Rais Samia amtwisha zigo bosi mpya Tanesco

May 24, 2025 2:43 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Amtaka kusimamia miradi ya umeme bila kuingiliwa na maslahi binafsi.
  • Ahimiza kuharakishwa kwa mradi wa uranium katika eneo la Tunduru.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo mahsusi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Lazaro Twange, akimtaka kwenda kusafisha “makandokando” katika shirika hilo muhimu katika uzalishaji wa nishati nchini. 

Katika hotuba yake wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi hao leo Mei 24, 2025 jijini Dar es Salaam, Rais Samia hakueleza kwa undani makandokando licha ya kumtaka Twange kusimamia mabadiliko ya kina ndani ya Tanesco. 

Tanesco, lililokuwa na mali zenye thamani ya zaidi ya Sh19.6 trilioni mwaka 2021/22, ni miongoni mwa mashirika ya umma muhimu zaidi katika kuchochea ukuaji wa uchumi nchini. 

Rais Samia amesema kuwa shirika hilo lina changamoto nyingi hasa katika usambazaji wa umeme, mfumo wa bili, na utekelezaji wa miradi ambazo zinahitaji usimamizi madhubuti na wenye nidhamu.

Viongozi wateule wakiapa kiapo cha maadili kwenye hafla ya uapisho iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam. Picha /Ikulu mawasiliano.

“Nilimwona Naibu waziri Mkuu (Dk Dotto Biteko) kaenda kazunguka hakufurahishwa na aliyoyakuta katika maeneo mengine nenda kasimame uyafanyie kazi,” amesisitiza Rais Samia.

Licha ya kuwa Rais Samia hakutaja kwa kina makandokando hayo ya Tanesco, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2023/24, ilionesha kuwa Tanesco ilikuwa miongoni mwa mashirika saba ya umma yaliyosababisha hasara ya jumla ya Sh966.42 milioni kutokana na mapato yaliyokusanywa kwa viwango visivyofaa.

Ripoti hiyo ilieleza zaidi kuwa wateja 7,056 waliendelea kutozwa kiwango cha chini cha matumizi (D1) licha ya matumizi yao kuwa juu ya kiwango hicho kwa zaidi ya miezi mitatu, hali iliyosababisha upotevu wa mapato wa Sh50.76 milioni  kutokana na udhibiti hafifu na ukosefu wa mifumo ya ufuatiliaji.

Baadhi ya viongozi wateule wakisaini kiapo katika hafla ya uapisho. Picha/ Ikulu Mawasiliano.

Rais Samia ameeleza kuwa miradi mingi ndani ya Tanesco imekuwa kivutio cha maslahi ya watu wengi na kumtaka kusimamia bila kujali maslahi ya watu binafsi. 

“Achana na “interest” (maslahi) za watu simamia sheria sera zako za shirika na miradi ilete faida kwa wananchi, hili ndio kubwa ninalolitegemea kutoka kwako,’’ amesisitiza Rais Samia katika hotuba yake.

Ataka umeme wa nyuklia

Rais Samia amewataka wasaidizi wake kusimamia ipasavyo rasilimali ya madini ya urani iliyopo ndani ya nchi, akieleza kuwa taifa lina uwezo wa kuzalisha umeme wa nyuklia kwa faida ya Watanzania.

“Siaminishwi kwamba umeme wa uranium ni hatari, nchi zilizoendelea wanatumia tena ni sehemu kubwa ya umeme wao. Sisi tuna ‘raw materials’ (malighafi) hapa, wanatuambia hatari ili wachimbe, wachukue waende kutengenezea kwao,” amesema Rais Samia.

Ili kufanikisha malengo hayo, amehimiza kuharakishwa kwa mradi wa uranium katika eneo la Tunduru mkoani Ruvuma ili taifa linufaike na rasilimali hiyo kabla haijasafirishwa nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks