Wizara ya Afya: Hakuna wagonjwa wengi wa Corona Hospitali ya Rufaa Shinyanga
- Imesema taarifa zinazosambazwa ni za uongo.
- Yakanusha mitungi ya oksijeni kutokukidhi mahitaji ya wagonjwa.
Dar es Salaam. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema taarifa zinasambaa mtandaoni kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga imeelemewa na wagonjwa wa COVID-19 siyo za kweli.
Licha ya kutokuwepo kwa wagonjwa wengi, Imesema imejiridhisha kuwa siyo kweli mitungi ya oksijeni haikidhi mahitaji wa wagonjwa wa COVID-19 hospitalini hapo.
“Hii taarifa ni ya uzushi,” imesema Wizara ya Afya katika ukurasa wake wa Twitter leo Julai 11, 2021 ikitolea maelezo moja ya taarifa inayodaiwa kuwa ni ya upotoshaji katika mtandao huo.
Hii taarifa ni ya uzushi, Wizara imejiridhisha kuwa hakuna wagonjwa wengi wanaopelekea mitungi ya Oksjeni kutokukidhi mahitaji. pic.twitter.com/DurA8fTqur
— Wizara ya Afya Tanzania (@wizara_afyatz) July 11, 2021
Taarifa hiyo ya wizara imekuja baada ya kusambaa kwa taarifa hasa katika mtandao wa Twitter kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inakabiliwa na wagonjwa wengi wa COVID-19, jambo linalosababisha mitungi ya oksijeni kuwa michache.
Kujilinda na habari za uzushi, wananchi wanashauriwa kupata taarifa za Corona kutoka mamlaka za afya ikiwemo Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Hata hivyo, Serikali ya Tanzania imeendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa kunawa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Latest
