Chadema kufanya uchaguzi wa viongozi wake kitaifa Januari, 2025
- Wagombea wana takribani siku 19 kuchukua fomu na kurudisha.
- Tangazo laja siku nne tangu makamu mwenyekiti wa chama hicho kutangaza nia ya kuwania uenyekiti wa chama.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kimetangaza kuwa kitafanya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa chama hicho Januari, 2025 katika nafasi 23 zinazojumuisha nafasi ya uenyekiti.
Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Desemba 16 makao makuu ya chama hicho Mikocheni jijini Dar es Salaam amesema fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ngazi ya taifa zitaanza kutolewa kesho Disemba 17, kwenye ofisi za makao makuu ya chama, mabaraza, kanda, sambamba na ofisi za chama ngazi ya mikoa na wilaya.
“Mwisho wa kurejesha fomu ni Januari 5, 2025, saa 10 jioni katika ofisi za makao makuu ya chama, Mikocheni au katika ofisi za kanda anayotoka mgombea husika. Aidha wanaachama wanaogombea katika mabaraza ya vijana, wanawake na wazee watatakiwa kurejesha fomu hizo katika ofisi za makao makuu ya mabaraza ya chama Kinondoni au katika ofisi za kanda anayotoka mgombea husika” amesema Mnyika.
Tangazo hilo la uchaguzi wa chama hicho limekuja ikiwa zimepita siku nne tangu Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara Tundu Lissu kutangaza rasmi nia ya kugombea uenyekiti wa chama hicho akieleza kusukumwa na mabadiliko ya hali ya kisiasa, hitaji la mabadiliko pamoja na haki ya katiba.
Mwenyekiti wa sasa ngazi ya taifa, Freeman Mbowe bado hajatangaza iwapo atawania tena nafasi hiyo ambayo tayari amekalia kwa miongo miwili ambapo aliwaambia wanahabari hivi karibuni kuwa wanachama ndio watakaoamua.
Mnyika ameongeza kuwa Ili kupata fomu ya kushiriki kinyang’anyiro cha uchaguzi huo ujao, kila mgombea atalazimika kulipa gharama zinazoendana na nafasi anayolenga kuhudumu.
Mathalani nafasi ya mgombea wa uenyekiti ngazi ya taifa fomu yake inalipiwa Sh1.5 milioni, makamu mwenyekiti wa bara na visiwani Sh750,000 wakati fomu ya wajumbe 8 wa kamati kuu italipiwa Sh300,000.
Kwa nafasi ya Baraza la Wazee (Bazecha) gharama ya fomu nafasi ya mwenyekiti taifa ni Sh300,000, makamu mwenyekiti bara Sh150,000 sambamba na Zanzibar Sh150,000.
Katibu mkuu, manaibu bara na visiwani, na mweka hazina Sh150,000, wajumbe watano wa baraza kuu Sh100,000 na wajumbe 20 wa mkutano mkuu kulipia Sh50,000.
Fomu za Baraza la Wanawake (Bawacha) mwenyekiti taifa itapatikana kwa Sh300,000 wakati makamu mwenyekiti bara na visiwani, katibu mkuu, manaibu katibu mkuu bara na visiwani, mratibu wa uenezi na mwekahazina wakilipia Sh150,000.
Aidha, fomu ya mratibu wa hamasa itatolewa kwa Sh100,000 na wajumbe 20 wa mkutano mkuu kulipia Sh50,000.
Mnyika ametoa rai kwa wenye nia ya kugombea kuzingatia katiba, kanuni, maadili ya wanachama na viongozi sambamba na miongozo mbalimbali ya Chadema akiitaja ya taratibu za kuendesha kampeni za uchaguzi ndani ya chama (2012) pamoja na mwongozo wa chama dhidi ya rushwa wa 2012.