Sababu za Tanzania kutokuwa na mapato makubwa ya kodi
- Rais John Magufuli amesema hali hiyo inatokana na mapungufu yanayojitokeza katika mifumo na taratibu za ukusanyaji kodi ikiwemo wigo mdogo wa kulipa kodi usioendana na idadi ya watanzania.
- Amesema vyanzo vya ukusanyaji kodi havitumiwi vizuri jambo linalotoa mwanya kwa wafanyabiashara kukwepa kodi wakishirikiana na baadhi ya wafanyakazi wa TRA.
- Ameagiza kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kutengeneza mazingira ya ulipaji kodi, kupitia upya viwango vya kodi na taasisi za biashara na uwekezaji ikiwemo TPA na TIC kuondoa urasimu katika shughuli zao.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema Tanzania haifanyi vizuri katika ukusanyaji wa mapato ikilinganishwa na nchi jirani kutokana na mapungufu yanayojitokeza katika mifumo na taratibu za ukusanyaji kodi ikiwemo wigo mdogo wa kulipa kodi usioendana na idadi ya Watanzania.
Rais Magufuli amesema licha ya takwimu kuonyesha kuwa uchumi unakua kwa kasi na mfumuko wa bei kushuka mpaka asilimia tatu, bado ukusanyaji wa mapato hauridhishi na jitihada zaidi zinahitajika kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kulipa kodi ili kukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati.
Wizara ya Fedha na Mipango inaeleza kuwa makusanyo ya mapato yameongezeka hadi kufikia wastani wa Sh1.3 trilioni kwa mwezi tangu mwaka 2016 ukilinganisha na Sh850 bilioni iliyokuwa inakusanywa kabla ya ujio wa Serikali ya awamu ya tano.
Dk Magufuli, aliyekuwa akizungumza katika kikao kazi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wakuu na makatibu wa mikoa kinachofanyika Jijini Dar es Salaam leo (Desemba 10, 2018), amesema Tanzania yenye idadi kubwa ya watu kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki, ina dadi ya walipa kodi wapatao 2.27 milioni ambapo uwiano wa kodi ukilinganisha na Pato la Taifa (GDP) ni asilimia 12.8.
“Taxi base yetu ya makusanyo ni ndogo mno, ikiwa Msumbiji wako milioni 27, walipa kodi ni milioni 5.3. Sisi tuko milioni 55, walipa kodi ni milioni 2.2 lazima tufike mahali tujiulize, kwa hiyo utaona kwamba kuna mahali tumeshindwa,” amehoji Magufuli.
Rais John Magufuli akihutubia wakati wa kikao kazi cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wakuu na makatibu wa mikoa kinachofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Picha| Michuzi.
Sababu za Tanzania kuwa na uwiano mdogo wa walipa kodi
Rais Magufuli ameweka wazi kuwa hali hiyo inatokana na Tanzania kutotumia vizuri fursa ya vyanzo vya mapato vilivyopo katika kukusanya kodi ikiwemo sekta ya uvuvi katika bahari kuu, madini na uchimbaji wa gesi asilia.
Sababu nyingine ni kushindwa kama nchi kurasimisha sekta isiyo rasmi hasa wafanyabiashara wadogo na kuifungamanisha na sekta rasmi ili kuwatambua na kuwafikia walipa kodi katika maeneo waliyopo nchini.
Sekta isiyo rasmi, kwa mujibu wa Rais Magufuli, inakaribia kufikia asilimia 60 hadi 70 ambapo Serikali inakusanya mapato kutoka sekta rasmi yanayofikia kati ya asilimia 30 hadi 40, ikiwa na maana kuwa kodi nyingi za nyumba, maghala, hoteli zinapotea.
Kuhusu ufanisi wa ukusanyaji wa mapato, Rais amesema ni mdogo licha ya takwimu kuonyesha makusanyo ya kodi yanaongezeka kila mwaka jambo linaloirudisha nchi nyuma ikilinganishwa na Kenya ambayo inafanya vizuri katika kukusanya kodi zake.
“Nitoe mfano, mwaka 2013/14 wenzetu wa Kenya walipanga kukusanya Dola za Marekani bilioni 9.74 lakini walikusanya Dola za Marekani bilioni 9.64. Sisi katika mwaka huo tulipanga kukusanya Dola za Marekani bilioni 4.8 na tutakusanya Dola za Marekani bilioni 4.4,” amesema Rais.
Dk Magufuli hakuacha pia kuzungumzia kodi kubwa wanayotozwa wananchi hasa kodi ya majengo ambayo imesababisha wananchi wengi kukwepa kodi na kuikosesha Serikali mapato na hili linajidhihirisha katika idadi ndogo ya majengo yanayosajiliwa na kuingizwa katika mfumo wa kodi kila mwaka.
“Mathalani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita tumekusanya Sh74.5 bilioni na hapo wameniambia katika miezi sita iliyopita tumekusanya Sh8 bilioni na majengo yaliyosajiliwa mpaka sasa ni majengo milioni 1.6 hiki pia ni kichekesho,” amesema Rais akionyesha kushangazwa na idadi ndogo ya majengo yaliyosajiliwa ukilinganisha na idadi ya watanzania wanaofikia milioni 55.
Zinazohusiana:
Dk Magufuli ametuhumu ukwepaji wa kodi unaofanywa na wafanyabiashara wanaoshirikiana na baadhi ya wafanyakazi wa TRA wasio waaminifu ambao hutumia mwanya wa mawasiliano hafifu na mifumo ya makusanyo ya kodi ambayo haijaimarishwa kujipatia fedha zinazotakiwa kuingia katika mfumo rasmi wa Serikali.
Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli ameagiza kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kutengeneza mazingira ya ulipaji kodi, kupitia upya viwango vya kodi, taasisi za biashara na uwekezaji ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuondoa urasimu katika shughuli zao ili kuharakisha uwekezaji nchini.
Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere amesema mamlaka hiyo imefanikiwa kuunganisha mifumo ya kodi ya forodha na kodi za ndani ili kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato.
Amesema wataendelea kusisitiza nidhamu na maadili kwa wafanyakazi wa TRA ili kuziba mianya yote ya rushwa na kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unaongezeka kufikia malengo yanayowekwa na Serikali kila mwaka.
“Tunaendelea kukusanya kodi ya majengo ambapo mpaka sasa tumekusanya kiasi cha Sh8.8 bilioni wakati lengo likiwa shilingi bilioni 21 tuna uhakika tutafikia lengo la kukusanya kodi hii,” amesema Kichere.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema kama wizara watahakikisha wanasimamia matumizi sahihi ya mashine ya EFD, kutanua wigo wa ulipaji kodi kwa wananchi, kudhibiti misamaha ya kodi isiyo na tija na kurahisisha taratibu za kulipa kodi, ada na tozo mbalimbali.