Dk Biteko awataka Makatibu Mahsusi kujiendeleza kitaaluma
- Asema kujiendeleza kitaaluma kutawawezesha kuendaana mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Mwanza. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametoa wito kwa makatibu mahsusi nchini kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia sambamba na kuboresha utendaji kazi wao.
Dk Biteko aliyemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kufungua Mkutano wa 11 wa kitaaluma wa Makatibu Mahsusi leo Mei 23, 2024 jijini Mwanza amesema ni ngumu kwa watumishi hao kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia bila kuwa na elimu.
“Kama mnavyofahamu kuwa dunia ya leo ni kijiji kutokana na mabadiliko ya teknolojia na utandawazi ambayo kwa kiasi kikubwa yanachochea maendeleo ya teknolojia hususan Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)…
…Hivyo ni jukumu lenu kama chama cha kitaaluma kuwa na mkakati wa kushawishiana kujiendeleza kitaaluma kwenda sambamba na mabadiliko hayo” amesema Dk Biteko.
Soma zaidi:Viwanja Afcon vyaongeza bajeti ya michezo mara nane Tanzania
Amesema mfumo wa kisasa wa matumizi ya kompyuta na vishikwambi ambao kwa pamoja unarahisisha utendaji kazi zao na ni jukumu lao kama waandishi waendesha ofisi kuhakikisha kuwa wanabobea katika fani hii na matumizi ya vifaa hivi kwenye kada yao.
DK Biteko pia amewataka makatibu mahususi hao kusaidia wengine katika kutatua changamoto mbalimbali katika maeneo yao ya kazi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema kuwa Serikali imefanya maboresho kadhaa katika kada ya makatibu mahsusi kwa lengo la kuboresha taaluma hiyo nchini.
“Mwanzoni kabisa taaluma hii ilikuwa inaitwa uhazili na kada yao hawa walikuwa wanaitwa makatibu mahsusi, tangu mwaka jana muundo umebadilika na sasa kwa kada yao wanaitwa waandishi waendesha ofisi na kiutumishi wamepanda kwa ngazi ya mshahara hadi kufikia TGSH hivyo maafisa hawa sasa wanasoma kufikia shahada hadi ngazi ya ubobevu,” amesema Simbachawene.

Makatibu Mahsusi wakiwa kwenye mkutano wa pamoja uliofanyika Jijini Mwanza. Picha na Mariam John/ Nukta
Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA), Zuhura Maganga amesema lengo la mkutano huo ni kudumisha taaluma, kukuza uwajibikaji, kuipa hadhi taaluma yao, kuboresha maslahi yao pamoja na kutoa huduma bora kwa waajiri na wananchi.
Ametaja baadhi ya mafanikio ya chama hicho kuwa ni kuishawishi Serikali kuanzisha shahada ya uzamili katika Chuo cha Uhazili Tabora na Chuo cha Utumishi wa Umma pamoja na kuboresha muundo wa maendeleo wa kada ya waandishi waendesha ofisi hadi kufikia daraja la afisa mwendesha ofisi mkuu.