Serikali yatangaza ufadhili wa masomo ya kibingwa kwa kada ya afya

August 21, 2025 4:32 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Sh 9 bilioni yatengwa kufadhili wataalamu 300 katika mwaka wa fedha 2025/26.

Arusha. Serikali ya Tanzania imetangaza nafasi 300 za ufadhili masomo ya kibingwa kwa kada ya afya kupitia Mpango wa Ufadhili wa Masomo unaojulikana kama ‘Samia Health Super-Specialization Program.

Samia Health Super-Specialisation Program ni mpango maalum wa kutoa ufadhili wa masomo ya ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi unaosimamiwa na Wizara ya Afya kwa ajili ya kuwaendeleza watumishi wa sekta ya afya kusoma masomo ya kibingwa na kibobezi kwenye fani mbalimbali za afya zinazotolewa kwenye vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Taarifa ya Waziri wa Afya Jenista Mhagama, iliyotolewa leo Agosti 21, 2025 inabainisha kuwa dirisha la maombi ya ufadhili huo litafunguliwa kwa siku 23 tu kuanzia leo hadi Septemba 12, 2025 huku maombi yakitakiwa kuwasilishwa kwa njia ya kielektroniki.

“Dirisha la kutuma maombi ya ufadhili wa Samia Health Super-Specialization Program 2025/2026 limefunguliwa kuanzia tarehe 20 Agosti, 2025 hadi tarehe 12 Septemba, 2025…

…Maombi ya ufadhili yawasilishwe kwa njia ya kielektroniki kupitia tovuti https://esponsorship.moh.go.tz/ Aidha, nasisitiza kuwa maombi yatakayofanyiwa kazi ni yale yatakayowasilishwa kwa njia ya mfumo huo tu,” amesema Mhagama.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2025/26 Wizara imetenga Sh9 bilioni kwa ajili ya mafunzo ya wataalamu hao katika ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi katika fani mbalimbali za kipaumbele katika Sekta ya Afya.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kugharamia mafunzo kwa wataalamu bingwa na bobezi300  watakaokuwa wanaendelea na masomo pamoja na wapya watakaopata ufadhili kwa mwaka 2025/2026.

Ufadhili huo utasaidia  kuimarisha na kusogeza huduma bora za afya, kupunguza rufaa za matibabu nje ya nchi na hivyo kupunguza gharama kwa Serikali na wananchi pamoja na kuvutia tiba utalii,

Mhagama amebainisha kuwa wanufaika wanalipiwa ada na posho ya utafiti kwa wanaosoma vyuo vya ndani ya nchi na kwa wanaosoma nje ya nchi wanalipiwa ada, nauli, posho ya utafiti na posho ya kujikimu. 

“Malipo ya posho ya utafiti na posho ya kujikimu yatazingatia viwango vilivyopangwa na Wizara. Ufadhili huu sio mkopo ni ‘grant’ wanayopewa wanufaika kwa masharti maalum ya kuendelea kufanya kazi nchini baada ya kuhitimu,” amefafanua Mhagama.

Vigezo vya ufadhili

Wizara ya Afya imeainisha vigezo vya kupata ufadhili huo kuwa ni pamoja na mtumishi atakayeomba ufadhili kuwasilisha maombi kwa njia ya mfumo, awe raia wa Tanzania, mtumishi wa Serikali, awe na barua ya udahili kutoka kwenye chuo kinachotambuliwa na Serikali ndani au nje ya nchi na awe anakwenda kusoma fani za kipaumbele zilizoainishwa na Wizara. 

“Vile vile, ufadhili utazingatia uhitaji unaotokana na uhaba wa taaluma/fani kwenye kituo anachotoka mtaalamu. Kwa mantiki hiyo, kipaumbele cha kupata ufadhili kitategemea upungufu wa taaluma aliyoomba kwenda kusoma kwenye kituo chake cha kazi, sifa nyingine ni kama zilivyoainishwa kwenye tangazo la ufadhili litakalowekwa kwenye tovuti ya Wizara ya Afya,” ameongeza Mhagama.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW