Wanafunzi wa kike shule za kata wapata fursa ya kujifunza programu za kompyuta

Zahara Tunda 0336Hrs   Septemba 11, 2018 Teknolojia


Wanafunzi wakifanya kwa vitendo jinsi ya kufungua tovuti katika mafunzo yanayoendeshwa na Vodacom na DTBi, katika maabara ya Kompyuta Shule ya Msingi, Kijitonyama kisiwani. Picha| Zahara Tunda.

  • Lengo ni kuwafundisha watoto wakike wengi zaidi kuhusu masuala ya uandaaji wa programu za kompyuta na simu.
  • Vodacom yajitosa kushirikiana na DTBi kuwapa mafunzo hayo yatakayosaidia pia kutengeneza tovuti zao binafsi na wateja.
  • Watoto wakike washauriwa kutokuogopa masomo ya sayansi kwa kuwa ya nafursa zaidi.

Dar es Salaam: Baadhi ya wanafunzi wa kike wa shule za sekondari za kata Jijini Dar es Salaam wamepata fursa ya mafunzo ya kuandaa programu za kompyuta na simu hatua itakayowasaidia kwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano nchini. 

Mafunzo hayo yaliyoanza kutolewa kuanzia Septemba 10, 2018 na kampuni ya huduma za simu ya Vodacom na atamizi ya biashara na Teknohana (Dar Teknohama Business Incubator,(DTBi) ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) yamelenga kuwasaidia watoto wakike kujua hatua za mwanzo za kutengeneza programu za simu na kompyuta (coding) zikiwemo tovuti. 

Kwa kipindi kirefu, watoto wakike wamekuwa nyuma katika kuyapenda masomo hayo hasa  wale waliopo shule za sekondari za umma kwa kuona ni vitu vigumu kujifunza hali iliyotokana na ukosefu wa miundombinu rafiki ya kujifunzia kama kompyuta, maabara za kisasa na utayari wa mwanafunzi mwenyewe.

Mara baada ya mafunzo hayo siku tano yanayoishia Septemba 14, 2018  wanafunzi hao wataendelea kufuatiliwa wakiwa mashuleni ili waweze kuendelezwa zaidi ili kupata ujuzi unaotakiwa. 

“Lengo ni kumsaidia mwanafunzi wa kike kujifunza kutengeneza tovuti (Website), jinsi ya kutengeneza ukurasa wake binafsi na mambo muhimu ya kujifunza katika kufanya coding,” amesema Meneja Rasilimali Watu wa Vodacom, Emmaculate Mwaluko.

Hata hivyo, mafunzo hayo yamewalenga wanafunzi wa shule za kata, wenye umri wa miaka 14 hadi 18 ambao wameanza na wanafunzi 40 kutoka shule za sekondari Goba, Mabibo, Salma Kikwete, Makongo Juu na Turiani huku wanafunzi wakionyesha kufurahia mafunzo hayo na ari ya kujifunza zaidi.


Zinazohusiana: Michael Tumaini: Mwanafunzi wa shule ya kata aliyetengeneza ‘AC’, Power Bank ya simu

                            Umemejua unavyoboresha, afya, elimu Bagamoyo


“Nimejifunza mengi kwa somo hili la kwanza, nilikuwa sijui hata maana ya 'website' (tovuti) ndio nimejua leo,” amesema Felista Kihindo mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Mabibo.

Licha ya mradi huo kuonyesha dalili za mafanikio kwa kushawishi wanafunzi wa kike kuhudhuria, bado unakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kupata maabara za kompyuta za kuwafundishia wanafunzi na utayari mdogo wa walimu kuwaruhusu wanafunzi hao kuhudhuria mafunzo. 

“Nashauri walimu waruhusu wanafunzi nafasi kama hizi zikitokea kwani ilikuwa sio rahisi kuwapata wanafunzi kuja kujifunza,” amesema Mwaluko.

Baadhi ya walimu, wameeleza kuwa mafunzo hayo ni mazuri kwa wanafunzi wa ngazi zote hivyo ni vyema wadau wakajitolea kuhakikisha watoto wakike hawaachwi nyuma katika masuala ya sayansi na teknolojia.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kijitonyama Kisiwani, Charles Nombo aliyejitolea chumba cha maabara ya kompyuta kwa ajili ya mafunzo hayo ameiomba Vodacom na wadau wengine kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi wa shule ya msingi ili kuwajengea wanafunzi msingi mzuri wa teknolojia tangu wakiwa wadogo.

“Sayansi na teknolojia ni muhimu na hasa katika kuelekea uchumi wa kati, na mategemeo yangu Vodacom mtakuja hadi shule ya msingi,” amesema Nombo.

Related Post