Vijana waanika fursa zilizojificha katika matumizi ya mitandao ya kijamii
Jopo la vijana wakijadiliana wakati wa mkutano wa Fursa kwa Vijana uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Picha| Jalilu Zaidi.
- Mitandao ni majukwaa ya kubadilishana uzoefu na fursa mbalimbali ambazo vijana wakizitumia vizuri zitawasaidia kuboresha maisha yao.
- Wamehimizwa kushughulikia changamoto zilizopo katika jamii kwa kutumia teknolojia rahisi itakayowasaidia kuboresha maisha yao.
- Kwa vijana wanaotaka kuajiriwa wametakiwa kuwa na nidhamu ya muda na kutafuta ujuzi na maarifa ya msingi yanayohitajika katika soko la ajira.
Dar es Salaam. Mitandao ya kijamii ni fursa ya kujumuika na kubadilishana uzoefu wa mambo mbalimbali. Lakini ni zaidi ya hapo inaweza kutumika kama nyenzo ya kupata ajira na kuboresha maisha ya vijana ambao wanaotumia teknolojia.
Paschal Masalu, mwanzilishi wa jukwaa la mtandaoni la Elimika Wikiendi amenufaika na uwepo wa mitandao ya kijamii kutoa elimu na kuipa jamii inayomzunguka maarifa mbalimbali kila jumamosi kupitia mtandao wa Twitter, lengo likiwa kuelimisha na kukuza lugha ya Kiswahili.
Akishirikiana na wenzake Badru Rajabu na Dickson Kamala hawakuishia mtandaoni, waliandaa mkutano wa vijana ili kuwakutanisha vijana sehemu moja na kuzungumza lugha moja itakayowasaidia kupiga hatua katika maisha.
Mkutano huo ulipewa jina la fursa kwa vijana uliwakutanisha vijana zaidi ya 100 katika ukumbi wa ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) jijini Dar es Salaam wakiongozwa na vijana waliobobea katika sekta ya elimu, uongozi, biashara na ujasiriamali kuelimisha mbinu mbalimbali za kujikwamua kiuchumi na jinsi ya kuzitafuta fursa kwa vijana wanaochipukia katika teknolojia.
“Baada ya kuulizwa maswali mengi kuhusu fursa zinapatikanaje na kuona kiu ya vijana kujua tukaamua kuaanda hili jukwaa la fursa za vijana tuweze kuwakutanisha vijana ,” amesema Masalu.
Zinazohusiana: Fursa za mikopo, soko kuwanufaisha wakulima wa miwa Mbigiri
Wahitimu vyuo vikuu wakumbushwa kuchangamkia fedha za halmashauri
Katibu Mkuu Msaidizi wa kamati ya kimataifa ya vijana (International Youth Organization), Dk Hilda Jacob amesema vijana waliopo shuleni wanapaswa kuanza kujizoesha kufanya shughuli ndogo ndogo ambazo zinaweza kuwaingizia kipato wakati wakisubiri kuhitimu na kupata kazi rasmi.
“Tumia simu yako, kupata pesa, kufanya freelance (kazi binafsi) kwasababu tuna fursa nyingi kwa wanafunzi msisubiri mpaka mmalize shule,” amesema Dk Jacob.
Wametakiwa kuongeza ushirikiano utakawasaidia kupata ujuzi na maarifa ya msingi yanayoendana na ukuaji wa teknolojia ili wawe sehemu ya kutatua changamoto za jamii na kuboresha maisha yao.
“Tumia watu angalia tatizo ili kupata fursa na upate mtaji lakini kumbukeni kila mjasiriamali mmoja anahitaji zaidi ya watu watano wenye ujuzi katika nyanja tofauti tofauti,” amesema Jeniffer Shigoli, mjasirimali kutoka Malkia Investements Limited.
Pia vijana wamehimizwa umuhimu wa kuzitambua fursa zilizopo katika halmashauri zao ikizingatiwa kuwa zimeweka utaratibu wa kutenga asilimia tano ya mapato kwa ajili ya vijana na wanawake ili kuwakwamua kiuchumi.
Mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo amesema vijana waamke na wawashugulishe viongozi wa Serikali ili kubaini maeneo muhimu ya uwekezaji yanayoweza kuleta matokeo chanya katika jamii.
Mwegelo ambaye amekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya vijana amesema yuko tayari kufanya kazi na vijana katika wilaya yake hasa katika kutumia rasilimali muhimu za biashara na ardhi ya kilimo.
Kwa vijana wanaotaka kuajiriwa wametakiwa kuwa na nidhamu ya muda na kutafuta ujuzi na maarifa ya msingi yanayohitajika katika soko la ajira pamoja na kuongeza wigo wa marafiki wenye manufaa ndani na nje ya nchi.
“Vijana wanaopenda kuajiriwa lazima mjue vitu vitatu, kufanya utafiti wa kampuni au shirika unalotaka kwenda, pili kuwa na uwezo wa kujielezea kwa muda mfupi na kueleweka na mwisho kutunza muda,” amesema Michael Marwa, Mtaalam wa maswala ya watoto, kutoka shirika la Sema Tanzania.