Lissu: Sativa amenilipia fomu ya uenyekiti Chadema
- Asema ni kwa sababu ya mapambano yake ya kupigania haki kwa Watanzania.
Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu amechukua rasmi fomu ya kugombea uenyekiti wa chama hicho huku akibainisha kuwa amelipiwa gharama za fomu hiyo na mwanachadema Edgar Mwakalebela maarufu kama Sativa.
Sativa alikuwa Mkazi wa Mbezi wilayani Ubungo ambaye alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Juni 23, 2024 na kupatikana mkoani Katavi siku nne baadae akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili ambapo kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani Sativa alipatikana Juni 27, 2024 asubuhi katika Hifadhi ya Katavi.
Lissu aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Disemba 17, 2024 mara baada ya kuchukua fomu ya uenyekiti kwenye makao makuu ya Chadema Mikocheni jijini Dar es Salaam, amesema Sativa amefikia uamuzi huo kwa kuwa anaamini ataweza kupigania haki za Watanzania.
“Sativa amenipigia simu akaniambia naomba nikulipie hiyo fomu kwa sababu naamini kama ukiwa mwenyekiti wa hichi chama utafanya ile kazi ambayo inahitajika kufanyika katika nchi hii, na hiyo ni kupigania haki za Watanzania, kupigania Tanzania mpya itakayo hakikisha kwamba hatutekwi na kupotezwa,” amesema Lissu.
Lissu ameongeza kuwa yeye au wanachama wanaomuunga mkono kugombea uenyekiti wangeweza kulipia Sh1.5 milioni lakini fedha hizo hazitatumika kwa kuwa ameridhia ombi la Sativa.
Kwa mujibu wa Lissu, kwa sasa Sativa yupo uhamishoni kutokana na hofu ya uhai wake ambapo amekuwa akivishutumu vyombo vya dola kuhusika na zoezi la kutekwa kwake Juni 2024.
nje ya nchi kwa mujibu wa Lissu, ni miongoni mwa wahanga wa matukio ya utekaji ambayo yameripotiwa na Jeshi la Polisi.
Kiongozi huyo mwandamizi ndani wa Chadema aliwasili makao makuu ya chama hicho kuchukua fomu majira wa saa 06:15 mchana, ikiwa zimepita siku tano tangu alipotangaza rasmi nia ya kugombea nafasi hiyo ya juu zaidi ndani ya chama.
Jana Desemba 16, Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika alitoa tangazo la uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa chama hicho sambamba na kutoa utaratibu wa kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali zoezi zilizoanza kutolewa leo Desemba 17 ambapo mwisho wa kuzirudisha ni Januari 5, 2025 majira ya saa 10 jioni.