Sababu Mbowe kugombea tena uenyekiti Chadema

December 21, 2024 4:34 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema hawezi kung’atuka wakati chama hicho kikiwa kwenye mivutano.

Arusha. Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe amesema atagombea tena uenyekiti wa chama hicho kwa kuwa bado kipo kwenye mivutano.

Mbowe ametoa uamuzi huo ikiwa ni saa 48 tangu aombe kupewa muda wa kutafakari kuhusu hatma ya nafasi hiyo ya unyekiti aliyohudumu katika miaka 20 iliyopita.

Kwa maamuzi hayo Mbowe anakuwa mtia wa tatu katika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho akichuana vikali na Tundu Lissu pamoja na mgombea mwingine katika uchaguzi utakaofanyika Januari 2025.

Akizungumza na wanahabari pamoja na wanachama wa chama hicho leo Disemba 21, 2024 nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam Mbowe amesema kuwa alitamani sana kung’atuka katika nafasi hiyo lakini imeshindikana

“Nimetafakari kwa kina sana, nilitamani kuondoka lakini siwezi kuondoka katikati ya mivutano iliyopo, kwa hiyo Chadema nipo, nitakuwepo. Nitagombea,” amesema Mbowe. 

Kwa mujibu wa Mbowe miongoni mwa sababu zinazomfanya kugombea tena ni kuendelea kukipa nguvu chama hicho kuelekea kwenye uchaguzi mkuu huku kukiwa na changamoto za nyingi ikiwemo mifumo mibovu ya uchaguzi.

“Bado tuna matatizo mengi yanayohitaji ufumbuzi…tumeona uchaguzi wa juzi ulivyokuwa na mwaka ujao tuna uchaguzi, sisi Chadema tunasema ‘No reforms no elections’ tunaendelea kupambana na tutaendelea kudai katiba, mifumo huru ya uchaguzi na sheria za haki za uchaguzi,”amesema Mbowe.

Katika hatua nyingine Mbowe amewahakikishia wananchi kuwa chama hicho kitaendela kudumu hata akiondoka madarakani.

“Naona watu wengi wanapiga ramri Chadema inaenda kupasuka, inapasukia wapi? Huyu anayefikiria na kuiombea Chadema ife yeye siyo mwana Chadema…

…Hiki chama ni taasisi kamili hakitauwawa na Mbowe ama mtu mwingine yoyote kwa sababu hiki chama kimeenda zaidi ya kuwa chama cha Chadema na kuwa chama cha Watanzania.”amesema Mbowe.

Aidha, Mbowe amewataka wagombea wa uongozi wa ngazi ya Taifa ya chama hicho kufanya kampeni kwa haki na amani huku wakizingatia kukilinda kwani ni jukumu lao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks