Rais Samia: Shule zizalishe wataalamu zaidi kuliko wasomi
- Azitaka shule kuzalisha wahitimu watakaoweza kuajirika na kujiajiri
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa shule nchini kujikita katika kuzalisha wataalamu wa kada mbalimbali ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira zinazotokana uwekezaji unaoendelea katika nyanja tofauti.
Kauli ya Rais Samia inakuja wakati ambao wadau wa elimu nchini Tanzania wamekuwa wakipigia chapuo mabadiliko ya mfumo na Sera ya Elimu nchini kwa kuwa hauwaandai wahitimu kujitegemea baada ya kumaliza masomo yao.
Hata hivyo, tayari Serikali imeshafanya maboresho ya Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 ambapo hivi sasa watafundishwa stadi za amali pamoja na masomo ya nadharia ili kuwaandaa kutotegemea kuajiriwa pekee wanapohitimu.
Rais Samia aliyekuwa akihutubia wakati wa kufungua Shule mpya ya Sekondari iliyopo Misufini, Bumbwini, Zanzibar, leo Januari 8, 2025 amesema maono ya Taifa ni kuhakikisha watoto wanapata elimu inayowatayarisha kuwa wataalamu wa fani mbalimbali, ili waweze kuchangia maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
“Hapa tulipofika bado tuna maono ya mbele, maono yetu ni kusomesha watoto wetu wawe wataalamu na sio tu wasomi. Unaweza ukawa msomi, lakini ulichokisoma hakikusaidii wewe wala Taifa. Ukiwa mtaalamu wa eneo fulani, utautumia utaalamu huo kujisaidia wewe na kusaidia Taifa lako,” amesema Rais Samia.
mwonekano wa Shule ya Sekondari ya Balozi Seif, kutoka kushoto ni jengo jipya liliozinduliwa, zikifuatiwa na Rais samia akiwa na wanafunzi ndani ya vyumba vya maabara na maktaba. Picha |Ikulu
Wakati wa hotuba yake ameeleza umuhimu wa shule na taasisi za elimu nchini kutayarisha vijana kwa soko la ajira, akisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika nchini unahitaji nguvu kazi yenye taaluma na ujuzi maalum.
Rais Samia ametolea mfano wa namna vijana wa Zanzibar walivyopishana na fursa ya ajira zaidi ya 400 zilizotokana na uwekezaji hoteli ya kimataifa iliyofunguliwa katika kisiwa cha Bawe kutokana na kukosa utaalamu wa ajira husika.
“Hiyo inatuambia hatujafanya kazi nzuri kuzalisha wataalamu katika sekta ya utalii…ile ni nafasi ya vijana wetu wa kizanzibar, lakini hatukupata sisi, wamepata vijana wa Kitanzania (bara),” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amehimiza shule na vyuo kushirikiana katika kutoa elimu ya vitendo na kuzalisha wataalamu wa sekta mbalimbali ambao wataweza kuajirika, akisisitiza kuwa lengo ni kuzalisha vijana wenye ujuzi wa fani mbalimbali, ambao wataweza kujiajiri au kushindana kwenye soko la ajira.
Ufunguzi wa Shule ya Sekondari aliyoipa jina la Balozi Seif iliyopo Misufini ni mojawapo ya hatua katika kuimarisha miundombinu ya elimu Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Mapinduzi ya mwaka 1964.
Hata hivyo, Rais Samia amewataka wazazi kusimamia wajibu wao kikamilifu kwa kuwahimiza watoto wao kuzingatia masomo na kuchangia michango midogo pale inapobidi, sambamba nakuwataka walimu na wanafunzi kuitunza miundombinu ya shule hiyo ya kisasa.