Uhamiaji, Dar es Salaam.
Lakini kwa waliowasilisha ofisi zilizoko mikoani, huchukua siku 10 za kazi, na siku 14 kwa maombi yanayotoka ofisi zilizoko nje ya Tanzania.
Kumbuka, malipo yote ya Pasipoti yanafanyika kupitia namba za kumbukumbu za malipo na si mkononi, na ni vizuri kufuatailia maombi yako wewe mwenyewe pasipo kutumia vishoka.
Latest