ACT Wazalendo waibua hoja nzito bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi 2023-24

May 23, 2023 2:09 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Wasema kuna ucheleweshaji wa miradi ya ujenzi unaoiongezea Serikali hasara.
  • Watilia shaka ubia wa Serikali na sekta binafsi kwenye utekelezaji wa miradi.
  • Washauri iundwe tume teule kuchunguza madai ya ubadhirifu.

Dar es Salaam, Chama cha ACT- Wazalendo kimeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka na thabiti ili kuboresha utendaji kazi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ambao kimedai umekuwa ukisua sua katika baadhi ya maeneo na kuisababishia Serikali hasara.

Waziri Kivuli wa Miundombinu, Ujenzi na Reli, Mohamed Juma Mtambo aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Mei 23, 2023 katika ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam amebainisha kuwa baada ya uchambuzi wa bajeti ya wizara hiyo wamebaini mambo nane ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi.

Uchambuzi huo wa ACT unakuja ikiwa imepita siku moja tu baada ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kuomba kuidhinishiwa Sh3.5 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za wizara hiyo kwa mwaka 2023/24.

Ucheleweshaji na Kuongezeka gharama kwa mradi wa Reli ya kisasa (SGR)

ACT imebainisha kuwa kumekuwa na ucheleweshaji wa kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa reli ya SGR unaosimamiwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC), jambo lililosababisha Serikali kupata hasara. 

Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, kipande cha Dar es Salaam- Morogoro ambacho kilipangwa kukamilika Novemba Mosi 2019 bado hakijakamilika ambapo kimesogezwa mbele kwa siku 1,414 na kuisababishia Serikali hasara ya Sh25 bilioni.

“Mradi huo uliongezwa muda wa kukamilika mara saba zaidi, na kuongeza siku 1,414 hadi muda wa kukamilika, sawa na miaka 3.8. Ila hadi sasa bado ujenzi haujakamilika kwa muda uliopangwa hii imepelekea kuongezeka kwa gharama ya zaidi ya Sh25 bilioni ambazo ni Dola za Marekani milioni 11.32,” amesema Mtambo.

Aidha Mtambo amebainisha kuwa kumekuwepo na ongezeko la fedha katika ununuzi wa vichwa vya treni kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi na  Mdhibiti Mkuu wa hesabau za Serikali (CAG) ya mwak 2021/22 kinyume na taratibu huku pia TRC ikishutumiwa kufuata masharti ya benki ya Standard Chartered katika kupata mkandarasi na kusababisha Serikali kupata hasara ya zaidi ya Sh1.7 trilioni.

“ACT Wazalendo tunaendelea kusisitiza wito wetu kwa Bunge la Tanzania kuunda Kamati teule ya Bunge kufanya uchunguzi wa kina wa masuala haya matatu yaliyoibuliwa na CAG katika taarifa yake ya mwaka huu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa hoja hizi ni nzito sana na hazipaswi kusubiri utaratibu wa kawaida,” amesisitiza Mtambo, Magomeni jijini Dar es Salaam.

Waziri Kivuli wa Ujenzi, Miundombinu na reli akizungumza na wanahabari katika ofisi za chama hicho Magomeni jijini Dar es Salaam.PichalEsau Ng’umbi

Ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) una walakini

ACT Wazalendo imedai kuwa uamuzi wa Serikali kuihusisha sekta binafsi katika ujenzi wa miradi yake hautakuwa na tija bali unaongeza gharama kutokana na matarajio ya faida na pia ni njia ya Serikali kuficha deni la Taifa.

Mtambo amebainisha kuwa kutokana na gharama za mtaji pamoja na matarajio ya faida miradi hii inapokamilika huwalazimisha wakazi wa maeneo husika kutozwa ili wanufaike nayo akitolea mfano daraja la Kigamboni.

“Miradi itakayojengwa kwa mtindo huu inakuja na tozo, makato na kodi kwa watumiaji ili kupata mapato na faida kwa aliyewekeza jambo linaloweza kuwaondoa wanachi wasioweza kumudu gharama hizo kutumia miundombinu hiyo au kuanzisha bughudha katika kutumia kwake,” amesema Mtambo.

Katika mpango wa bajeti ya mwaka 2023/24  baadhi ya miradi inayokusudiwa kutekelezwa kwa njia ya PPP ni pamoja na  mradi wa reli ya Mtwara – Mbambabay pamoja na  Barabara ya Chalinze hadi Morogoro.


Zinazohusiana


Kutokana Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kujiendesha kwa hasara, ACT imeshauri Serikali kulipatia shirika hilo ndege ambazo huwa inakodi kutoka kwa Wakala wa ndege za Serikali ili kupunguza gharama za uendeshaji na CAG afanye ukaguzi maalum kuhusiana na manunuzi ya ndege hizo ili kubaini kama kuna mapungufu yalitokea.

Msongamano katika bandari ya Dar es Salaam

Ili kukabiliana na msongamano wa magari katika bandari ya Dar es Salaam, chama hicho kimeshauri wadau wote wa bandari kuunganishwa kwenye mfumo unaotumiwa bandarini hapo ili kurahisisha upakiaji na upakuaji mizigo pamoja na kuziboresha bandari za Tanga, Mtwara pamoja na Lindi.

Mashaka ya ubora mradi wa mabasi yaendayo haraka 

Kwa mujibu wa Mtambo, uchambuzi iliofanywa na ACT Wazalendo umebaini kwamba mradi wa mabasi yaendayo haraka wa awamu ya pili (CBD – Mbagala, Km 20.3 na (CBD – Gongolamboto km 23.33) ni miongoni  mwa miradi inayotekelezwa kwa kiwango cha chini kabisa kutokana na hoja zilizoibuliwa katika ripoti ya CAG.

“Hoja alizoziibua CAG zinaonyesha wazi wazi harufu ya ubadhirifu na au uhujumu wa mradi. Kwa kuwa mradi huu ni mkopo ambao utalipwa na kila Mtanzania awe wa Dar es Salaam au nje ya Dar es Salaam tuna mashaka kuwa barabara nzima itakuwa mbovu na hata kusababisha maafa kwa watumiaji,” amesema Mtambo.

Miongoni mwa mapungufu yaliyobainishwa kwenye ripoti ya CAG katika ujenzi wa kipande cha CBD-Mbagala ni pamoja na unene wa lami, viwango vya chini vya madaraja ya watembea kwa miguu na vizuizi vya ajali vya barabara ya juu ya Kilwa na Mandela.

Hoja nyingine zilizowasilishwa na ACT ni pamoja na kutokuwepo kwa gharama halisi za matengenezo ya vivuko na ucheleweshaji wa ukarabati wa vivuko ambapo wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kuchunguza upya zabuni ya MV Kigamboni ili kubaini kama hakuna ubadhirifu.

ACT wameishauri Serikali kuitupia macho sekta ndogo ya madereva ambao wamekuwa kiungo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi ndani na nje, hivyo ni vema wakashughulikia madai yao ikiwemo kuboreshwa kwa maslahi pamoja na usalama ili kuongeza morali ya kusukuma gurudumu la maendeleo.

Barabara za pembezoni zimulikwe

Wameitaka Serikali kuondoa matabaka nchini kwa kutekeleza miradi ya barabara za mijini pekee na kuziacha za pembezoni jambo linalokwamisha ukuaji wa uchumi.

Mtambo amesema kuwa miradi ya barabara ya  Soni-Bumbuli-Dindira-Kongowe yenye kilomita 74, barabara ya Mtwara-Newala-Masasi,  Barabara ya Likuyufusi-Mkenda kilomita 122.50, Nachingwea-Liwale kilomita 130, na Nangurukuruku-Liwale kilomita 210 imekuwa ikitengewa bajeti kila mwaka bila utekelezaji wowote.

“ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuchukua hatua stahiki na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika haraka iwezekanavyo ndani ya muda uliotolewa ili kuondoa mateso kwa wananchi na kuchagiza maendeleo ya watu wanaoishi pembezoni,” amesema Mtambo.

Enable Notifications OK No thanks