Rais Samia awafuta kazi Nape Nnauye, January Makamba
- Ametua Silaa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari huku Deo Ndejembi akiteuliwa kuongoza ardhi.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewafuta kazi mawaziri waandamizi wawili wa Serikali yake usiku wa kuamkia leo akiwemo Nape Nnauye ambaye amekuwa akikosolewa vikali na wadau wa demokrasia baada ya kauli yake inayoelezea upatikanaji wa matokeo haramu katika uchaguzi.
Katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Rais Samia ametengua uteuzi wa January Makamba, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Nnauye aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Mawaziri hao wanafutwa kazi ikiwa ni mwaka mmoja umesalia kuelekea uchaguzi mkuu ambao Rais Samia anatarajia kutetea kiti chake kwa muhula wa pili baada ya kushika madaraka hayo kutokana na kifo cha mtangulizi wake, Dk John Magufuli Machi 17, 2021.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa usiku wa Jumapili, Rais Samia amewateua Jerry Silaa kuwa Waziri wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Deogratius Ndejembi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Kabla ya uteuzi huyo Ndejembi anayeenda kuchukua mikoba ya Silaa, alikuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

January Makamba, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni miongoni mwa mawaziri waliotenguliwa jana usiku na Rais Samia. Picha|Maktaba.
Mabadiliko ya lala salama
Katika mabadiliko hayo ya madogo ya baraza la mawaziri mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, Rais Samia amewateua Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ridhiwani Kikwete kushika nafasi aliyokuwa akiingooza Ndejembi.
Kabla ya uteuzi huo, Kombo alikuwa ni Balozi wa Tanzania nchini Italia wakati Kikwete alikuwa ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi wa Umma.
Aliyejiuzulu ubunge kupangiwa kazi nyingine
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Sharifa Nyanga ameeleza katika taarifa hiyo kuwa Cosato Chumi ameteuliwa kuwa Naibu Waiziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki akichukua nafasi ya Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye jana aliwasilisha barua ya kujiuzulu ubunge kwa Spika wa Bunge kutokana na sababu za “kijamii”.
Hata hivyo, Ikulu imeeleza kuwa Balozi Mbarouk atapangiwa kituo kingine cha kazi.
Wizara aliyekuwa akiiongoza Makamba imefumuliwa yote baada Rais Samia kumfuta kazi Stephen Byabato alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki na kumteua Dennis Londo kushika wadhifa huo.
Nape lilikuwa ni suala la muda
Kabla ya utenguzi wa Nape, mwanasiasa huyo alijikuta katika shinikizo kubwa la kujiuzulu na wadau wa demokrasia nchini baada ya kutoa kauli iliyoashiria kuwa huenda uchaguzi ujao usiwe halali licha ya jitihada za Rais Samia kuboresha mazingira ya kidemokrasia.
Nape alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya Habari akieleza kuwa Byabato ambaye ni Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM) asiwe na wasiwasi kwa kuwa uwezekano wa kushinda ni mkubwa sana inategemeana na mtu anayehesabu kura kwa kuwa huwa kuna kura “halali, nusu halali na haramu.”
“Matokeo ya kura sio lazima yawe yale ya kwenye boksi inategemea na nani anahesabu na kutangaza na kuna mbinu nyingi kuna halali, kuna nusu halali na kuna haramu na zote zinaweza kutumika ili mradi tu ukishamaliza unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe…kwa hiyo wanaotaka kushindana naye wajipange,” alisema Nape.
Baada ya kauli hiyo, Nape alikosolewa vikali katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari huku wengine wakieleza bayana kuwa alikuwa anakwamisha jitihada za Serikali ya Rais za kuboresha mazingira ya demokrasia nchini. Ikulu haikueleza bayana sababu za kutengua uteuzi wa Nape.
Nnauye, aliyeomba radhi baadaye akieleza kuwa ulikuwa ni utani, aliteuliwa na Rais Samia Januari 2022 kuongoza wizara hiyo akichukua nafasi ya Innocent Bashungwa. Hii ni mara ya pili ndani ya miaka 10 Nape anaeleza mbinu haramu za kushinda uchaguzi ikiwemo kauli yake maarufu ya “Bao la mkono”.
Habari za nyongeza na Fatma Amiry.