Neema au hasara? Wakulima watakiwa kujipanga mvua za masika Tanzania

February 18, 2021 2:31 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Watakiwa kulima mazao yanayostahimili mvua kuwa ili kuongeza uzalishaji.
  • Mvua hizo ni mahususi kwa mikoa inayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka.
  • Mamlaka pia zatakiwa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kuepusha maafa.

Dar es Salaam. Wakulima wanaoishi katika mikoa inayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka wametakiwa kulima mazao yanayostahimili mvua nyingi ili kuongeza uzalishaji huku mamlaka husika zikikumbushwa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wakati mvua za masika zikianza. 

Msimu wa mvua za masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).

Maeneo mengine yanayopata aina hizo za mvua ni ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.  

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk Hamza Kabelwa akitoa taarifa ya mwelekeo wa msimu wa mvua za masika katika kipindi cha Machi hadi Mei 2021 amesema maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Ziwa Viktoria yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. 

Maeneo ya pwani ya kaskazini yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Msimu wa mvua za masika unatarajiwa kuambatana na vipindi vya mvua kubwa hususan katika kipindi cha mwezi Machi.

“Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na inavyotarajiwa katika kipindi chote cha msimu (wa masika), kwa ujumla mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka,” Dk Kabelwa ameeleza wanahabari jijini Dar es Salaam. 

Mambo wanayotakiwa kufanya wakulima

Kutokana kuwepo kwa mvua katika maeneo hayo, wakulima wanatakiwa kujipanga kuzitumia ili kuongeza uzalishaji kwa kulima mazao yanayostahimili mvua nyingi yatakayowasaidia kupata kipato kwa ajili ya kuendesha maisha.

Lakini mvua hizo zinaweza kuathiri baadhi ya mazao kwa sababu hali ya unyevunyevu wa udongo na maji ya kutosha inatarajiwa. 

“Hali  hiyo ya unyevunyevu hususan katika maeneo ya ukanda wa ziwa Victoria na nyanda za juu kaskazini mashariki yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani, inaweza kuathiri ukuaji wa baadhi ya mazao yasiyohitaji maji mengi, kama vile mahindi, maharagwe na mazao ya mizizi,” amesema Dk Kabelwa.

Wakulima wanahimizwa kutafuta na kutumia ushauri wa wataalam wa kilimo ikiwa ni pamoja na maafisa ugani katika maeneo yao. 


Soma zaidi: 


Mtaalam huyo wa hali ya hewa amesema pia miundombinu ya usafirishaji inaweza kuathirika hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. 

“Mamlaka husika zinashauriwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuchukua tahadhari ya hali ya hewa inayotarajiwa katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali kama vile reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege,” amesisitiza. 

Katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, sekta ya usafirishaji hususan usafiri wa ardhini inaweza kunufaika kutokana na vipindi vya ukavu vinavyoweza kujitokeza. 

Pia wananchi wametahadharishwa juu ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika kipindi hicho vinavyoweza kuambatana na mafuriko na kusababisha uharibifu wa miundombinu, shughuli za kijamii kuathirika, upotevu wa maisha na mali.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW