Watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) walia na usalama wao kuelekea uchaguzi Mwanza
- Wasema ni kipindi ambacho kinawakosesha usingizi
- RPC Mwanza aahidi ulinzi kwao, awataka askari kata kutambua maeneo yenye walemavu hao.
- Awashauri kutoa taarifa haraka wanapohisi mienendo ya kutia shaka.
Mwanza. Watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani Mwanza wameliomba Jeshi la Polisi mkoani humo kuimarisha ulinzi kwao hususani kipindi hiki cha chaguzi ambapo matukio mengi ya uhalifu dhidi yao ikiwemo kuuawa na kukatwa viungo vya miili yao hutokea.
Baadhi ya walemavu waliokuwa wakizungumza kwenye kikao kilichowakutanisha pamoja Wakaguzi wa Kata kutoka jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela na maofisa ustawi wa jamii leo Mei 14, 2024 wamesema miaka ya uchaguzi ni miongoni mwa vipindi wanavyovihofia maishani mwao.
“Kipindi cha uchaguzi ndio kipindi ambacho kinatupa shida hata ukilala unalala kwa shida sana, hasa kwa mkoa huu ambapo matukio ya watu kuuawa hutokea kwa wingi,” amesema Mhoja.
Soma zaidi: Elimu ya Veta inavyowainua walemavu wa akili Tanzania
Mwalimu Mashine Matuju ambaye naye ni mlemavu wa ngozi ameongeza kuwa watoto ndio huathirika zaidi na matukio ya kihalifu dhidi yao, wakifuatiwa na wanawake ambao wengi wao hukimbiwa na waume zao.
“Maeneo ya vijijini ndio waathirika zaidi kwakuwa huko miundombinu ni mibovu, barabara, hakuna umeme hivyo ni wajibu wa polisi na viongozi wengine kushirikiana kuwatambua watu wenye ulemavu kwenye maeneo yao ili waweze kuwa salama,” amesema Mwalimu Matuju.
Mwenyekiti wa Chama Cha Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Mwanza, Masumbuko Marco amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kuheshimiwa na kulindwa ni sawa na Watanzania wengine hivyo jamii inapaswa kuwa mstari wa mbele kuwawezesha kupata haki zao kikamilifu.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amewaagiza wakaguzi wa kata mkoani humo kuhakikisha wanasimamia usalama kwenye kata zao pamoja na kuyatambua maeneo wanayoishi watu wenye ualbino na kusimamia mashauri yao mahakamani.
“Kikao hiki ni muhimu kwa sababu katika maeneo yao zipo kamati za usalama watakapoenda kukaa kwenye vikao hivyo agenda namba moja iwe ni kuhakikisha mnazungumzia suala la ulinzi na usalama kwa watu wenye ulemavu wa ngozi,” amesema Mutafungwa.
Aidha, Mutafungwa amewashauri watu wenye ulemavu wa ngozi mkoani humo kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama mara moja pale wanapohisi mambo yasiyo ya kawaida kwenye jamii zao ili hatua za haraka zichukuliwe.
Latest



