TLS yatoa rai Serikali kuheshimu haki Ngorongoro
- Yaitaka kurudisha huduma za jamii na vituo vya kusajili wapiga kura.
Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetoa rai kwa Serikali kuheshimu haki ya wananchi wa Ngorongoro na maeneo mengine kwa kuwarudishia huduma za jamii zilizositishwa.
Kupitia chapisho la TLS lenye kichwa ‘Taarifa kwa umma kuhusu wito wa wananchi wa Ngorongoro kutaka kuheshimiwa kwa haki zao’, wananchi hao wamelalamikia kuondolewa kutoka kwenye maeneo yao bila ridhaa na kusitishiwa huduma muhimu za kijamii kama shule, huduma za afya, na maji hali inayosababisha waishi kwenye mazingira magumu.
Rai ya TLS inatolewa ikiwa ni siku mbili baada ya kusambaa kwa picha na video kwenye mitandao ya kijamii zikionesha maandamano yaliyofanyika Agosti 18, 2024 ambapo mamia ya wananchi wa Ngorongoro walijitokeza kuwasilisha madai yao.
Kupitia tangazo la Serikali Na. 673 la Agosti 2, 2024, jumla ya kata 11, vijiji 25 na vitongoji 96 vya halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro vimefutwa kupitia amri inayojulikana kama Amri ya Marekebisho ya Amri ya Mgawanyo wa Maeneo ya Utawala katika Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) ya Mwaka 2024.
Kufutwa kwa usajili wa kata hizo kunawaondelea wakazi wote wanaoishi kwenye vijiji na vitongoji vyake kukosa nafasi ya kusajiliwa na kupiga kura, kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka 2024, pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025.
“Pia, vituo vya kujiandikisha kwa ajili ya kupigia kura ambavyo wanachi wa Ngorongoro wanalalamika kwamba havipo katika maeneo yao virudishwe ili wapate kuitumia haki yao ya kikatiba ya kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za mitaa uliopangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka 2024 pamoja na Uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2025,” imeeleza taarifa ya TLS.
Mgogoro wa ardhi Ngorongoro kati ya Serikali na wananchi umekuwa ukiendelea kwa zaidi ya miaka ishirini bila kupatiwa suluhu kutokana na ukinzani uliopo kati ya mahitaji ya ardhi na sera za Serikali zinazotaka kulinda ikolojia ya eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Baraza la Uongozi la TLS limeunda kamati maalum itakayosimamia na kufuatilia kwa karibu suala la Ngorongoro ili kupata ukweli kamili na kuhakikisha misingi ya sheria za nchi inafuatwa na haki za wananchi zinaheshimiwa.
Kwa mujibu wa aliyekuwa msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi tangu Serikali ilipoanzisha utaratibu wa kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro Juni 2022 ni wakazi 3,822 na mifugo 18,102 pekee ndiyo wamehama hadi kufikia Januari 17, 2024 kuelekea kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga, huku wananchi 100,015 sawa na asilimia 96 wakisalia.
Latest