Rais Magufuli ataja sababu za kuwafuta kazi Dk Tizeba, Mwijage

November 13, 2018 11:25 am · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kushindwa kwa baadhi ya taasisi zilizo chini ya wizara wanazoziongoza kutekeleza wajibu wao ipasavyo, ikiwemo kutafuta masoko na kupanga bei ya mazao ya wakulima.
  • Mawaziri wapya walioapishwa nao wapewa changamoto ya utendaji uliotukuka.

Dar es salaam Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuwafuta kazi mawaziri Dk Charles Tizeba wa Wizara ya Kilimo na Charles Mwijage wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, leo ametaja sababu za uamuzi huo ikiwemo kushindwa kuwajibika katika nafasi zao. 

Rais Magufuli alimteua Japhet Hasunga kuwa Waziri wa Kilimo akiziba nafasi ya Dk Tizeba huku nafasi ya Dk Mwijage ikichukuliwa na Joseph Kakunda.

Akizungumza leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha mawaziri hao wawili na manaibu mawaziri wanne, Rais Magufuli amesema alifikia uamuzi wa kuwafuta kazi Mwijage na Dk Tizeba kwasababu ya kutowajibika katika nafasi zao jambo lililoleta changamoto ya kuwahudumia wananchi hasa katika sekta ya kilimo na biashara.

“Katika majukumu haya hasa katika sekta ya kilimo na viwanda, sekta hiyo ni muhimu na nyeti kwa maendeleo ya watanzania. Mara nyingi nimekuwa nikigombana na Waziri Mkuu mbona huko mambo hayaendi vizuri, mbona hapa hapaendi vizuri kwasababu hawa mawaziri wote, yeye ndiye kiranja wao,” amesema Rais.

Rais Magufuli amebainisha kuwa hali hiyo imesababisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutimiza majukumu ya yaliyopaswa kufanywa na mawaziri hao na wakati mwingine kulazimika kumpigia simu usiku akihoji utendaji wa baadhi viongozi wa Serikali katika kushughulikia masuala muhimu ya maendeleo.


Zinazohusiana:   


Pia baadhi ya taasisi zilizo chini ya wizara hizo, zimeshindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo, ikiwemo kutafuta masoko na kupanga bei ya mazao ya wakulima.

Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Bodi ya Mazao Mchanganyiko ambayo kazi yake ni kupanga bei za mazao, bodi za pamba, korosho na tumbaku.

“Kuna bodi ya mazao mchanganyiko iko pale tangu enzi za baba wa Taifa jukumu lake ni kuregulate  kupanga) bei na kutafuta soko nje na kuuza mazao, kuna TANTRADE ambayo jukumu lake ni kutafuta biashara ya mazao hata madini, na bodi nyingine mbalimbali za mazao, bodi ya pamba, korosho, tumbaku zote zina wataalum wazuri sana, lakini linakofika suala la mazao ya watanzania hawashughuliki.

“Kwenye bajeti ya Malawi imetenga kiasi cha dola za Marekani 27.2 milioni fedha za kununua vyakula, bodi hizi zimefanya jitihada gani kwenda kutafuta soko, unapoona kuna kilio kikubwa waziri mkuu anaenda kutatuta, ninampenda sana Mwijage nampenda sana Tizeba lakini kwa hili hapana,” amesema Rais.

Mawaziri hao walishindwa kutatua changamoto ya bei ya kahawa ambapo baadhi ya wakulima walilazimika kusafirisha kimagendo zao hilo hadi nchi jirani ya Uganda ili kutafuta bei nzuri. 

Rais John Magufuli akimuapisha Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara leo Ikulu Jijini Dar es Salaam. Picha| Michuzi blog.

Eneo lingine ambalo Rais ameweka wazi ni kusuasua kwa mchakato wa usambazaji wa mbolea katika maeneo mbalimbali nchini mwanzoni  mwa mwaka huu na kusababisha usumbufu kwa wakulima ambao mazao yao yalianza kuharibika.

“Mtakumbuka hata wakati ule tunashughulikia mbolea kwenda kusini ilibidi yeye mwenyewe akamsimamie Mheshimiwa waziri (Dk Tizeba) na kuanza kusomba pale nilikuwa nimefikia top (juu) kabisa kwamba natoa siku saba hizi lakini bahati nzuri mbolea ikasombwa.

“Nikasema inawezekana wamejisahau nikwambia Waziri Mkuu wakumbushe mawaziri wako hizi kazi za uwaziri ni utumwa ni lazima tuwe watumwa wa watu hasa watu maskini,” amesema Rais.

Hakuishi hapo, ameongeza kuwa kutowajibika kwa mawaziri hao kumesababisha baadhi ya chai ya wakulima kuharibika ikiwa shambani kutokana na kiwanda cha chai cha Mbonde  kushindwa kufanya kazi kwa miaka nane, lakini alipoenda Waziri Mkuu alitatua changamoto iliyokuwepo.

Awali, akizungumza katika hafla ya uapishaji, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewapongeza mawaziri na manaibu waziri waliochaguliwa na kuwataka kufanya kazi kwa bidii katika maeneo yao ili waendane na kasi ya Serikali ya awamu ya tano. 

Hasunga na Kakunda watakuwa na kibarua kigumu cha kuzinyoosha wizara zao ikizingatiwa ni wizara nyeti zinazogusa moja kwa moja maslahi ya wananchi ambao wanategemea kilimo na biashara kuendeleza maisha yao.   

Naye Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema anaamini mawaziri waliochaguliwa watafanya kazi kwa weledi na kutimiza majukumu yao kwasababu ni wabunge ambao amefanya nao kazi kwa karibu wakati wa shughuli za bunge.

Enable Notifications OK No thanks