Zifahamu sifa za kujiunga na JKT
- Ni pamoja na kuwa na afya njema, akili timamu, na kutokuwa na alama yoyote ya michoro mwilini (Tattoo).
Dar es Salaam. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza nafasi za mafunzo ya kujitolea kwa vijana wote wenye sifa za kujiunga kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwa mwaka 2024.
Taarifa iliyotolewa jana Septemba 25, 2024, na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Kanali Juma Mrai, kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Brigedia Rajabu Mabele, imesema usaili utaanza Oktoba 1 hadi Novemba 3, 2024, kwa mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya JKT, ili vijana hao waweze kujiunga na jeshi hilo, wanapaswa kuwa na sifa mbalimbali ikiwemo kuwa raia wa Tanzania ambacho ni kigezo namba moja
Kwa vijana wenye elimu ya darasa la saba wawe na umri wa kuanzia miaka 16 hadi 18, na ni wale waliomaliza Elimu ya Msingi kuanzia mwaka 2021, 2022, 2023,ambao wanatakiwa kuwa na cheti halisi cha kumaliza elimu ya msingi.
Kwa vijana wenye elimu ya kidato cha nne, umri usiwe zaidi ya miaka 20, waliomaliza elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2021, 2022, 2023, na awe na cheti halisi cha kumaliza elimu ya sekondari (Secondary Leaving Certificate) na cheti halisi cha matokeo (Academic Certificate).
Aidha, awe na ufaulu wa daraja la kwanza hadi daraja la nne ambapo kijana mwenye Daraja la Nne awe na ufaulu wa alama kuanzia 26 hadi 32.
Kwa vijana wenye elimu ya kidato cha sita, umri usiwe zaidi ya miaka 22, waliomaliza elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2021, 2022, 2023, na awe na cheti halisi cha kumaliza elimu ya sekondari (Secondary Leaving Certificate) na cheti halisi cha matokeo (Academic Certificate) na awe na ufaulu wa kuanzia daraja la kwanza hadi la nne.
Kwa upande wa vijana wenye elimu ya stashahada, umri usiwe zaidi ya miaka 25, awe na vyeti vya sekondari na cheti cha chuo.
Vijana wenye elimu ya shahada, umri usiwe zaidi ya miaka 26 na awe na vyeti vya sekondari na cheti cha chuo.
Kwa upande wa vijana wenye elimu ya shahada ya uzamili, umri usiwe zaidi ya miaka 27 na awe na vyeti vya sekondari na cheti cha chuo.

Vijana wa JKT katika picha ya pamoja wakisikiliza maagizo. Picha|Kijiwe Forum
Hata hivyo, vijana wanaotarajia kujiunga kwenye mafunzo hayo pia wanapaswa kuwa na afya njema, akili timamu, na asiwe na alama yoyote ya michoro mwilini (Tattoo).
Pia awe mwenye tabia na nidhamu nzuri, hajapatikana na hatia mahakamani na awe hajawahi kufungwa.
Aidha anatakiwa kuwa na kitambulisho cha Taifa au namba ya utambulisho kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Sifa nyingine ya kujiunga na mafunzo hayo ni kuwa na cheti halisi cha kuzaliwa (Original Birth Certificate).
Sanjari na sifa hizo,muombaji asiwe ametumikia Jeshi la Polisi, Magereza, Chuo cha Mafunzo, au Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo, wala kuajiriwa na idara nyingine Serikalini.
Asiwe amepitia JKT katika operesheni za nyuma kwa kundi la kujitolea na kundi la lazima (mujibu wa sheria).
Asiwe anajihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya, bangi, na yanayofanana na hayo.
Aidha, JKT imetoa angalizo kuwa kijana atakayepatikana na nyaraka za kughushi atachukuliwa hatua kali za kisheria kulingana na taratibu zilizopo.