Saa 48 kuamua hatma ya Mbowe kugombea uenyekiti Chadema
- Asema atatoa majibu juu ya kugombea kwake Jumamosi, Disemba 21, 2024.
- Akemea makundi na kujigawa kwa wanachama wa chama hicho.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe ameomba saa 48 kwa wanachama wake kutoa tamko juu ya hatima yake kugombea tena nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.
Mbowe ambaye amekuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa miaka 20 ametoa ombi hilo kwa wanachama na viongozi wa chama hicho waliokusanyika leo Disemba 18,2024 nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam wakishinikiza mwenyekiti huyo kugombea tena.
“Kuna watu wamenitisha hapa na kuniambia usiondoke bila kutoa jibu, sasa ndugu zangu msinipeleke hivyo, mimi naomba nimesikia rai yenu na nimesikia hisia zenu ninaomba mnipe masaa 48 …
…Leo ni siku ya Jumatano nipeni Alhamisi nipeni na Ijumaa, siku ya Jumamosi nitazungumza na waandishi wa habari saa tano asubuhi katika ukumbi huu huu.” amesema Mbowe.
Katika siku za hivi karibuni chama hicho kimekuwa katika vuguvugu la kisiasa linalochangiwa na uchaguzi mkuu wa ndani utakaofanyika January 2025 ambapo siku chache zilizopita aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) Tundu Lissu alichukua fomu ya kugombea uenyekiti.
Hata baada ya Lissu kuchukua fomu Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika aliweka wazi kuwa Mbowe bado hajachukua fomu na mpaka kufikia Disemba 16 mwaka huu ni wagombea wawili tu waliotia nia katika nafasi hiyo.
Aidha, Mbowe amekemea vikali vitendo vya baadhi ya wanachama kuunda makundi mbalimbali ndani ya chama, na kudai kuwa vitendo hivyo vinafanya chama kuwa na mgawanyiko na hivyo kurudisha nyuma shughuli na maendeleo ya chama.
“Sijapenda namna ambavyo makundi mbalimbali ndani ya chama chetu yanahasimiana kwa kukashifiana, kutukanana, kudhalilishana na zaidi kusema uongo,” amesema Mbowe.
Pia amewatoa wasiwasi wanachama kwa kuwaeleza kuwa hakuna aina yoyote ya matusi ama tuhuma na kashfa zozote ambazo zitamuondoa katika misingi ya uongozi wa chama au kumfanya atetereke kwa namna yeyote akiwa kama mwenyekiti wa sasa wa chama hicho.
“Hakuna idadi ya mishale na matusi inaweza ikaniondoa sentimita moja au milimita moja kwenye msimamo na msingi wangu wa kiuongozi” amesisitiza Mbowe.