TCU yaacha maumivu vyuo vikuu, ikivifuta vituo viwili

September 26, 2018 12:53 pm · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yavifuta Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji cha Tabora (TEKU) na Kituo cha Msalato cha Chuo kikuu Mt. Yohana Tanzania  Dodoma (SJUT).
  • TCU yapiga pini vyuo vingine saba saba kudahili wanafunzi wapya kwa ngazi zote za masomo na katika programu.
  • Bodi ya mikopo yawahakikishia mikopo wanafunzi watakaohamishwa katika utekelezaji wa agizo la TCU.
  • Baadhi ya vyuo vyajipanga kuhamisha wanafunzi katika vyuo vilivyofutwa.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imevifuta vyuo viwili na kusitisha mafunzo katika vyuo vingine vitano na kuamuru wanafunzi wote wanaoendelea na masomo kuhamishiwa katika vyuo vingine nchini, uamuzi unaowaacha wanavyuo wa taasisi hizo katika sintofahamu ya mustakabali wa elimu yao.

Vyuo vilivyotangazwa kufutwa na TCU leo hii (Septemba 25, 2018) ni Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji cha Tabora (TEKU) na Kituo cha Msalato cha Chuo Kikuu Mt. Yohana Tanzania (SJUT) kilichopo mkoani Dodoma.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amevitaja vyuo  vitano vilivyoagizwa kusitisha mafunzo katika mwaka ujao wa masomo kuwa ni Chuo Kikuu cha Mlima Meru (MMU), Chuo Kikuu cha Bagamoyo (UoB) na Chuo Kikuu cha Eckernford Tanga (ETU) kilichopo mkoani Tanga.

Vingine ni Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta- Kituo cha Arusha (JKUAT- Arusha Centre) na Chuo Kikuu Kishirikishi cha Josiah Kibira (JOKUCo) kilichopo Bukoba mkoani Kagera.

“Vyuo hivi viko chini ya uangalizi maalum na hivyo haviruhusiwi kudahili wanafunzi wapya kwa ngazi zote za masomo (kuanzia astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu) kwenye programu zote za masomo,” amesema Prof Kihampa katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo. 


Saba vingine vyapigwa ‘pini’ kudahili ngazi zote

Sanjari na uamuzi huo, TCU imezuia vyuo vingine saba kudahili wanafunzi wapya kwa ngazi zote za masomo na katika programu vikiongozwa na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini (KIUT), Chuo Kikuu cha Marian (MARUCo), Chuo Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT) na Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU) kilichopo mkoani Mbeya.

Zuio hilo la TCU limevigusa pia Chuo Kikuu cha Marian (MARUCo, Chuo Kikuu Kikuu Kishirikishi cha Kumbukumbu ya Kadinali Rugambwa (CARUMUCo), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Sebastina Kolowa (Sekomu) na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania Kituo cha Mtakatifu Marko (SJUT – St Mark’s Centre kilichopo Buguruni jijini Dar es Salaam. 

Prof Kihampa amesema kuwa uamuzi huo umechukuliwa baada ya tume kufanya ukaguzi wa kawaida na wa kushtukiza katika vyuo hivyo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo na kubaini “changamoto mbalimbali zinazoathiri utoaji wa elimu bora katika baadhi ya vyuo”.

“Tume inawaarifu wanafunzi wote wanaotakiwa kuhama kuwasiliana na vyuo vyao kwa ajili ya maelekezo kuhusu taratibu za kuhama na vyuo wanavyotakiwa kuhamia,” amesema Prof Kihampa.

Baadhi ya viongozi wa vyuo hivyo wameeleza kuwa watafanya taratibu za kuwahamisha wanafunzi ili waendelee na masomo yao.


Zinazohusiana: Safari bado ndefu kufikia 50 kwa 50 elimu ya juu Tanzania

                         TCU wafungua dirisha dogo la usajili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu


SJUT kuhamisha wanafunzi wake

Makamu Mkuu wa SJUT, Profesa Emmanuel Mbennah ameiambia Nukta kuwa uamuzi wa kufunga kituo cha Msalato siyo wa TCU bali ulikuwa ni mchakato wa ndani ulioanzishwa na utawala baada ya kubaini kuwa kilikuwa hakikidhi vigezo vya ndani kutokana na kuwa na idadi ndogo ya wanafunzi.

“Seneti ilikaa na kuamua Msalato ‘centre’ (kituo) ifungwe na baadaye walipeleka ‘council’ (baraza) ikapitisha kwasababu kulikuwa na wanafunzi wachache na TCU waliridhia uamuzi wetu,” amesema Prof Mbenah.

Kituo hicho kwa mujibu wa Prof Mbena, kilikuwa na wanafunzi 23 tu wanaosomea masomo ya theolojia kinyume na matakwa ya TCU inayotaka kituo hicho kiwe angalau na wanafunzi 500.

Kutokana na hatua hiyo, Prof. Mbena amesema kuwa wanafunzi hao watahamishwa katika kampasi ya Chifu Mazengo iliyopo takriban kilomita sita na kituo hicho ili wakamalizie masomo yao huko akieleza kuwa ni vigumu kupata wanafunzi 500 kama zilivyo kozi nyingine kwa kuwa huusisha wanafunzi wenye wito na dini. 

Heslb yawapa matumaini watakaohamishwa

Hata wakati wanafunzi wa vyuo hivyo wakisubiri mustakabali wa kuhamishiwa taasisi nyingine, moja ya changamoto itakayowakabili ni uhamishaji wa mikopo yao ya elimu ya juu ambayo hutolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa HESLB, Veneranda Malima ameiambia Nukta kuwa wanafunzi hao hawatakiwi kuhofia kwa kuwa wataendelea kupata mikopo yao hata baada ya kuhamishiwa katika vyuo vingine.

Sisi hatuna shida tutatumia taarifa za uhamisho kutoka TCU na kuendeea kutoa mikopo kwa wanafunzi hao,” amesema Malima.

Nyongeza na Nuzulack Dausen.

Enable Notifications OK No thanks