Watengeneza maudhui mtandaoni Tanzania kutozwa kodi ya asilimia 5
- Serikali yasema lengo ni kuongeza wigo wa kodi na kuzingatia kanuni za usawa za utozaji wa kodi.
- Hatua hiyo inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh968 milioni mwaka ujao wa fedha wa fedha wa 2024/25.
Dar es Salaam. Kama wewe ni mtengeneza maudhui mtandaoni mkaazi nchini Tanzania jiandae kuanza kulipa kodi ya asilimia tano ambayo Serikali imependekeza kuanza kutumika katika mwaka wa fedha wa 2024/25 unaoanza Julai mosi.
Lengo la hatua hii ni kuongeza wigo wa kodi na kuzingatia kanuni za usawa za utozaji wa kodi, amesema Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 leo Juni 13, 2024 bungeni jijini Dodoma.
Dk Mwigulu amesema hatua hiyo inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh968 milioni mwaka ujao wa fedha wa fedha wa 2024/25.
Wakati huo huo, Waziri Mwigulu amependekeza kuweka takwa kwa raia wa kigeni (non-resident) kukusanya kodi ya zuio kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye malipo yanayofanywa kwenda kwa mtengeneza maudhui mkaazi (resident digital content creator).
“Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh675 milioni,” amesema Dk Mwigulu wakati hotuba yake iliyojaa sifa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa “amefanya makubwa”.
Kwa nyakati tofauti, wadau wa uchumi wa kidijitali nchini Tanzania wamekuwa na maoni tofauti kuhusu kodi ya maudhui yanayozalishwa mtandaoni huku baadhi wakidai kiwango cha mapato hayo ni kidogo hivyo kutoza kodi ni kuwaumiza vijana na wajasiriamali yaliojiajiri mtandaoni.
Soma zaidi:
- Bajeti ya Tamisemi yapaa kwa Sh336 bilioni
- Bajeti Wizara ya Madini yaongezeka, miradi ya maendeleo ikisuasua
- ACT Wazalendo waibua hoja nzito bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 2023-24
Waziri huyo pia amependekeza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye huduma ya data zinazotolewa mtandaoni (online data service).
“Mabadiliko haya yanaenda sambamba na kuweka tafsiri ya maneno online data services na kujumuisha huduma hiyo kwenye wigo wa utozaji wa huduma za kidijitali,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, hatua hiyo itasaidia kuongeza wigo wa kodi na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
Ikiwa Serikali itaanza kutoza kodi hiyo kwenye huduma ya data inatarajia kuongeza mapato ya kwa kiasi cha Sh16.4 bilioni katika mwaka ujao wa fedha.
Serikali inapendekeza kutoza Kodi ya Zuio kwa kiwango cha asilimia 3 kwenye mapato yatokanayo na uhamishaji au ubadilishanaji wa mali za kidijitali (digital assets).
Mabadiliko haya yanaenda sambamba na kuweka tafsiri ya maneno “mali za kidijitali”.
Waziri Mwigulu amesema mmiliki wa jukwaa au mtu yeyote atakayefanikisha zoezi la uhamishaji au ubadilishanaji, atawajibika kuwa wakala wa kukusanya kodi hiyo na kuiwasilisha kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Raia wa kigeni anayemiliki jukwaa linalotumika kufanikisha uhamishaji au ubadilishanaji wa mali za kidijitali, atapaswa kujisaliji chini ya mfumo uliopo wa simplified tax regime.
“Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh465 milioni,” amesema Dk Mwigulu.