Magari 10 yanayopendwa zaidi na Watanzania

June 18, 2021 9:24 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Toyota IST inashika nafasi ya kwanza kwa kupendwa. 
  • Asilimia 80 ya magari hayo ni ya kampuni ya kutengeneza magari ya Toyota.
  • Makampuni mengine ni Subaru na Nissan.

Dar es Salaam. Gari ni chombo muhimu cha usafiri lakini kulinunua inategemeana na mambo mbalimbali ikiwemo unene wa mfuko wako, mazingira ambayo utalitumia gari lako na pia kazi yake. 

Wengine huenda mbali zaidi na kuangalia matumizi ya mafuta ya gari hiyo kwa kuangalia ukubwa wa “CC” za gari hiyo.

Kwa lugha rahisi, “Cc” ni nguvu ya injini ambayo inapimwa kwa uwezo wa kutumia mafuta. Kadiri CC ya injini inavyokuwa kubwa ndivyo injini hiyo hutumia mafuta mengi zaidi. 

Kampuni ya nchini Japan ambayo inauza magari yaliyotumika, (second hand) ya SBT Japan imetoa orodha ya magari ambayo yananunuliwa na kutumiwa na Watanzania katika shughuli mbalimbali kwa mwaka 2021.

Hii ndiyo orodha ya magari 10 ambayo yanabamba zaidi Tanzania ambayo yamekuwa chaguo la Watanzania kutoka maeneo mbalimbali duniani:

10: Toyota Ractis

Kama wewe ni mtembezi, unaweza kukubaliana na mimi kuwa huwezi kumaliza siku nzima bila kuonana na gari hizi. 

Ractis ambayo injini yake ina ukubwa wa CC 1,290 inauzwa kwa bei tofauti tofauti kulingana na mwaka wa kutengenezwa na umbali ambao imetembelea.

Kwa makadirio, unahitaji Sh4.9 milioni kuagiza gari hiyo ikiwa fedha hiyo ni ya kulipia gari tu, nje ya gharama zingine ikiwemo usafiri na kodi.

Ractis inayokuja na siti tano, milango mitano na inatumia petroli imeshuka nafasi mbili kwa kununuliwa na Watanzania kutoka nafasi ya nane katika orodha iliyotolewa na SBT mwaka jana.

Ractis inayokuja na siti tano, milango mitano na inatumia petroli. Picha| Google Images.

09: Subaru Forester

Ikiwa imeshuka kutoka nafasi ya saba kwa mwaka jana, Subaru Forester imeendelea kusumbua mitaa ya hapa na pale nchini Tanzania.

Gari hiyo ambayo injini yake ina uwezo wa CC 1994, unaweza kuinunua kwa wastani wa Sh5.7 milioni nje ya gharama nyingine ikiwemo kodi.

Forester inakuja na siti tano na uwezo wa kufanya kazi kwa mfumo wa “4WD” yaani uwezo wa matairi yote manne kufanya kazi kwa wakati mmoja.

08: Toyota Corolla Spacio

Gari hii ilikuwa namba sita mwaka 2020 kwa kupendwa na Watanzania hadi kufikia mwezi wa sita mwaka huu huenda watu walipunguza kasi ya kuiagiza.

Spacio ambayo unahitaji walau Sh5.3 kuiagiza, ina injini yenye uwezo wa CC1490  inakuja na siti saba na hivyo kuwa miongoni mwa magari yanayoweza kukidhi mahitaji ya familia yenye watu wengi.

07: Nissan Dualis

Gari hii ni mpya katika orodha za SBT iliyotolewa mwaka huu. Sifa zake huenda ndiyo zimewavutia watu wengi na kupenyeza kwa mara ya kwanza katika orodha hiyo ya dhahabu.

Dualis ambayo itakuhitaji uwe na walau Sh7.8 milioni kuiagizia (nje ya kodi) ina injini yenye uwezo wa CC1190, siti tano na chaguo la kununua 2WD ama 4WD.

Gari hiyo inatumia nishati ya petroli na muundo wake kwa SBT unaanzia mwaka 2007-2011.

06: Toyota Corolla Rumion

Gari hii ilishika nafasi ya tisa mwaka jana hivyo kupanda hadi nafasi ya sita mwaka huu, ni dalili kuwa ni kipenda roho cha Watanzania wengi.

Ikiwa inahitaji walau Sh5.5 kuagiza, Rumion inayotumia petroli inakuja na siti tano na chaguo la 2WD ama 4WD.

Gari hii injini yake ina uwezo wa CC 1496 hadi CC 1797 muundo ukianzia mwaka 2007 hadi 2011.

Nisan Dualis Ni gari pekee kutoka kampuni ya Nissan iliyoingia kwenye orodha hii.Picha| Google Images.

05: Toyota Premio

Gari hii ni bingwa mtetezi kwani hata mwaka jana, ilishikilia namba hii hii. Premio ambayo bei yake ya makadirio ya kuagiza ni kuanzia Sh7.5 milioni huku uwezo wa injini yake ukiwa ni CC 1496 hadi CC 1998.

Premio inakuja na siti tano na milango minne.

04: Toyota Harrier

Ni ngumu kuishi Dar es Salaam na usipishane na gari hili. Mbali na ukubwa wake wa wastani, huenda muonekano wake pia ukawa ni chanzo cha kuwavutia Watanzania wengi.

Mwaka jana, Harrier ilishika nafasi ya tatu na huenda ikaendelea kubaki katika nafasi hiyo au ikapanda siku zijazo. 

Harrier inaambatana na injini yenye uwezo tofaauti tofauiti kuanzia CC1360 hadi CC2990 kulingana na mwaka iliyotengenezwa huku Sh12.2 milioni ikiwa ni bei ya makadirio ya chini ya kuagiza gari hiyo.

03: Toyota Crown

Kukatiza mitaa ya jiji la Dar es Salaam bila kuona vijana wakiwa na gari hii ambayo mwaka jana ilikuwa katika nafasi ya pili, ni ngumu.

Crown ambayo inahitaji kima cha chini cha Sh6.3 milioni bila kuhusisha kodi muonekano wake wa ndani ni kati ya vitu vinavyoipa gari hii upekee.

Huenda Watanzania wameiagiza sana kwa sababu injini yake ni ya CC 1988 hadi  CC 2997 kulingana na mwaka wa matengeenzo.

Ni vigumu kumaliza siku bila kuona gari aina ya Toyota IST ikikatiza katika barabara za ardhi ya Tanzania. Picha| Google Images. 

02: Toyota Alphard

Kwa mwaka jana, gari hii ilishika nafasi ya nne na mwaka huu imepanda hadi nafasi ya pili kudhihirisha inachangamkiwa zaidi na Watanzania.

Alphard yenye CC 2362 hadi CC 3,456, inaagiziwa kwa wastani wa kianzio cha Sh7.1 huku ikiambatana na siti nane.

Gari hiyo inafaa kwa matumizi ya familia na ofisi kwani ina nafasi kubwa na muonekano wa kifahari kwa aina ya gari za “mini van”.


01: Toyota IST

Kama wewe ni mdau wa usafiri wa kuagiza kwa njia ya mtandao, hautapinga nafasi ya IST katika orodha hii.

Kutokana na uwezo wake wa kutumia mafuta, IST imekuwa gari inayoagizwa na Watanzania wengi kwa ajili ya usafiri binafsi na hata kwa malengo ya kibiashara.

Gari hiyo ambayo uwezo wa injini yake ni kuanzia CC 1298 hadi CC 1,797 inaweza kuagizwa kwa Sh5.3 ikiwa bei hiyo ni nje ya kodi na gharama nyingine zitakazohusika.

Mwaka jana, Mratibu wa biashara za kimataifa wa kampuni ya SBT kutoka Japan Muzzamil Ihsan aliiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa orodha ya gari yanayopendwa na Watanzania hutolewa kwa mujibu wa taarifa za gari zilizoingizwa nchini Tanzania tangu kampuni hiyo ianze biashara na Tanzania 1993.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV