Fahamu maana ya tarakimu kwenye namba ya NIDA
- Tarakimu hizo humuwezesha mhusika kufahamu anwani za makazi aliyopo.
Arusha. Licha ya kukamilika kwa zoezi la anwani za makazi nchini Tanzania, ni Watanzania wachache wanaofahamu anwani zao na jinsi ya kuzitumia pale inapohitajika.
Mwaka 2022 Serikali ya Tanzania ilianza rasmi zoezi la uwekaji wa anwani za makazi katika mikoa na wilaya zote nchini ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Posta ya mwaka 2003.
Sera hiyo inaelekeza kuwepo kwa anwani za kitaifa zitakazowezesha ufikishaji wa barua, nyaraka, vifurushi na vipeto majumbani na katika ofisi mbalimbali.
Jambo lisilofahamika na wengi ni kuwa unaweza kutumia tarakimu zilizopo katika namba ya Nida kufahamu anwani ya makazi ya eneo unaloishi ili iwe rahisi kupokea mizigo na vifurushi pale utakapohitaji.
Mratibu msaidizi wa mfumo wa anwani za makazi Arnold Mkude aliyekuwa akizungumza kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Bongo ameeleza kuwa kupitia namba za Nida mtumiaji anaweza kufahamu anwani ya makazi ya sehemu anayoishi.
“Kwenye kitambulisho cha Nida inaanza mwaka wako wa kuzaliwa mwezi, tarehen zile namba tano zinazofuata ni posticode na namba ya kwanza kwenye zile tarakimu tano inamaanisha kanda,” amesema Mkude.
Kwa mujibu wa Mkude kama kitambulisho chako ulikipata jijini Dar es Salaam namba ya kwanza itaanza na moja kwa sababu Dar es Salaam ni kanda namba moja.
Tarakimu ya pili inamaanisha mkoa, ambapo mkoa wa Dar es Salaam ni umepewa namba moja huku tarakimu ya tatu ikitumika kuashiria wilaya na zile mbili za mwisho zikimaanisha kata anayotokea mmiliki wa namba hiyo.
“Namba za mwisho zipo mbli kwa sababu wilaya zetu zina kata zaidi ya 10 kwa hiyo ndiyo maana namba mbili za mwisho ni za kata,” amesemsa Mkude.
Baada ya kufahamu kata , Mkude amesema unaweza kufahamu namba ya nyumba ya muhusika kwa kuangalia jina la barabara na namba za nyumba ambazo zinakuwa upande wa kulia na kushoto wa barabara.
Upande wa kushoto wa barabara huwekwa namba witiri ambazo ni 1, 3, 5, 7 na upande wa kulia huwekwa namba shufwa ambazo ni 2, 6, 8.
Hivyo ikiwa unatafuta nyumba namba 5 katika mtaa fulani ni lazima utaipata upande wa kushoto wa barabara.
Huenda utambuzi huu ukawapita Watanzania ambao hawajajisajili kupata vitambulisho au namba ya Nida licha ya umuhimu wake katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo kusajili laini za simu.
Hivi sasa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ipo katika kampeni maalum ya kuhakikisha Watanzania milioni 1.2 wanapata vitambulisho hivyo kufikia mwezi Februari mwaka huu sawa na agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani Innocent Bashungwa.