Yafahamu magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

September 2, 2022 7:12 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Magari hayo ni yale yenye injini ndogo ikiwemo Toyota IST, Vitz na Passo.
  • Matumizi ya mafuta hutegemea na umbali ambao gari linatembea barabarani.
  • Wamiliki washauriwa kukagua magari yao mara kwa mara.

Dar es salaam. Kufuatia kuendelea kupanda kwa bei ya petroli na dizeli nchini Tanzania, wadau wa masuala ya vyombo vya moto wamependekeza baadhi ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta kwa Watanzania ili kupunguza gharama za maisha. 

Kwa mujibu wa bei kikomo za mafuta kwa mwezi Julai 2022 zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) bei ya  petroli kwa Mkoa wa Dar es Salaam inauzwa Sh3,320 kwa lita kutoka Sh2,994 iliyokuwa ikitumika Juni.

Wakati Mafuta ya dizeli kwa Mkoa wa Dar es salaam yanauzwa Sh3,143 kwa lita, wakazi wa Ruberwa wilayani Kyerwa mkoani Kagera ndiyo watanunua petroli kwa bei ya juu kuliko maeneo mengine Tanzania. Kwa mujibu wa Ewura petroli katika eneo hilo inauzwa Sh3,458.

Kwa mafuta yanayopitia bandari ya Mtwara, petroli sasa inauzwa Sh3,205 ambapo imeongezeka kutoa Sh2,979 kwa lita huku dizeli ikiuzwa kwa Sh3,172 kutoka Sh3,165.

Bei za mafuta zimekuwa zikipanda kwa miezi ya hivi karibuni duniani kote kutokana na vita inayoendelea ya Urusi na Ukraine ambayo imetatiza mifumo ya usafirishaji wa bidhaa hiyo. Urusi ni miongoni wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani.


Zinazohusiana:


Kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, baadhi ya wamiliki wa magari wameacha kuendesha magari yao na kuanza kutumia usafiri wa umma au kutumia magari yao kwa safari za dharura. 

Kivyera Banduka, mkazi wa jijini Dar es Salaam anasema kwa sasa hatumii gari lake binafsi kwenda kwenye shughuli zake bali anatumia daladala kwa sababu hawezi tena kumudu gharama za mafuta.

“Mara  baada ya bei ya mafuta kupanda nimepitia wakati mgumu sana, imebidi nipaki gari, au kwa wiki naenda na gari mara moja wakati zamani nilikuwa naenda kazini  na gari kila siku,” anasema Banduka.

Suluhu ya kupanda kwa bei ya mafuta

Kutokana na athari za kupanda kwa bei ya mafuta nchini, wadau wa masuala ya vyombo vya moto wamependekeza Watanzania kugeukia baadhi ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta ili kuwapunguzia gharama za kununua nishati hiyo.

Benjamin Mkwizu ambaye ni  wakala wa uagizaji wa magari kutoka nchini Japan kupitia kampuni ya Kangee Motors iliyopo Mtaa wa Kinondoni Vijana jijini Dar es salaam anasema magari yanayotumia mafuta kidogo ni yale yenye injini ndogo (cc) likiwemo Toyota IST na Vitz. 

“Gari zinazotumia mafuta kidogo ni zile za kuanzia cc650 mpaka cc1490 ambapo tunaweza kutaja magari kama Passo, IST pamoja na Vitz. Unaweza kutumia wastani wa lita moja kwa kilomita 12 au 13,” amesema Mkwizu.

Mkwizu anasema utofauti wa matumizi ya mafuta hutegemea umbali ambao gari limetembea, hata kama mtu anatumia gari ndogo. 

Baadhi ya magari  yenye injini kuanzia  cc 650 mpaka 1490 ni  Mazda Carol,Suzuki Kei,Nissan Cube,Toyota BB, na Honda Fit,Toyota Passo, pamoja na Toyota Ractics,

Baadhi ya magari ambayo yanatumia mafuta kidogo ni pamoja na Passo na Vitz. Picha| Esau Ng’umbi.

Fundi magari yanayotumia mafuta ya petroli, Rashid Mrindoko amesema inaweza kuwa ni vigumu kutaja moja kwa moja magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta kwa sababu matumizi hutofautiana.

Mrindoko nasema kinachoamua gari litumie kiwango fulani cha mafuta ni uwezo wa injini pamoja na ukubwa au udogo wake.

“Inategemeana na uwezo wa injini ya gari (CC). Injini yenye cc ndogo, ulaji wake wa mafuta ni mdogo  kuliko yenye cc kubwa. Kwa mfano, gari aina ya Noah au Voxy injini yake ni kubwa zaidi na  inatumia mafuta mengi kuliko Toyota IST kwa sababu injini yake ni ndogo,amesema Mrondoko.

Mrindoko anapendekeza magari ambayo watu wanaweza kutumia wakati huu ikiwemo Toyota Ist,Vits,pamoja na Passo.

Vipi kuhusu wamiliki wengine wa magari

Njia nyingine inayoweza kutumiwa na wamiliki wa magari kupunguza gharama za mafuta ni pamoja kuweka mazoea ya kukagua gari mara kwa mara ili kubaini mapungufu na kutengeneza haraka na kutoacha gari ikiunguruma kwa muda mrefu.

“Jiwekee utaratibu wa kukagua gari yako, unapohisi mabadiliko muone fundi kwa ushauri au matengenezo. Kuna wakati pampu inaweza ikawa haijakaa sawa hivyo inachoma mafuta mabichi au nozeli zimetanuka kwa hiyo zinamwaga mafuta mengi,” amesema Mrindoko mwenye uzoefu wa takribani miaka 10 kwenye fani ya magari.

Fundi huyo anasema watumiaji pia wanapaswa kujiwekea utaratibu wa kukagua gari yao kabla hujaiwasha ikiwemo kuangalia maji na oili kama zipo za kutosha.

“Kisha washa gari na usikilize muungurumo ikiwa kuna mabadiliko yoyote basi muone fundi ili kutambua tatizo ni nini,” anasema fundi huyo na kubainisha tabia hizo husaidia kupunguza matumizi makubwa ya mafuta yasiyo ya lazima.



Enable Notifications OK No thanks