Serikali kuanza kutumia mfumo mpya wa utumishi, mishahara Juni 2019
- Mfumo huo utaondoa changamoto za utendaji na utaboresha uwajibikaji na ufanisi wa watumishi wa umma serikalini.
- Serikali imesema itaendelea kutoa fursa za kupata mafunzo ya ndani na nje kwa wafanyakazi wake.
Dar es Salaam. Huenda utendaji na maslahi ya watumishi wa umma yakaboreshwa, baada ya Serikali kueleza kuwa ifikapo Juni mwaka huu itaanza kutumia mfumo mpya wa utumishi na mishahara unaokusudia kuimarisha uwajibikaji na uhusiano wa taasisi mbalimbali za Serikali.
Mfumo huo mpya utaunganisha mifumo mingine ya taasisi za Serikali yenye taarifa za kila mtumishi wa umma ili kuhakikisha unapunguza changamoto za watumishi hewa, wanaogushi vyeti na upotevu wa rasilimali fedha zinazotumika kwa wafanyakazi wasio na sifa.
Aprili 18, 2017, Rais John Magufuli aliagiza watumishi takribani 9,932 waliokutwa na vyeti vya kughushi waondolewe kazini baada ya kamati iliyoundwa ya kuhakiki vyeti vya watumishi wa umma kukamilisha kazi yake.
Maelezo hayo yametolewa bungeni leo (Januari 5, 2019) na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Mary Mwanjelwa wakati akijibu swali la mbunge wa kuteuliwa Janet Masaburi (CCM) aliyetaka kujua Serikali imejipanga vipi kikanuni kuwa na mfumo endelevu utakaokuwa madhubutu kwa uwajibikaji na uwajibishaji katika awamu zote zinazofuata.
Dk Mwanjelwa ambaye ameingia katika wizara hiyo hivi karibuni amesema Serikali imejipanga kuboresha mfumo mzuri zaidi tofauti na ule uliokuwa unatumika zamani ambao ulikuwa na changamoto mbalimbali za utendaji.
“Mfumo huu wa utumishi na mishahara wenyewe utakuwa na uwezo mkubwa sana wa kucapture (kuhusisha) taasisi zote umma nchini tofauti na ule ambao tunautumia sasa na ndiyo maana kumekuwa na malalamiko mengi,” amesema.
Zinazohusiana:
- Wanafunzi wa kike shule za kata wapata fursa ya kujifunza programu za kompyuta
- Vodacom, Google wazindua manunuzi ya ‘Apps’ kwa njia ya simu
- Kampuni ya Tanzania yashinda tuzo za ubunifu wa huduma za kifedha Afrika
Kupitia mfumo huo mpya uliobuniwa na kutengenezwa na vijana wa kitanzania utakuwa na uwezo pia kupata taarifa za kila mtumishi wa umma popote alipo.
“Mfumo huu tunategemea kuuanza rasmi mwezi wa sita mwaka huu ambao wenyewe utahusisha taasisi zote za umma na utaboresha hata mifumo ya utendaji kazi mingine,” amesema.
Katika hatua nyingine, Dk Mwanjelwa amesema Serikali itaendelea kuboresha utendaji wa watumishi wa umma kwa kutenga bajeti na kutoa fursa kwa wafanyakazi kupata mafunzo ya ndani na nje nchi ili kuongeza weledi na ufanisi.
Kwa mujibu wa Mwanjelwa, katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 watumishi 654 walipata mafunzo ya ujuzi na maarifa katika nchi washirika wa maendeleo za Austria, Japan, Indonesia, India, Jamhuri ya Korea na China.Mwaka uliofuata wa 2017/2018, idadi iliongezeka hadi kufikia 827.
Sera ya Menejimenti ya Ajira ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya 2008 kifungu 4(8), Sera ya Mafunzo katika Utumishi ya mwaka 2013 kifungo 4(2) na kanuni za kudumu katika utumishi wa umma za mwaka 2009 zinasisitiza mwajiri kuandaa mpango wa mafunzo kwa waajiriwa kulingana na mahitaji ya mafunzo.